60-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, Yafaa kusoma Qur’an Makaburini?
Je, Yafaa kusoma Qur’an Makaburini?
Hili ambalo halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), hakuliamrisha lakini aliamrisha tu kusomwa dua na kuwaombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakupenda watu wasome Qur’an makaburini kwa hadithi yake aliyosema, “Msizifanye nyumba zenu makaburi, kwani shetani hukimbia na huchukizwa na nyumba ambayo itasomwa surat Baqara.” Kadhalika haifai kuswali makaburini, hata ikiwa swala hiyo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Swalini nyumbani kwenu wala msizifanye nyumba zenu makaburi.” (Muslim) vile vile amesema, “mmoja wenu kukaa katika jiwe la moto akaunguza nguo yake na moto ule ukaingia katika ngozi yake ni bora kwake kuliko kukaa juu ya kaburi.” (Muslim) hali kadhalika amesema, “Msiswali makaburini na msikae juu yake.” (Muslim)