33-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Sifa ya swala ya Jeneza
Sifa ya swala ya Jeneza:
· Inapendeza idadi ya wenye kumswalia kuwa wengi na safu zikaongezeka nyuma ya jeneza.
· Atakayeongoza swala ya kumswalia maiti awe ni Imam au naibu wake au yule mwenye uwezo zaidi wa kusoma Qur’an, au awe mwenye kuijua Sunna zaidi au vinginevyo awe ni yule aliyekuwa mkubwa zaidi kwa umri.
· Inapendeza swala iwe nje ya msikiti karibu na anapoishi na hufaa ndani ya msikiti kwa haja.
· Imamu husimama usawa wa kichwa cha maiti mwanamume au katikati ya kiwiliwili (kiunoni) mwa maiti mwanamke.
· Jeneza huwekwa kiasi cha kuwa kichwa cha maiti huwa kuumeni mwa Imamu akiwa anaelekea Qibla.
· Imamu hunyanyua mikono yake katika takbira ya kwanza tu au katika takbira zote, na maamuma humfuata imamu wake.
· Imamu hunyanyua sauti yake kwa takbira, lakini maamuma hanyanyui sauti yake.
· Imamu baada ya takbira ya kwanza atasoma suratul Fatiha, ama baada ya takbira ya pili atamswalia Mtume kama ilivyo katika tashahhud, katika takbira ya tatu na ya nne atamuombea maiti dua maalum kisha atawaombea waislamu wote.
· Inapendeza dua zitakazosomwa ni zile ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) vinginevyo basi dua zozote zile zinazotaka maghfira na rehma kwa maiti.
· Akimaliza swala atatoa salamu mara moja tu kuumeni au akipenda atatoa salamu mbili.
· Inajuzu kuzidisha takbira na dua.
· Hakuna kurukuu na kusujudu katika swala ya jeneza na ni wajibu mtu kuchukua udhu wake.