39-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, maiti hulakiniwa majibu ya Malaika wawili?

 

Je, maiti hulakiniwa majibu ya Malaika wawili?

 

Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam): Kuwa maiti anapowekwa kaburini humjia malaika wawili wakali na humweka kitako na huanza kumhoji: ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako? Baada ya maswali hayo kila mja atajibu kulingana na maisha yake yalivyokuwa hapa duniani na Mwenyezi Mungu atawapa Ithbati wale wote waliokuwa wakimuamini yeye kwa kauli iliyo thabiti katika maisha haya ya dunia na huko akhera, na dhalimu atakuwa katika upotevu na Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo.

Maiti hanufaiki na Talqin ya walio hai kwake kama wanavyofanya wengine baada ya kuzika, mtu anasimama kaburini kisha anasema, ‘Ee, fulani bin fulani watakapokujia malaika wawili na wakakuuliza ni nani Mola wako, sema, Mola wangu ni Allah …’ jambo hili halikuthibiti kufanywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) au hata masahaba zake, lingekuwa ni jambo la kheri basi lingefanywa na hao wa mwanzo, maadamu hawakufanya basi atakayefanya atakuwa amefanya bid’a, na kila bid’a ni upotevu na kila upotevu ni katika moto. Hili si katika jambo ambalo litakalomnufaisha maiti. Hadithi iliyotangulia haina maelezo zaidi ya kumuombea na kumtaka awe thabiti katika kauli yake na sio kumlakinia kaburini.

Share