03-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumdhania mema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)

 
Kumdhania mema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)
 
Ni juu ya mja Muumini kumdhania mema Mola wake Mtukufu haswa zaidi ikiwa anakaribia kukutana nae Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) mimi ni mwenye dhana njema kwa mja wangu” (Bukhari na Muslim)
Vile vile katika hadithi nyingine Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Asife mmoja wenu ila awe ni mwenye dhana njema kwa Mola wake” (Muslim)
 
Katika jumla ya kumdhania vizuri Mola wako ni kuhisi ukarimu wake na fadhila zake, asimuhisi Mola wake kuwa ni dhalimu, bali amuhisi kuwa Mwenyezi Mungu anamtakia kheri katika maradhi yake hayo.
 
Mgonjwa katika hali yake ya maradhi azidishe khofu kwa Mola wake kwa madhambi aliyokuwa nayo na atarajie hali kadhalika rehema ya Mola wake Mtukufu. Khofu, matumaini na matarajio katika moyo wake ya kusamehewa madhambi pamoja na ulimi wake kuuharakisha kwa istighfaar na toba na dua kwa ajili yake ni sababu kubwa kabisa kuifanya dhana yake kwa Mola wake kuwa nzuri hivyo basi na Mola wake hawezi kuangusha dhana yake hiyo na matarajio yake kwake hivyo basi matokeo yake ni kuwa Mwenyezi Mungu nae atampa amani kwa anachokihofia.

Share