15-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Siku ya Saqifa
Hii ni siku aliyofariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na baadhi ya watu wa Madiynah walijikusanya mahali panapoitwa Saqiyfat Bani Saa'dah karibu na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kufungamana na Swahaba mmoja katika watu wa Madiynah aitwaye Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kumchagua kuwa ni Khaliyfah wa Waislam.
'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), alipopata habari hizo alimwendea Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kumhadithia yanayotokea, na wote kwa pamoja wakifuatana na Abu 'Ubaydah 'Aamir bin Al-Jarraah (Radhiya Allaahu ‘anhu)wakaelekea huko.
Abu Bakr wala 'Umar hawakuwa na tamaa ya UKhaliyfah kama tutakavyoona, na hii ni kwa sababu walimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimkatalia 'Ammi yake Al-'Abbaas, alipomuomba ampe ugavana wa mkoa mmojawapo, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;
"Sisi Wa-Allaahi hatumpi utawala mwenye kuuomba wala mwenye kuung'ang'ania."
Na hii ni kwa sababu utawala, si neema wala raha hata mtu aung'ang'anie na kuutaka. Mwenye kuung'ang'ania utawala ni yule asiyeelewa jukumu lake, ama sivyo asingeutaka. Na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyajua hayo vizuri .
Wengi walibabaika baada ya kuzipokea habari za kifo cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na miongoni mwao ni watu wa Madiynah waliojikusanya mahali hapo panapoitwa Saqiyfat Bani Saa'idah, wakasema kuwa; lazima pafanywe haraka kumchagua kiongozi wa umma kabla hapajatokea machafuko, na wakataka kiongozi huyo atoke katika watu wao (awe mtu wa Madiynah), kwa sababu Madiynah ni mji wao, na kwa sababu ya fadhila zao nyingi katika kuunusuru Uislamu, na kwa ajili hiyo wakaamua kumchagua Swahaba huyo aitwaye Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Mara baada ya kuwasili mahali hapo, 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)akataka kuuhutubia mkusanyiko huo, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimvuta nyuma na kumuomba amwachie yeye akhutubie, akajisogeza mbele na kusema;
"Enyi watu wa Madiynah, hakika hapana fadhila itakayowezwa kutajwa bila ya kutajwa nyinyi ….", akaendelea kuwapa sifa zao walizostahiki, kisha akasema.
"Lakini Khaliyfah wa Waislamu atoke kwetu sisi watu wa Makkah".
Katika kitabu chake kitukufu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) daima hutanguliza kuwataja watu wa Makkah 'Al-Muhaajiriyn' kabla ya watu wa Madiynah 'Al-Answaar'.
Allaah Anasema;
"Na wale waliotangulia wakawa wa kwanza katika (Uislamu) Muhajiri na Ansari…".
At Tawba-100
Mmoja katika watu wa Madiynah aitwaye Al-Khabbab bin Mundhir (Radhiya Allaahu ‘anhu)akasema;
"Kwetu atoke Amiri na kwenu Amiri".
Akainuka Swahaba mwengine ambaye pia ni katika watu wa Madiynah aitwaye Bashir bin Mubaarak (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kusema;
"Enyi Al-Answaar (Watu wa Madiynah), ingawaje sisi tumeipigania dini hii kwa hali na mali, lakini haijuzu kwetu kujifanya bora kuliko wenzetu, sisi tulifanya hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah na kumtii Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatokana na kabila la ki-Quraysh, na watu wake ndio wanaostahiki kutuongoza. Allaah Asinijaalie nikapingana nao. Muogopeni Mola wenu enyi watu wa Madiynah na msiwaendee kinyume Al-Muhaajiriyn (watu wa Makkah)".
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), akaunyanyua juu mkono wa 'Umar na wa Abu 'Ubaydah 'Aaamir bin Al-Jarraah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kusema;
"Huyu 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuomba Allaah kutokana naye autukuze Uislamu, na huyu Abu 'Ubaydah ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsifia kuwa ni 'Mwaminifu wa Ummah huu', mimi nimeridhika (achaguliwe) mmoja kati yao, (awe Khaliyfah)"
'Umar aliuchomoa mkono wake kwa nguvu mfano wa mtu aliyeshika jinga la moto na Abu 'Ubaydah akasema;
"La wa-Allaahi! Nina khiyari nikatwe kichwa changu bila ya kutenda dhambi yoyote, lakini sikubali niwe kiongozi wa watu akiwemo Abu Bakr ndani yao. Ewe Abu Bakr, Mtume wa Allaah alikutanguliza wewe utuswalishe, na katika kila kubwa na dogo aliridhika na wewe, basi kwa nini na sisi tusiridhike na wewe? Utandaze mkono wako tufungamane nawe, ew Abu Bakr".
Akautandaza, na katika riwaya zilizo sahihi, wa mwanzo kufungamana naye alikuwa Bashir bin Mundhir ambaye ni mtu wa Madiynah, kisha 'Umar kisha Abu 'Ubaydah kisha wakamvamia Maswahaba wote mmoja baada ya mmoja wakifungamana naye (Radhiya Allaahu 'anhum).
Siku ya msiba mkubwa kupita yote iliyopata kuwatokea Waislamu ilimalizika kwa amani baada ya kuweza kuiondoa khitilafu iliyozuka baina yao, na baada ya kupata matumaini kwa kumuona Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyeshika hatamu, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapokuwa anaumwa au anapopatwa na udhuru wowote, alikuwa daima akimtanguliza Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuswalisha watu, kuongoza misafara ya Hajj na kusimamia mambo mbali mbali.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiumwa katika maradhi yake ya mwisho, alimchagua Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) awaswalishe watu, na bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa)alipojaribu kumtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumpa 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) jukumu hilo badala ya baba yake kwa sababu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mwingi wa kulia anaposwalisha, Mtum e(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikasirika akamwambia;
"Mwambie Abu Bakr aswalishe watu!"