29-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumkafini na kumpamba maiti
Kumkafini na kumpamba maiti:
Baada ya kumkosha maiti kinachofuatia ni kumpamba, kwa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliyoisema, “Atakapomkafini mmoja wenu nduguye basi na ampambe.”
Kinachochungwa katika kumvisha sanda (kafini) maiti ni haya yafuatayo:
1. Fungu la mali ya maiti ndilo litumike katika jambo hili kama atakuwa amewacha mali.
2. Limsitiri kiwiliwili chake chote bila ya kufanyika kwa israfu.
3. Kitambaa chenyewe kiwe ni cheupe na kinapendeza kikiwa ni cha pamba.
4. Kutokuvishwa sanda katika vitu vilivyoharimishwa kama vile hariri, kwani hiyo ni haramu kwa mwanamume, kwa mwanamke ni halali katika hali ya kawaida lakini ikitumika kama sanda inakuwa ni katika israfu.
5. Maiti avishwe sanda kuanzia moja hadi tatu, haifai kuzidisha zaidi ya hapo. Inapendeza zaidi kuwa ni tatu tu.
6. Muhrim atakapokufa atazikwa kwa nguo zake mbili alizofia nazo.
7. Shahidi atazikwa kwa nguo zake alizofia nazo bila ya kukoshwa.
8. Sanda itakapokuwa ni ndogo na fupi basi kichwa cha maiti kitasitiriwa na kutawekwa katika miguu yake majani ya idhkhir au majani mengine yoyote.