23-Malaika: Malaika Hawana Sifa Ya Jinsia Ya Kiume Wala Ya Kike

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

23:  Malaika Hawana Sifa Ya Jinsia Ya Kiume Wala Ya Kike

 

Mapagani wa Kiarabu walifanya makosa makubwa walipodai kwamba Malaika ni wanawake na ni mabanati wa Allaah kama Anavyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا ۚ أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ ۚ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ"

 

Na wakawafanya Malaika ambao ni Waja wa Ar-Rahmaan kuwa ni wa kike. Je, kwani wameshuhudia uumbaji wao?  Utaandikwa ushahidi wao, na wataulizwa”. [Az-Zukhruf: 19]

 

Na Anasema tena:

 

"أَصْطَفَى الْبَنَاتِ عَلَى الْبَنِينَ  مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ"

 

Je, Amekhitari mabanati kuliko wana wa kiume?  ●  Mna nini! Vipi mnahukumu?”  [Az-Zukhruf: 153-154]

 

Hilo ni kosa kubwa kabisa walilolifanya mapagani hao, kwa kuwa hawana dalili inayothibitisha madai yao hayo ambayo yamekwisha andikwa, na Siku ya Qiyaamah watakuja kuulizwa walete dalili na hawatakuwa nayo.  Hii ndiyo hatari ya mtu kudai jambo lolote bila ya kuwa na dalili nalo, ajue kwamba atakuja atakwe ushahidi wake Siku ya Qiyaamah.

 

Hivyo basi kuwasifu Malaika kwa jinsia ya kike ni ukafiri, na pia ni ukadhibishaji wa Qur-aan Tukufu.  Ama kuelezewa kuwa wana jinsia au maumbile ya kiume, jambo hilo halikuja kwa uwazi katika Qur-aan wala katika Sunnah.

 
Sa’iyd bin Al-Musayyib amesema:  “Malaika “Alayhimus Salaam si wanaume wala wanawake, hawazaani, na hawali wala hawanywi”.

 

Ibn Hajar amesema:  “Malaika si wanaume wala wanawake”.

 

Na ‘Aliy Al-Qaariy amesema:  “Malaika ni waja watakatifu, hawamtangulii Allaah kwa neno, bali maagizo Yake wanayatekeleza, wamelindwa na makosa na hawamwasi Allaah, na wametakaswa na sifa ya kuwa wanaume au wanawake”.

 

Ama kuwasifu kwa jinsia ya kiume, Allaah Ametumia vitenzi vya kiume katika Aayah zote zinazohusiana nao, ingawa katika baadhi Ametumia vinavyoashiria uke kama neno مُعَقِّبَاتٌ katika Kauli Yake:

 

"لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ"

 

“Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa Amri ya Allaah”.   [Ar-Ra’ad: 13]

 

Hili limefafanuliwa kitaaluma na Mufassiruna waliobobea lugha. 

 

Jibriyl (‘alayhis-salaam) alikuwa akimjia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa umbo la mwanaume kwa sura ya Dihyat Al-Kalbiy, au bedui, na hata aliwajia Maswahaba kwa picha hiyo hiyo wakati walipokuwa wamekaa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Na pia alikuja kwa umbo hilo hilo wakati wa vita vya Badr, na hata Malaika walioteremka kuwasaidia Waumini kwenye vita.  Na hata kwa Bi Maryam, Jibriyl alimwendea kwa umbo la mwanaume.

 

Makusudio ni kwamba wanawajia wanadamu kama Mitume kwa sura ya mwanaume na si ya mwanamke, na hao Malaika wanasifiwa kwa sifa za kiume na si kwa sifa za kike, na hii haimaanishi kwamba ni wanaume katika maumbo yao ya asili.  Pamoja na yote hayo, hakuna yeyote ajuaye namna walivyoumbwa, sifa ya maumbile yao na uhakika wa kuumbwa kwao isipokuwa Allaah Ta’aalaa. Yeye Pekee Ndiye Ajuaye undani na uchambuzi wa yote.

 

 

Share