33-Malaika: Aina Za Ibada Ambazo Malaika Wanazifanya: (4)- Kumwogopa Allaah
Malaika
33: Aina Za Ibada Ambazo Malaika Wanazifanya
(4)- Kumwogopa Allaah
Malaika wanamwogopa na kumkhofu sana Allaah, wao wanamjua Allaah vyema na wanamwadhimisha mno. Allaah Akiwazungumzia Anasema:
"يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ"
“Wanamkhofu Rabb wao Aliye juu yao, na wanafanya yale wanayoamrishwa”. [An-Nahl: 50]
Anasema tena:
"يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ"
“Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao, na wala hawataomba shafaa’ah (yeyote) isipokuwa kwa yule ambaye (Allaah) Amemridhia, nao kutokana na kumkhofu, ni wenye khofu na kutahadhari”. [Al-Anbiyaa: 28]
Anasema pia:
"وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ ۚ حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ"
“Na wala haitofaa shafaa’ah (uombezi) mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini. Mpaka litakapoondolewa fazaiko nyoyoni mwao husema: Amesema nini Rabb wenu? Watasema: Ya haki, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa”. [Sabaa: 23]
Ibn Kathiyr amesema: “Hili pia ni daraja la juu kabisa katika uadhwama, nayo ni kwamba Allaah Ta’aalaa Anapotamka wahyi, Malaika husikia Maneno Yake na hupatwa na mshtuko mkubwa unaofuatiwa na mfano wa kifo kutokana na kumwogopa Allaah”. Tamko hili limesemwa vile vile na Ibn Mas-‘uwd, Masruwq na wengineo.
Toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu): Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا قَضَى اللَّهُ فِي السَّمَاءِ أَمْرًا ضَرَبَتِ الْمَلاَئِكَةُ بِأَجْنِحَتِهَا خُضْعَانًا لِقَوْلِهِ كَأَنَّهُ سِلْسِلَةٌ عَلَى صَفْوَانٍ فَإِذَا فُزِّعَ عَنْ قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ قَالُوا الْحَقَّ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ"
“Allaah Anapopitisha amri mbinguni, Malaika Hupiga mbawa zao kwa ajili ya kulitii Neno Lake ambalo ni kama sauti ya mnyororo (unaoburutwa) juu ya mwamba. Na fazaiko linapoondoka nyoyoni mwao huuliza: Nini Amesema Mola wenu? (Malaika wabebao ‘Arshi) hujibu: Ni haki, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (4800)].