22-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Nia Zinazopaswa Kuwekwa Na Wanandoa
Wote wawili, mume na mke waingie katika ndoa kwa kuwa na nia zifuatazo:
Kujiweka huru katika kutimiza matamanio ya jimai na kuhifadhi nafsi zao kutumbukia katika yale Aliyoyakataza Allaah سبحانه وتعالى (yaani uzinifu). Juu ya hivyo wanaandikiwa thawabu kama thawabu ya sadaka kila mara wanapojimai. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ifuatayo iliyotoka kwa Abu Dharr:
أَنَّ نَاساً مِنْ أَصْحَابِ النَّبِيِّ قَالُوا لِلنَّبِيِّ : يَا رَسُولَ اللّهِ ذَهَبَ أَهْلُ الدُّثُورِ بِالأُجُورِ. يُصَلُّونَ كَمَا نُصَلِّي. وَيَصُومُونَ كَمَا نَصُومُ. وَيَتَصَدَّقُونَ بِفُضُولِ أَمْوَالِهِمْ. قَالَ: ((أَوَ لَيْسَ قَدْ جَعَلَ اللّهِ لَكُمْ مَا تَصَّدَّقُونَ؟ إِنَّ بِكُلِّ تَسْبِيحَةٍ صَدَقَةً. وَكُلُّ تَكْبِيرَةٍ صَدَقَةٌ. وَكُلُّ تَحْمِيدَةٍ صَدَقَةٌ. وَكُلُّ تَهْلِيلَةٍ صَدَقَةٌ. وَأَمْرٌ بِالْمَعْرُوفِ صَدَقَةٌ. وَنَهْيٌ عَنْ مُنْكَرٍ صَدَقَةٌ. وَفِي بُضْعِ أَحَدِكُمْ صَدَقَةٌ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللّهِ، أَيَأْتِي أَحَدُنَا شَهْوَتَهُ وَيَكُونُ لَهُ فِيهَا أَجْرٌ؟ قَالَ: ((أَرَأَيْتُمْ لَوْ وَضَعَهَا فِي حَرَامٍ أَكَانَ عَلَيْهِ فِيهَا وِزْرٌ؟ فَكَذٰلِكَ إِذَا وَضَعَهَا فِي الْحَلاَلِ كَانَ لَهُ أَجْرٌ))
Baadhi ya Maswahaba wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم walimwambia: 'Ee mjumbe wa Allaah, wakwasi miongoni mwetu wamechukua thawabu (za Aakhirah). Wanaswali kama tunavyoswali, wanafunga kama tunavyofunga na wanatoa Sadaka kutoka ziada ya mali zao'. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Kwani Allaah Hakukujaalieni na nyinyi kuweza kutoa Sadaka? Hakika kila mara mkisema 'Subhaana-Allaah' (Ametakasika Allaah) ni Sadaka, na kila mkisema 'Allaahu Akbar' (Allaah ni Mkubwa Zaidi) ni sadaka, na kila mara mkisema 'AlhamduliLlaah' (Sifa zote ni za Allaah) ni Sadaka, na kila mkisema 'Laa Ilaaha Illa Allaah' ni Sadaka, na kuamrisha mema ni Sadaka, na kukataza maovu ni Sadaka na katika uhusiano wenu wa kujimai ni Sadaka)). Maswahaba wakasema: 'Ee Mjumbe wa Allaah, je, kuna thawabu ikiwa mmoja wetu atajitosheleza matamanio yake ya kujimai?' Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Je, hamuoni kwamba ikiwa atajitosheleza kwa yaliyo haramu si ingelikuwa ni dhambi juu yake? Basi, vile vile atakapojitosheleza (kujimai) kwa njia ya halali atapata thawabu))[1]
[1] Muslim, An-Nasaaiy katika "Al-Ishraah" na Ahmad