Imaam Ibn Baaz: Maana Ya Al-Kawthar Na Tofauti Yake Na Al-Hawdhw

 

 

Maana Ya Al-Kawthar Na Tofauti Yake Na Al-Hawdhw

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swali: Nini maana ya Al-Hawdhw Al-Mawruwd na ipi tofauti kati yake na mto wa Al-Kawthar?

 

Jibu: Al-Hawdhw Al-Mawruwd ni hodhi la Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) litakalokuwa katika ardhi (ya mkusanyiko) Siku ya Qiyaamah. Ama Al-Kawthar ni mto wa Jannah, unateremsha maji kupitia mifereji miwili kuja kwenye hodhi la ardhi (ya mkusanyiko) ambalo Allaah (سبحانه وتعالى) Alimuahidi Nabiy Wake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Watakunywa humo   Waumini katika Ummah wake. Nalo ni hodhi kubwa urefu wake ni (mwendo wa) mwezi mzima, na upana wake pia ni (mwendo wa) mwezi mzima. Watakunywa watu wa imaan, na atakaekunywa mara moja hatopata kiu tena milele. Vyombo vyake ni idadi ya nyota za mbingu, na maji yake yanateremka kutoka katika mto wa Al-Kawthar. Huo ndio ufafanuzi wa jambo hili.

 

Al-Hawdh liko katika ardhi na maji yake yanatoka Jannah (Peponi). Al-Kawthar ni mto uko Jannah na maji yake yanateremka kwenye hodhi hilo kupitia mifereji miwili kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa yatamiminika maji kwenye hodhi hilo Siku ya Qiyamah, na watakunywa Waumini katika Ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Naam.

 

Mtangazaji: Allaah Awabaarik. Je mnakusudia Ee Sheikh, kuwa ni ardhi hii ama ardhi ya mkusanyiko?

 

Sheykh: Ni ardhi inayojulikana yaani Ardhw Al-Mahshar (Ardhi ya mkusanyiko), naam.

 

Mtangazaji: Naam Allaah Awabaarik. Inamaanisha sio ardhi hii iliyopo sasa?

 

Sheikh: Hapana! Mto wa Jannah upo, Allaah Anasema:

 

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾

Hakika Sisi Tumekupa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Al-Kawthar (Mto katika Jannah). [Al-Kawthar (108:1)]

 

Nao ni mto mkubwa uko Jannah, na Siku ya Qiyamah utakuwa ukimimina maji ardhini kupitia mifereji miwili kwenye ardhi ambayo itabadilishwa Siku ya Qiyaamah, na watu watakuwa kwenye ardhi hiyo. Naam

 

[Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

 

 

Share