06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Pambo La Meno
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo
الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ
Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu
06-Pambo La Meno:
Uislamu umehimiza kuyatunza meno, na kwa ajili hiyo, umesunisha kutumia mswaki.
Abu Hurayrah: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَوْلاَ أَنْ أَشُقَّ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ لأَمَرْتُهُمْ بِتَأْخِيرِ الْعِشَاءِ وَبِالسِّوَاكِ عِنْدَ كُلِّ صَلاَةٍ"
“Lau si kuhofia kuwafanyia uzito Waumini, ningeliwaamuru waicheleweshe ‘Ishaa na wapige mswaki wakati wa kila Swalaah”. [Al-Bukhaariy (887) na Muslim (252) na tamshi ni lake]
Ni Haramu Kupasua Mwanya Katika Meno
Hii inafanyika kuonyesha kwamba mtu ana umri mdogo au kwamba meno yake ni mazuri. Kufanya hivi bila kuwa kunahitajika kwa tiba ni haramu, kwa kuwa ni ubadilishaji wa uumbaji wa Allaah na kudanganya.
Rasuli (Swalla Allaah ‘Alayhi wa aalihi wa sallam):
"لَعَنَ الْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ لخَلْقِ اللَّهِ"
“Amewalaani wanawake wenye kupasua mwanya wa meno ili waonekane wazuri, hao wanabadilisha uumbaji wa Allaah”. [Al-Bukhaariy (4886) na Muslim (2125)]
Akifanya hivi kwa ajili ya matibabu, basi itaruhusiwa. Inaruhusiwa vile vile kuyakaza meno kwa dhahabu kama yatahofiwa kutoka, na pia kupandikiza meno na magego. Haya yote yanaruhusiwa kutokana na dharura. [Al-Mughniy (3/15,16)]