09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walioharamishwa Kwa Sababu Ya Kunyonya

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

09-Walioharamishwa Kwa Sababu Ya Kunyonya:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:  

 

"وَأُمَّهَاتُكُمُ اللَّاتِي أَرْضَعْنَكُمْ وَأَخَوَاتُكُم مِّنَ الرَّضَاعَةِ"

 

“Na mama zenu ambao wamekunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya”.  [An-Nisaa: 23]

 

Na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na binti ya Hamzah:

 

"إِنَّهَا لَا تَحِلُّ لِي، إِنَّهَا اِبْنَةُ أَخِي مِنْ اَلرَّضَاعَةِ، وَيَحْرُمُ مِنْ اَلرَّضَاعَةِ مَا يَحْرُمُ مِنْ اَلنَّسَبِ"

 

Yeye si halali kwangu, ni binti ya kaka yangu wa kunyonya, na lililo haramu kwa sababu ya kunyonya ni haramu pia kwa sababu ya nasaba” [Al-Bukhaariy (2645) na Muslim (1447)]

 

Kwa Hadiyth hii, tunapata kujua kwamba walioharamishwa kutokana na kunyonya ni wale wale walioharamishwa kutokana na unasaba.  Na pia, mwanamke mnyonyeshaji,  anawekwa daraja moja na mama mzazi, yaani anakuwa ni kama mama mzazi.  Hivyo basi, wanawake walioharamishwa kwa mwanaume kwa sababu ya kunyonya ni hawa wafuatao:

 

1-  Mwanamke aliyemnyonyesha, na mama yake mzazi (hawa wanakuwa ni mama zake).

 

2-  Mabinti wa mwanamke aliyemnyonyesha, ni sawa waliozaliwa kabla yake au baada yake (hawa watakuwa ni dada zake).

 

3-  Dada wa aliyemnyonyesha (huyu anakuwa ni khalati yake).

 

4-  Binti ya binti wa aliyemnyonyesha (huyu anakuwa ni binti ya dada yake).

 

5-  Mama ya mume wa mnyonyeshaji ambaye maziwa yake yamepatikana kutokana na mimba iliyotokana na mume huyo (mama huyo anakuwa ni bibi yake).

 

6-  Dada ya mume wa mnyonyeshaji (huyu anakuwa ni shangazi yake).

 

7-  Binti ya mtoto wa kiume wa mnyonyeshaji (huyu ni binti ya kaka yake).

 

8-  Binti ya mume wa mnyonyeshaji hata kama ni wa mke mwingine (huyu ni dada wa kunyonya kutokana na baba).

 

9-  Dada za mume wa mnyonyeshaji (hawa ni mashangazi zake).

 

10-  Mke mwingine wa mume wa mnyonyeshaji (huyu ni mke wa baba yake).

 

11-  Mke wa mtoto aliyenyonya ni haramu kwa mume wa mnyonyeshaji (huyu ni mke wa mtoto wake).

 

Kwa kuwa sababu ya uharamisho ni maziwa ambayo yanapatikana kwa mwanamke kutokana na mimba aliyoipata kutokana na mumewe.  Na mtoto anapoyanyonya, anakuwa ni sehemu ya sehemu za anayemnyonyesha.

 

Kati ya yanayoonyesha hayo, ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru ‘Aaishah amruhusu kuingia kwake Aflah kaka wa Abul Qa’iys ambaye ni ami yake wa kunyonya.  [Al-Bukhaariy (5103) na Muslim (1445)]

 

Imenukuliwa kwamba Ibn ‘Abbaas: 

 

"سُئِلَ عَنْ رَجُلٍ، كَانَتْ لَهُ امْرَأَتَانِ فَأَرْضَعَتْ إِحْدَاهُمَا غُلاَمًا وَأَرْضَعَتِ الأُخْرَى جَارِيَةً فَقِيلَ لَهُ هَلْ يَتَزَوَّجُ الْغُلاَمُ الْجَارِيَةَ؟ فَقَالَ لاَ، اللِّقَاحُ وَاحِدٌ"

 

“Aliulizwa kuhusu mtu mwenye wake wawili.  Mke mmoja akamnyonyesha mtoto wa kiume mtumwa na mwingine binti kijakazi.  Je, mtoto huyo anaweza kumwoa binti kijakazi?  Akasema hapana, kwa sababu mume ni mmoja”.  [Maalik (2/602), At-Tirmidhiy (1149) na wengineo kwa Sanad Swahiyh iliyoishia kwa Ibn ‘Abbaas]

 

Hii ndio kauli ya Maswahaba na Fuqahaa wote.  [Al-Ummu (5/34), Al-Badaai’u (4/3), Al-Mughniy (6/572), na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/53)]

 

12-  Ikiwa mwenye kunyonyeshwa ni binti, basi mume wa mwanamke mnyonyeshaji haruhusiwi kumwoa (huyu ni baba yake), na kaka wa mume wa mwanamke mnyonyeshaji (huyu ni ami yake), na baba yake (huyu ni babu yake).

 

Faida:

 

Uharamu unamhusu tu mtoto aliyenyonya na wala haumhusu yeyote katika nduguze.  Kwa mfano, dada yake wa kunyonya hawi ni dada wa kaka yake.  Qaaidah katika hili inasema:  “Walionyonya ziwa moja wanakuwa ni ndugu”.  Kwa mfano, kaka wa aliyenyonyeshwa ambaye hakunyonya naye ziwa moja, anaruhusiwa kumwoa binti ya mwanamke aliyemnyonyesha kaka yake, kwa kuwa binti huyu anazingatiwa kuwa ni ajnabiya kwake ingawa ni dada wa kaka yake kwa kunyonya.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share