15-Malaika: Je, Tunaweza Kuwaona Malaika Katika Umbile Lao Halisi?
Malaika
15: Je, Tunaweza Kuwaona Malaika Katika Umbile Lao Halisi?
Haijawahi kuelezwa kwamba kuna yeyote katika umma huu ambaye amewaona Malaika katika umbile lao asilia isipokuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeye alimwona Jibriyl (‘alayhis salaam) mara mbili katika umbile lake asili Alilomuumbia nalo Allaah Ta’aalaa. Mara ya kwanza ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَقَدْ رَآهُ بِالْأُفُقِ الْمُبِينِ"
“Na kwa yakini (Rasuli) alimuona (Jibriyl) katika upeo wa macho ulio bayana”. [At-Takwiyr: 23].
Na ya pili ni:
"وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ ● عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ ● عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ"
“Na kwa yakini amemuona (Jibriyl) katika uteremko mwingine • Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa • Karibu yake kuna Jannah ya Al-Ma-waa”. [An-Najm: 13-15].
Ibn Kathiyr amesema: “Neno Lake Ta’aalaa: وَلَقَدْ رَآهُ بِالأُفُقِ الْمُبِينِ lina maana:
Kwa hakika Muhammad alimwona Jibriyl anayemletea Wahyi kutoka kwa Allaah ‘Azza wa Jalla katika umbile lake Alilomuumba nalo Allaah ‘Azza wa Jalla akiwa na mbawa mia sita katika upeo wa macho ulio bayana. Hii ilikuwa ndio mara ya kwanza huko Al-Batwhaa”.
Anaendelea kusema: “Jibriyl alikuwa anamjia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sura tofauti. Mara kwa sura ya Dihyat bin Khaliyfah Al-Kalbiy, mara nyingine kwa sura ya bedui, na mara nyingine katika umbile lake asili aliloumbiwa nalo. Ana mbawa mia sita, na kati ya kila mbawa mbili ni kama baina ya mashariki na magharibi. Alimwona katika umbile hili asilia mara mbili; mara alipokuwa anashuka toka mbinguni kuja ardhini, na mara nyingine kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa Rasuli alipopandishwa mbinguni”.
Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na Aayah hizi mbili. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"إنما هو جِبريلُ، لم أرَه على صورتِه التي خُلِقَ عليها غيرَ هاتين المرَّتَينِ، رأيتُه مُنهَبِطًا من السَّماءِ، سادًّا عِظَمُ خَلْقِه ما بين السَّماءِ إلى الأرضِ"
“Hakika huyo ni Jibriyl, sikuwahi kumwona katika umbo lake la asili isipokuwa mara hizi mbili. Nilimwona akishuka toka mbinguni huku mwili wake ukiziba sehemu yote baina ya mbingu mpaka ardhini”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (177)]
Naye Bi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) aliulizwa kuhusu Neno Lake Ta’aalaa:
"ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ"
“Kisha akakurubia na akashuka”. Akasema:
"إنما ذاك جبريلُ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، كان يأتيه في صُورةِ الرِّجالِ، وإنَّه أتاه في هذه المرَّةِ في صُورتِه التي هي صورتُه، فسدَّ أُفُقَ السَّماءِ"
“Hakika huyo ni Jibriyl (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam), alikuwa anamjia (Rasuli) katika sura ya mwanaume, na mara hii amemjia katika sura yake ambayo ndiyo ya asili, akaziba upeo wote wa mbingu”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (177)]