32-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Sifa Ambazo Mke Na Mume Wanatakiwa Kuwa Nazo: Mume

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

 

الصِّفَاتُ المطْلُوْبَةُ في الزَّوْجَينِ

 

Sifa Ambazo Mke Na Mume Wanatakiwa Kuwa Nazo:

 

Alhidaaya.com

 

 

 

32:  Sifa Ambazo Inapendeza Mume Kuwa Nazo: Mume

 

1-  Awe ameshika dini:

 

Ni kwa Kauli Yake Ta’alaa:

 

"وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ"

 

“Na mtumwa Muumini ni bora kuliko mshirikina japo akikupendezeni”.  [Al-Baqarah: 221]

 

2-  Awe amehifadhi kiasi fulani Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla:

                                                                                                                            

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha mtu mmoja katika Maswahaba wake kwa Qur-aan kidogo aliyohifadhi.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5029) na Muslim (1425)]

 

3-  Awe na nyenzo za kuolea kwa aina zake mbili ambazo ni uwezo wa kujimai, na gharama za kuolea pamoja na kipato cha kuendeshea maisha.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewahimiza vijana kuoa wakati wanapokuwa na uwezo wa mahitajio ya ndoa.  Alimwambia Faatwimah bint Qays:

 

"وَأَمَّا مُعَاوِيَةُ فَصُعْلُوكٌ لاَ مَالَ لَه"ُ

 

“Ama Mu’aawiya, huyo ni masikini hohehahe, hana chochote”.  [Muslim (1480), An-Nasaaiy (3245) na Abu Daawuwd (2284)]

 

5- Awe mwenye muamala mwema kwa wanawake:

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuhusiana na Abu Jahm:

 

"أَمَّا أَبُو جَهْمِ فَرَجُلٌ لا يَضَعُ عَصَاهُ عَنْ عَاتِقِهِ، وَلكِنْ انْكِحِي أُسَامَةَ"

 

“Ama Abu Jahm, yeye ni mtu ambaye hashushi fimbo yake begani (yaani anapiga sana, au anasafiri sana), mwache Usamah akuoe”.  [Muslim (1480), An-Nasaaiy (3245) na Abu Daawuwd (2284)]

 

5-  Mwanamke afurahi akimwona:

 

Ili asipate hisia ya kichefuchefu na kupoteza hamu naye, lakini pia asije kukufuru neema anazopata toka kwa mumewe.

 

6-  Asiwe tasa:

 

Ni kwa Hadiyth zinazogusia fadhla ya kuwa na watoto.

 

7-  Alingane viwango na mwanamke:  

 

Ulingano huu ni mfanano na usawa katika aina hizi zifuatazo:

 

(a)  Ulingano wa dini:   Hili ni sharti muhimu la kuswihi kwa ndoa kwa makubaliano ya ‘Ulamaa.  Haifai mwanamke wa Kiislamu kuolewa na kafiri kwa ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa.

 

Lakini pia haitakikani kwa Muislamu kumwozesha binti yake mwema mtu fasiki, kwani Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ ۖ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ ۚ أُولَـٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ ۖ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ"

 

Kauli ovu inaendana na watu waovu, na watu waovu wanaendana na kauli ovu.  Na kauli njema inaendana na watu wema, na watu wema wanaendana na kauli njema.  Hao wametakaswa na tuhuma za wanayoyasema, watapata maghfirah na riziki karimu”.  [Nuur: 26]

 

Hili pamoja na ubaya wake, lakini halizuii kuswihi kwa ndoa.

 

2-  Ulingano wa nasaba:  Hili limetiliwa maanani sana na Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na Imaam Maalik.

 

3-  Ulingano wa mali.  Allaah Ta’aalaa Amesema: 

 

"الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ"

 

“Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao”.  [An-Nisaa: 34]

 

Hili limezingatiwa na ‘Ulamaa wa Kihanafiy, Kihanbali na Kishaafi’iy. ‘Ulamaa wa Kimaaliki hawajalizingatia hili.  Wanasema kwamba mali ni kitu kinachoweza kuondoka kama afya na kuja ugonjwa.  Hivyo basi, mwanamke mwenye uwezo wa mali, anaweza kuolewa na mume fakiri.

 

4-  Ulingano  wa uhuru:  (Yaani muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa kijakazi).  Limezingatiwa hili na Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik.

 

5-  Ulingano wa kazi:  (Mume mwenye kazi duni sana haendani na mwanamke mwenye wadhifa wa juu kama injinia au daktari).

Hili limezingatiwa kwa umuhimu mkubwa pia na ‘Ulamaa wa Kihanafiy, Kihanbali na Kishaafi’iy.

 

6-  Kusalimika na kasoro zozote mbaya. Ni kama ukoma, mbalanga, wendawazimu na kadhalika.

 

Lakini Je, Ulingano Huu Ni Sharti Ya Kusihi Kwa Ndoa?

 

‘Ulamaa wana kauli mbili kuhusiana na shurutisho la ulingano huu.  Kauli iliyo sahihi zaidi ni ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa akiwemo Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad, lakini pia imesimuliwa toka kwa ‘Umar na Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhumaa).  Kauli hii inasema kwamba ulingano si sharti ya kuswihi ndoa kwa mujibu wa dalili zifuatazo:

 

1-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha Zaynab binti Jahsh (toka ukoo mtukufu wa Asad) Zayd bin Haarithah (ambaye alikuwa ni mtumwa mwachwa huru wa Rasuli).  Kisa chao kimeelezewa katika Qur-aan Tukufu ambapo Allaah Anasema:

 

"وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّـهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّـهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ ۖ فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا"

 

“Na pale ulipomwambia yule ambaye Allaah Amemneemesha nawe ukamneemesha:  Mshikilie mkeo, na mche Allaah!  Na ukaficha katika nafsi yako ambayo Allaah Ametaka kuyafichua, na unakhofu watu, na hali Allaah Ana haki zaidi umkhofu.  Basi Zayd alipomaliza haja kwake Tukakuozesha”.  [Al-Ahzaab:  37]

 

2-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni wa ukoo wa Haashimiy, aliwaozesha mabinti zake wawili kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan ambaye ni Mquraysh.  Amesema (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَى كِنَانَةَ مِنْ وَلَدِ إِسْمَاعِيلَ، وَاصْطَفَى قُرَيْشًا مِنْ كِنَانَةَ، وَاصْطَفَى مِنْ قُرَيْشٍ بَنِى هَاِشِمٍ، وَاصْطَفَانِي مِنْ بَنِي هَاشِمٍ"

 

“Hakika Allaah Amewateua Kinaanah toka kwa watoto wa Ismaa’iyl, na Amewateua Maquraysh toka kwa Kinaanah, na Amewateua Baniy Haashim toka kwa Maquraysh, na Ameniteua mimi toka kwa Baniy Haashim”.  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim (2276) na At-Tirmidhiy (3605)]  

 

3-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha Usaamah bin Zayd (mwachwa huru) Faatwimah bint Qays ambaye ni Mquraysh.  Hadiyth kuhusiana na hili imeelezewa nyuma.

 

4-  Toka kwa Abu Maalik Al-Ash’ariyy, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَرْبَعٌ فِي أُمَّتِي مِنْ أَمْرِ الْجَاهِلِيَّةِ لَا يَتْرُكُونَهُنَّ: الْفَخْرُ فِي الْأَحْسَابِ، وَالطَّعْنُ فِي الْأَنْسَابِ، وَالِاسْتِسْقَاءُ بِالنُّجُومِ، وَالنِّيَاحَةُ"

 

“Mambo manne ya kijahiliya yako katika umma wangu, hawatoyaacha:  Kujifaharisha kwa hadhi, kudharau nasaba za wengine, kuomba mvua kwa nyota (kuitakidi kuwa ndizo sababu), na kuomboleza kwa malalamiko”.  [Muslim: (934) na wengineo]

 

5-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ"

 

Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu.  Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha katika Fadhila Zake.  Na Allaah Ni Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote”.  [An-Nuwr: 32]

 

Umasikini wa mposaji usiwe ndiyo sababu ya kumkatalia, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutengenekewa hali siku za mbeleni.

 

 

6-  Hadiyth ya Abu Sa’iyd:  Kwamba Zaynab, mke wa Ibn Mas-‘uwd alikwenda kwa Rasuli na kumwambia: 

 

"يَا رَسُولَ اَللَّهِ، إِنَّكَ أَمَرْتَ اَلْيَوْمَ بِالصَّدَقَةِ، وَكَانَ عِنْدِي حُلِيٌّ لِي، فَأَرَدْتُ أَنْ أَتَصَدَّقَ بِهِ فَزَعَمَ اِبْنُ مَسْعُودٍ أَنَّهُ وَوَلَدُهُ أَحَقُّ مَنْ تَصَدَّقْتُ بِهِ عَلَيْهِمْ، فَقَالَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: "صَدَقَ اِبْنُ مَسْعُودٍ، زَوْجُكِ وَوَلَدُكِ أَحَقُّ مَنْ تَصَدَّقْتِ بِهِ عَلَيْهِمْ".

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Hakika wewe umetuamrisha leo tutoe swadaqah, nami nilikuwa na kidani changu nikataka kukitoa.  Lakini Ibn Mas-‘uwd akadai kwamba yeye na wanaye wana haki zaidi ya kupewa swadaqah hiyo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Amesema kweli Ibn Mas-‘uwd.  Mumeo na wanao wanastahiki zaidi swadaqah yako”.  [Al-Bukhaariy (1462) na Muslim (1000)] 

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba Bi Zaynab alikuwa na hali nzuri zaidi ya kifedha kuliko mumewe Ibn Mas-‘uwd.

 

7-  Hadiyth ya Abu Hurayrah: 

 

"أَنَّ أَبَا هِنْدٍ، حَجَمَ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي الْيَافُوخِ، فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:‏"‏ يَا بَنِي بَيَاضَةَ، أَنْكِحُوا أَبَا هِنْدٍ وَانْكِحُوا إِلَيْه"

 

“Kwamba Abu Hind  alimuumika Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  katikati ya kichwa chake.  Na Rasuli akasema:  Enyi Bani Bayaadha!  Mwozesheni Abu Hind (banati zenu), na nyinyi oeni kwake (banati zake)”.  [Hadiyth Hasan.  Abu Daawuwd (2102), Al-Haakim (2/164) na Al-Bayhaqiy (7/136)]

 

Abu Hind hana uhusiano na Baniy Bayaadha, bali alikuwa mtumwa kwao kisha wakamwacha huru.  Lakini pia alikuwa ni muumikaji, na kazi hii ilikuwa ndiyo duni zaidi kuliko zote kwa wakati huo.

 

 

8-  Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: 

 

"اشْتَرَيْتُ بَرِيرَةَ فَاشْتَرَطَ أَهْلُهَا وَلاَءَهَا فَذَكَرْتُ ذَلِكَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: أَعْتِقِيهَا فَإِنَّ الْوَلاَءَ لِمَنْ أَعْطَى الْوَرِقَ.‏ قَالَتْ فَأَعْتَقْتُهَا، فَدَعَاهَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَخَيَّرَهَا مِنْ زَوْجِهَا فَقَالتْ: لَوْ أَعْطَانِيْ كذا وكذا مَا ثبتُّ عِنْدَهُ"

 

“Nilimnunua Bariyrah, lakini wanaommiliki walishurutisha kwamba fungamano lake libakie kwao.  Nikamweleza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallama) hilo naye akaniambia:  Mwache huru, kwa sababu fungamano linakuwa kwa yule aliyelipa pesa, nami nikamwacha huru.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwita na kumkhiyarisha kati ya kubaki na mumewe au kuvunja ndoa, naye akasema:  Hata akanipa nini sibaki naye”.    [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (2536) na Muslim (1504)] 

 

Mumewe alikuwa ni mtumwa, na Bariyrah baada ya kuachwa huru, akawa muungwana, ndiyo maana Rasuli akamkhiyarisha. Na kama mumewe angekuwa muungwana, basi Rasuli asingemkhiyarisha, bali angebakia kwa mumewe.

 

Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:

 

"فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: لَوْ راجعته، فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اللَّهِ تَأْمُرُنِي؟ قَالَ: إِنَّمَا أَشْفَعُ قَالَتْ: لَا حَاجَةَ لِي فِيهِ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Natamani lau ungelirejea uishi naye.  Akasema:  Je hiyo ni amri ewe Rasuli wa Allaah?  Akamwambia:  Hapana, bali ni ombi.  Akasema:  Sina haja naye”.  [Al-Bukhaariy (5283), Abu Daawuwd (2231), An-Nasaaiy (8/245) na Ibn Maajah (2075)]

 

9-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا جَاءَكُمْ مَنْ تَرْضَوْنَ دِينَهُ وَخُلُقَهُ فَأَنْكِحُوهُ، إِلاَّ تَفْعَلُوا تَكُنْ فِتْنَةٌ فِي الأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيْرٌ"

 

“Akiwajieni mnayemridhia dini yake na tabia yake, basi mwozesheni.  Na kama hamtofanya, basi utakuwepo mtafaruku na uharibifu mkubwa ardhini”.  [At-Tirmidhiy (1090) na wengineo.  Ina asaaniyd dhaifu, lakini matini nyingine za kisharia zinaipa nguvu]

 

Ahmad katika riwaayah yake mashuhuri, Ath-Thawriy na baadhi ya ‘Ulamaa wa Kihanafiy, wanasema kwamba ulingano wa viwango ni sharti.  Wametoa dalili ambazo baadhi yake hazijathibiti.  Ama zilizothibiti, hizo haziko wazi katika kushurutisha hilo, lakini pia hazina nguvu ya kupinga Hadiyth zilizotangulia.

 

Faida:

 

Ya kwanza:

 

Kwa wale wenye kushurutisha ulingano, haki hiyo inakuwa ni ya mwanamke na mawalii.  Kwa maana kwamba ikiwa mwanamke na walii wake wataridhia kutokuweko ulingano huo, basi ndoa ni sahihi.  Si Imaam Ahmad wala mwingine yeyote katika ‘Ulamaa aliyesema kwamba itakuwa ni batili.  [Zaadul Ma’aad (5/161) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/284)]

 

Ya pili:

 

Wengi katika wanaoshurutisha ulingano ili ndoa iswihi, wanaona kwamba ulinganio ni sharti lazimisho, kwa maana kwamba nikaha itakuwa ni lazima kama ulinganio upo, na kama itafungwa bila kuwepo ulinganio lakini kwa ridhaa ya mwanamke na mawalii, basi itaswihi.  Lakini kama mmoja wa mawalii hatoridhia, basi ndoa haitofungwa, itafutwa.

 

Ya tatu:

 

Ulingano unazingatiwa kwa mwanamume tu na si kwa mwanamke.  Ikiwa mtu atamwoa mwanamke ambaye harandani naye, basi hakuna tatizo, kwa kuwa usimamizi unakuwa mkononi kwake, watoto watanasibishwa naye, na talaka anaimiliki.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioa kwenye makabila tofauti ya Waarabu na hakuna aliye sawa naye kwa dini wala kwa nasaba, na pia alilala na vijakazi.  Na yeye anasema:

 

"مَنْ كَانَتْ عِنْدَهُ جَارِيَةٌ فَعَلَّمَهَا وَأَحْسَنَ تَعْلِيمَهَا وَأَحْسَنَ إِلَيْهَا، ثُمَّ أَعْتَقَهَا وَتَزَوَّجَهَا فَلَهُ أَجْرَانِ"

 

“Atakayekuwa na kijakazi, kisha akamfundisha na akamwelimisha vyema, na isitoshe akamtendea wema, halafu akamwacha huru na kumwoa, basi ana ujira mbili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (2544), Muslim (154).  Angalia Al-Mughniy (6/487), Al-Mabsuwtw (5/29) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/287)]

 

 

 

 

 

Share