21-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mkamuaji Maziwa
Kabla ya kupewa Ukhalifa, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akipenda kwenda kuwasaidia masikini na wazee na vilema, akiwapikia na kuwaoshea vyombo vyao na hata kuwakamulia maziwa.
Siku moja baada ya kuwa Khaliyfah wa Waislamu, alikwenda kuwatembelea baadhi ya wale masikini aliokuwa akiwatumikia, na mara baada ya kugonga mlango wa mojawapo ya nyumba hizo mtoto mdogo alifungua, na alipoulizwa na mamake ;
'Nani anayegonga mlango mwanangu?'
Mtoto akajibu;
'Mkamuaji maziwa amekuja, mama'
Mama alipomwona Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akastuka na kusema;
'Mwanangu, sema 'Khaliyfah wa Waislamu'.
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;
'Mwache, kwani ameniita kwa jina ninalolipenda kuliko yote'
Alikuwa akiwapenda masikini na akipenda kuwatumikia, na alikuwa akiwapenda watumwa na aliwakomboa wengi kwa mali yake.
Alimkomboa 'Amir bin Fuhayra, Zubayr, Ummu aAbsi na mwanawe, na wengi katika Maswahaba waliokuwa wakiteswa na makafiri wakati ule, na siku ile alipomkomboa Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliambiwa na kafiri aliyekuwa akimtesa na kumuadhibu;
'Ungeniambia huna isipokuwa vijisenti kidogo tu, basi ningekuuzia'
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;
'Wa-Allaahi ungelitaka hata riali mia za dhahabu basi ningelikulipa'.
Huyu ndiye Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mwingi wa huruma, mwingi wa kuona haya, hasa anaposifiwa mbele ya watu, alikuwa akisema;
"Mola wangu nijaalie niwe bora kuliko wanavyonifikiria na unisamehe kwa yale wasiyoyajua juu yangu na usinihisabie kwa wanayoyasema."
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema juu yake;
"Mwenye huruma kupita wote katika umma wangu Abu Bakr"
Imaam Ahmad na Ibni Habaan.