15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Sifa Ya Nyonyesho Lenye Kuleta Umahram

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

15-Sifa Ya Nyonyesho Lenye Kuleta Umahram:

 

Je, ni lazima mtoto anyonye ziwa lenyewe (titi)?

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba maziwa ya mnyonyeshaji yanaleta umahram ni sawa mtoto akiyanyonya toka kwenye titi, au akakamuliwa kwenye chombo akanyweshwa, au akanyweshwa kwa mrija kupitia mdomoni au puani au kwa njia yoyote ile iwayo, muhimu tu maziwa yafike tumboni na yawe ndio lishe yake na chakula chake, yamshibishe, yaoteshe misuli na yakuze mifupa yake.   Na hii ni kwa neno Lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إِنَّما الرَّضَاعَةُ مِنَ المَجَاعَةِ"

 

“Nyonyesho lizingatiwalo, ni lile la (kushibisha) njaa ya mtoto”.  [Al-Bukhaariy (5102) na Muslim (1455)]

 

Ibn Hazm ana rai nyingine kuhusiana na hili.  Anasema kwamba kiini cha mtoto kuwa mahram kwa anayemnyonyesha ni kile kinachoitwa kunyonya.  Na kunyonya kunakojulikana na wote ni mtoto kulitia ziwa mdomoni na akanyonya maziwa.  Ama yule aliyekamuliwa maziwa, halafu akayanywa kwa kutumia chombo, au aliyekamuliwa kwenye mdomo wake akayameza, au maziwa yakachanganywa na mkate au chakula, hayo yote hayaleti umahram wowote!!

 

Ninasema:  “Haya ni madhehebu ya Al-Layth, Daawuwd na Adh-Dhwaahiriyyah.  Lakini kauli ya Jumhuwr ndio yenye nguvu zaidi, kwa kuwa linalozingatiwa ni mtoto kunyanywa maziwa na kuingia tumboni kwa njia yoyote ile.  Na kama atakunywa na maziwa yakaishia mdomoni tu halafu akayatema, basi maziwa hayo hayaleti umahramu.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Faida:

 

Msichana Bikra Akitokwa Na Maziwa Halafu Akamnyonyesha Mtoto Wa Kiume, Je, Mtoto Huyo Atakuwa Mahram Yake?

 

Mwanamke akitokwa na maziwa bila kuingiliwa, ni sawa akiwa bikra au amewahi kuolewa, basi maziwa yataleta umahram kwa mujibu wa Jumhuwr ya ‘Ulamaa.  Mtoto aliyenyonyeshwa na hao, atakuwa ni mtoto wao, kwa kuwa hayo ni maziwa ya mwanamke ambayo yanaleta umahram sawa na yale yaliyotokana na kujimaiwa, na maziwa ya mwanamke yameumbwa kwa ajili ya lishe ya mtoto.  Na hili ni jambo la nadra kutokea, na likitokea, basi umahram unabaki palepale.

 

 

Share