07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Hukumu Za Kuangalia: Mwanamke Kuwaangalia Wanaume Wasio Maharimu Wake
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ وَأَحْكَامُ النَّظَرِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia
أَحْكَامُ النَّظَرِ
Hukumu Za Kuangalia
07-Mwanamke Kuwaangalia Wanaume Wasio Maharimu Wake:
Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, ni haramu kwa mwanamke kuangalia uso wa mwanaume asiye maharimu kwa matamanio. Na ikiwa bila matamanio na hakuna hofu ya fitnah, basi itajuzu. Sehemu zinazoruhusiwa kuangaliwa kwa kauli yenye nguvu ni zile zisizo kati ya kitovu na magoti ikiwa hakuna hofu ya fitnah. Hili linatiliwa nguvu na:
- Hadiyth ya ‘Aaishah:
"رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمًا عَلَى بَاب حُجْرَتِي، وَالْحَبَشَةُ يَلْعَبُونَ فِي الْمَسْجِدِ وَرَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَسْتُرُنِي بِرِدَائِهِ، أَنْظُرُ إِلَى لَعِبِهِمْ"
“Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku hiyo kwenye mlango wa chumba changu huku Wahabeshi wakicheza ndani ya Msikiti (kwa mikuki), Rasuli wa Allaah akanifunika kwa ridaa yake ili niweze kuwaangalia wanavyocheza”. [Al-Bukhaariy (455) na Muslim (892)].
Hadiyth iko wazi kwamba mwanamke anaruhusiwa kumwangalia mwanaume.
- Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Faatwimah binti Qays:
" فَاذْهَبِي إِلَى ابْنِ أُمِّ مَكْتُومٍ فَكُونِي عِنْدَهُ فَإِنَّهُ رَجُلٌ أَعْمَى تَضَعِينَ ثِيَابَكِ عِنْدَهُ"
“Basi nenda kwa Ibn Ummi Maktuwm uishi kwake, yeye ni kipofu, utaweza kuvua nguo zako huko (naye hawezi kukuona)”. [Swahiyh Muslim (1480)]
Hii ni dalili kwamba mwanamke anaruhusiwa kumwangalia mwanaume sehemu ambazo mwanaume haruhusiwi kumwangalia mwanamke. Ama uchi, hilo haliruhusiwi. [Al-Jaami’u Liahkaamil Qur-aan cha Al-Qurtwubiy (12/228)].
Kwa muktadha huu, dalili hizi mbili zinakuwa mahsusi kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ"
“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao”. [An-Nuwr: 31].
Lakini hata hivyo, mwanamke kuruhusiwa kumwangalia mwanaume kunashurutishwa kuwe bila matamanio, kusalimike na fitnah na iweko haja. Na hili halimaanishi kwamba anaruhusiwa kuchanganyika na wanaume ajaanib (wasio maharimu), kuangaliana nao uso kwa uso na kuzungumza nao bila uwepo wa haja. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.