35-Malaika: Malaika Ni Wajuzi Wa Kutekeleza Kazi Zao
Malaika
35: Malaika Ni Wajuzi Wa Kutekeleza Kazi Zao
Malaika wana elimu na ujuzi wa mambo mbalimbali kwa mujibu wa kazi wanazokalifishwa na Allaah Ta’alaa. Allaah Ta’aalaa Anasema:
وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ● قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"
“Na Akamfunza Aadam majina yote (ya kila kitu), kisha Akavionesha mbele ya Malaika; Akasema: Niambieni majina ya hivi mkiwa ni wakweli ● Wakasema: Utakasifu ni Wako, hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Baqarah: 31-32]
Allaah Ta’aalaa Amewafunulia baadhi ya Malaika Wake elimu ambayo wanaihitaji katika majukumu Aliyowabebesha kama Malaika wanaosajili matendo ya binadamu. Malaika hawa ni lazima wayajue matendo yote mema na mabaya yanayomhusu mwanadamu pamoja na vipimo vyake, matamshi yao, mienendo yao na kadhalika. Ni lazima pia wajue lugha ili waweze kupambanua kati ya mema wanayoyasema watu au mabaya. Allaah Ta’alaa Anasema:
"وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ● كِرَامًا كَاتِبِينَ ● يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ"
“Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi (na kuchunga) ● Watukufu wanaoandika (amali). Wanajua yale myafanyayo”. [Al-Infitwaar: 10-12]
Malakul Mawt (Malaika wa kutoa roho) anajua wakati, saa, dakika, sekunde ya kuitoa roho ya kiumbe na mahala pa kufia kiumbe hicho. Kadhalika, ana utaalamu wa kibobezi wa kuitoa roho ya kafiri na roho ya Muislamu, kwani kuna tofauti kati ya roho mbili hizi, pamoja na viumbe vinginevyo. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ"
“Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa”. [As-Sajdah: 11]