43-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, kunafaa kukusanyika kwa ajili ya Taazia?
Je, kunafaa kukusanyika kwa ajili ya Taazia?
Mkusanyiko wa namna hii haufai; sio makaburini au sehemu yoyote maalum kwa ajili ya tukio hilo. Ama baadhi ya watu wenye kutaka kheri katika jamaa za maiti husimama safu moja ndefu makaburini, na hivyo huja watu mmoja mmoja wenye kutoa mkono wa pole kisha wakawasalimia na kuwapa mkono wa pole wafiwa mmoja mmoja. Jambo hili pamoja na kuwa makusudiwa yake ni kuondosha bid’a ya kukusanyika majumbani kwa ajili ya taazia ila nalo ni katika makosa na hayajathibiti katika Sunna na hayakufanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) na hata wakati wa masahaba zake. Jambo hili lina ugumu katika utekelezaji wake kwani watu wa maiti katika kutekeleza kwake yawahitajia kusimama muda mrefu kusubiri mkono wa pole kutoka kwa waliohudhuria mazishi, hii ni taklifu ambayo haitakiwi waipate wafiwa. Linaloweza kufanyika ni kuwa watu hupeana pole popote pale penye wasaa bila ya taklifu kwa pande zote mbili.