01-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Akiutafuta Ukweli Kabla Ya Muhammad ( صلى الله عليه وسلم) kupewa Utume

 

 

01- Abu Bakr Asw  -Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu)

Akiutafuta Ukweli Kabla Ya Muhammad

(Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Kupewa Utume

 

Alhidaaya.com

 

 

Kabla ya kuja kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapakuwa na wanaomuabudu Allah isipokuwa watu wachache sana wakiwemo wafuatao:

 

Qussa bin Saaida

Zayd bin 'Amr

Waraqah bin Nawfal (aliyekuwa akifuata dini ya Kimasihi) na Abi Qays ibn Anas.

 

Hawa walikuwa wakisema wazi wazi kuwa wao wanamuabudu Allaah wa kweli Rabb wa Ibraahiym ('Alayhis-Salaam).

 

Ma-Quraysh hawakuwadhuru watu hao kwa sababu hawakuwa wakiitukana miungu yao, na pia kwa sababu walikuwa na wafuasi wachache sana waliokuwa wakiwaendea na kuwasikiliza.

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa wachache hao.

 

Alikuwa akihudhuria vikao vyao na kuwasikiliza wakizungumza juu ya Allaah wa kweli aliyekuwa akiabudiwa na Ibraahiym na Ismaa'iyl ('Alayhima-salaam), na juu ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye wakati wa kuja kwake umekwishawadia, na kwamba Mtume huyu ndiye atakayewarudisha watu katika ibada ya Allaah mmoja wa kweli.

 

Vikao hivyo ndivyo vilivyomsaidia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuiona nuru ya Utume kwa haraka, akawa anajitayarisha na kuisubiri.

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mfanya biashara marufu sana mwenye kujulikana kwa uaminifu wake hapo Makkah, heshima yake ilikuwa kubwa sana baina ya ma-Quraysh, na alikuwa mtu mwenye elimu kubwa ya kuhifadhi nasaba za makabila na mataifa ya Kiarabu, na kwa ajili hiyo alipewa yeye jukumu la kushughulikia mambo ya fidia panapotokea matatizo hayo baina ya makabila..

 

 

Share