13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu:Pambo La Kutia Rangi
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ
Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo
الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ
Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu
13-Pambo La Kutia Rangi:
Haijuzu kwa mwanamke wala mwanamume kunyofoa mvi. Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"لاَ تَنْتِفُوا الشَّيْبَ، مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَشِيبُ شَيْبَةً فِي الإِسْلاَمِ إِلاَّ كَانَتْ لَهُ نُورًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ "
z
“Msinyofoe mvi, kwani hakuna Muislamu yeyote anayeota mvi akiwa ndani ya Uislamu, isipokuwa zitakuwa ni nuru kwake Siku ya Qiyaamah”. [Abu Daawuwd (4202) kwa Sanad Hasan]
Lakini, pamoja na katazo hilo, inaruhusiwa kuzitia nywele rangi njano au nyekundu. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى لَا يَصْبِغُوْنَ فَخَالِفُوْهُمْ"
“Hakika Mayahudi na Manaswara hawatii rangi nywele, basi wakhalifuni”. [Al-Bukhaariy (3462) na Muslim (2103)]
Kibora zaidi cha kubadilisha rangi nywele ni hina na “katam”. “Katam” ni majani ya mti wa salam (mimosa tree).
Abu Dharr:
"إِنَّ أَحْسَنَ مَا غَيَّرْتُمْ بِهِ الشَّيْبَ الْحِنَّاءُ وَالْكَتَمُ"
“Hakika kizuri zaidi mnachobadilishia kwacho rangi mvi, ni hina na katam”. [At-Tirmidhiy (1573), An-Nasaaiy (8/139) na Ibn Maajah (3622). Kuna mvutano kwenye Sanad yake]
Hina inajulikana na wote, na katam ni mmea ambao hutumiwa kutilia rangi.
Kutia nywele rangi nyeusi ni haramu. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoona nywele na ndevu za Abu Quhaafah nyeupe mithili ya hisopo siku ya ukombozi wa Makkah alisema:
"غَيِّرُوا هَذَا بِشَيْءٍ وَاجْتَنِبُوا السَّواد"
“Badilisheni hii kwa chochote, lakini epukeni nyeusi”. [Muslim (2102), An-Nasaaiy (5076) na Abu Daawuwd (4204)]
Inaruhusiwa Kupaka Hina Au Katam Wakati Wa Hedhi:
Toka kwa Mu’aadhah:
"أَنَّ امْرَأَةً سَأَلَتْ عَائِشَةَ: تَخْتَضِبُ الخَائِضُ؟ فَقَالَت: قَدْ كُنَّا عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَخْتَضِبُ، فَلَمْ يَكُنْ يَنْهَانَا عَنْهُ"
“Kwamba mwanamke mmoja alimuuliza ‘Aaishah kama mwenye hedhi anaweza kupaka hina (au rangi). Akasema: Tulikuwa tunapaka tukiwa na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hakuwa akitukataza hilo”. [Ibn Maajah (656) kwa Sanad Swahiyh]
Kadhalika, inaruhusiwa wakati wa twahara, lakini ni lazima aiondoshe akitaka kutawadha kama itakuwa inazuia maji kufika kwenye ngozi. Ibn ‘Abbaas amesema:
"كُنَّ نِسَاءَنَا يَخْتَضِبْنَ بِاللَّيْلِ، فَإِذَا أَصْبَحْنَ، فَتَحْنَهُ فَتَوَضَّأْنَ وَصَلَّيْنَ، ثُمَّ يَخْتَضِبْنَ بَعْدَ الصَّلَاةِ، فَإِذَا كَانَ عِنْدَ الظُّهْرِ، فَتَحْنَهُ فَتَوَضَّأْنَ وَصَلَّيْنَ فَأَحْسَنَّ خِضَابًا، وَلَا يَمْنَعُ مِنَ الصَّلَاةِ "
“Wake zetu walikuwa wakijitia hina (au katam) usiku, na wanapopambaukiwa wanaitoa, wakatawadha na kuswali, kisha baada ya kuswali hujitia tena. Inapofika adhuhuri wanaitoa tena, wakatawadha na kuswali, tena wanaitia vizuri kabisa, na haliwazuii hilo kuswali”. [Ad-Daaramiy (1093) kwa Sanad Swahiyh]