13-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Baadhi ya matendo yenye kumfaa maiti

 
Baadhi ya matendo yenye kumfaa maiti:
 
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Anapokufa mwana adamu amali zake zote zinakatika isipokuwa mambo matatu: sadaka yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha na mtoto mwema ambae atamuombea mzazi wake (baada ya kifo chake).” (Muslim)
 
Vile vile katika hadithi nyingine amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Hakika katika amali njema ambazo zitamfuatia muumini (baada ya kifo chake) ni mambo haya yafuatayo: elimu aliyoifundisha na akaieneza, mtoto mwema aliyemuacha au msahafu aliouacha kama mirathi au msikiti alioujenga au nyumba ya kupumzikia (wanakaa) walioharibikiwa safari, mto aliotengeneza njia yake au sadaka aliyoitoa kutoka katika mali yake alipokuwa na afya yake njema na pindi alipokuwa hai na baada ya mauti yake.” (Ameifanyia tahsiin Albani)
 
 
Hii ni mifano mizuri kabisa ya wema na sadaka yenye kuendelea. Mifano hii ina manufaa mengi katika maisha ya muumini na baada ya kifo chake.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Ni nani miongoni mwenu aliyepambazukiwa akiwa amefunga? Abubakar akajibu, ‘Mimi’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza tena, “Ni nani miongoni mwenu aliyeshuhudia Jeneza?” Abubakar akajibu, ‘Mimi’. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza tena, “Ni nani miongoni mwenu aliyelisha masikini?” Abubakar akajibu, ‘Mimi’ baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Hazikusanyiki amali njema hizi kwa mtu siku moja ila mtu huyo ataingia peponi.” (Muslim)
 
Hali kadhalika amesema tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Atakayeshuhudia jeneza kisha akaliswalia basi atapata Qiirati moja, na mwingine akalishuhudia hadi akazikwa atapata Qiirati mbili.” Pakaulizwa na hizo Qiirati mbili ni nini? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “ni mfano wa milima miwili mikubwa” (Bukhari na Muslim)
 
Katika riwaya nyingine “ kila Qiirati moja ni sawa na mlima Uhud”  
 
 Milango ya kheri ni mingi sana mfano ya milango hiyo ni katika swala, kutoa sadaka, kufanya dhikri tofauti, kuhiji kwa mwenye uwezo, kwenda kufanya Umra (ziara au hija ndogo), kuwafanyia wema wazazi wako wawili, kuunga udugu (kuwatembelea ndugu na kuishi nao vizuri), kupigana jihadi, kujifunza na kufundisha na kadhalika katika kheri kuna milango zaidi ya hii na Mwenyezi Mungu ameahidi watu kulipwa mema.
 
Share