Ufafanuzi Kuhusu Bid'ah Nyenzo Na Nyongeza Za Maswahaba Na Mataabi'iyn Sio Bid'ah?

 

Ufafanuzi Kuhusu Bid'ah Nyenzo Na Nyongeza Za Swahaba Na Mataabi'iyn Sio Bid'ah?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu Aleikum,

 

I live in the U.K and I really apologise that i could only speak and read but not clearly write in the Swahili language. I am very impressed with your website and the teachings of Islam through Quran and Sunnah. My question is regarding the word 'bid'a'. I am very confused about it as the Islamic scholars have two different opinions for it, those totally against it and those who have divided it into two categories, good and bad quoting the hadith of Umar bin Khatab of Taraweeh prayer  for their proof when he said "what a good bid'a". These scholars also say if every thing is regarded as bid'a then things like, compilling Quran into a book, carpets in the mosque, loud speakers in the mosque, driving cars, using computers and so on are all bi'da. Furthermore they also say something does not become prohibited in Islam unless there is a clear verse or hadith doing so like loud dhikr and dancing. Can you please reflect on these?

 

Assalamu Aleikum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Naona itakuwa ni vyema mada au swali hili tulieleze kwa kina kupitia kwa vipengele fulani. Baadhi ya vipengele vya Bid’ah ni kama vifuatavyo:

 

 

1. Kila bid’ah ni Dhwalaalah.

Kilugha Bid’ah ni kitu chochote kipya au kitu ambacho hakijafanywa kabla, yaani, hakina mfano kabisa wa mbeleni. Katika muono wa kishari’ah, kila Bid’ah ni Dhwalaalah na hakuna Bid’ah hasanah au sayyi-ah (Bid’ah nzuri na mbaya). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth, “Kullu Bid’atin dhwalaalah wa kullu dhwalaalatin fin naar.” (Kila Bid’ah ni Dhwalaalah (upotevu) na kila Dhwalaalah ni motoni)” [Imepokewa na Imaam Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na wengineo].

 

 

Dhwalaalah ina maana ya kwenda kombo au kufuata njia ya upotevu na kwenda kinyume na ukweli. Tukitazama Qur-aan, tutaona vipi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametumia neno hilo ‘dhwalaalah’ au ‘dhwaal’. Neno hili linatumika kwa mtu anayefanya dhambi au anafanya kosa katika mambo ya kidini lakini na pia linatumika kwa wale watu ambao wamepotea kutoka kwa njia nyoofu au wale walioigawa dini. Kwa mfano katika Suwraah Al-Faatihah (Suwraah ya kwanza), neno lililotumika ni ‘Dhwaalliyn’ halikutumika kwa wafanyao madhambi pekee lakini limetumika kwa watu waliopotea kutoka kwa ile njia ya sawa, yaani Wakristo. Hivyo pale Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoielezea bid’ah, alitumia neno kali sana kwa upotevu huo, yaani dhwalaalah, kama alivyosema, “Kulla bid’atin dhwalaalah” (kila bi’dah ni dhwalaalah)”. Hakusema kuwa kila bid’ah ni dhambi au ni kosa lakini kwa hakika ni jambo ambalo ni kubwa kuliko hilo. Huu ni upotevu, jambo ambalo linamtoa mtu katika Swiraatul Mustaqiym (njia ilinyooka).

 

 

2. Bid’ah inafanywa kama njia ya kumridhisha na kuja karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Kwa maneno mengine, yeyote anayefanya bid’ah, anadai kwa kufanya hivyo atakua karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hii ni tofauti kabisa na kufanya dhambi kama alivyosema Imaam Ahmad bin Hanbal, “Mkosefu mkubwa (faasiq) katika msimamo wa Ahlus-Sunnah Wal Jama’ah ni bora kabisa kuliko mchaji Allaah miongoni mwa Ahlul-Bid’ah (watu wa Bid’ah)”. Mwenye kufanya dhambi (mkosefu), kwa uchache, anajua ya kwamba chochote afanyacho ni makosa na wala hadai kuwa hilo ni halali na kuwa analifanya ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hata hivyo, yule anayefanya bid’ah sio tu anakwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah lakini bado anadai ya kwamba anayofanya ni sawa na anafanya hivyo ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ni njia ya kumleta karibu zaidi Naye (Allaah). Na huu ni uwongo mkubwa zaidi ambao mtu anafanya kwa kusema kuwa kitendo hiki kinamridhisha Allaah na hana dalili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa dai lake hilo.

 

 

Hivyo, sehemu ya wazo hili la bid’ah ni kuwa yule mwenye kufanya hudai kwamba linakubaliwa na dini pamoja na Shari’ah na ni lenye kumpendeza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hii ndio nukta inayogawanya baina ya bid’ah na jambo lisilokuwa bid’ah.

 

 

3. Bid’ah inaweza kuwa kuanzisha kitendo kipya na pia kukibadilisha kitendo kilichokuwepo mwanzo.

 

Maana yake ni, pale mtu anapoanzisha kitendo kipya huku akidai kuwa kitendo hicho kimekubaliwa na Shari’ah bila dalili yoyote ni bid’ah. Kwa namna hiyo hiyo, pale mtu anapoacha kitu fulani akidai kuwa kwa kuacha kitu hicho basi anamridhisha Allaah na hana dalili yoyote kutoka kwa Qur-aan au Sunnah, hiyo pia inakuwa bid’ah. Kwa mfano, wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuja watu watatu katika nyumba zake na kuwauliza wakeze kuhusu ‘Ibaadah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), walipoelezewa waliona ni kama kidogo sana. Hivyo wakajipangia jinsi watakavyofanya ‘Ibaadah zao, mmoja akasema yeye ataswali usiku kucha bila kulala, na mwengine akasema yeye atafunga kila siku bila kuacha, na wa tatu akasema kuwa yeye hatooa kamwe. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoambiwa habari hiyo aliagizwa waitwe na kuwauliza je, ndio nyinyi mliosema kadhaa na kadhaa nao wakajibu ndio. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya haraka kuzikemea na kuzikataza bid’ah hizi ambazo zinaonekana ni nzuri (huenda sisi tukadhania na kufikiria je, kutakuwa na makosa ya mtu kumuabudu Allaah kwa wakati wote?). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaeleza hawa watu kuwa yeye anamcha Allaah zaidi kuliko wao na ana taqwa ya daraja ya juu lakini anaswali usiku na kulala, anafunga na kula na ameoa wake (si mke mmoja). Na akamalizia kwa kusema yeyote atakayekengeuka na Sunnah zangu basi si katika mimi (yaani si pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Hadiyth hii imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].

 

 

Hapa ukitazama katika watu hawa watatu, wawili wa kwanza walikuwa tayari kuongeza ‘Ibaadah zao zaidi na zile ambazo zipo katika shari’ah na wa tatu akataka kuacha ‘Ibaadah ya ndoa ambayo ipo katika shari’ah na iliyokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Huyu wa tatu alikuwa ataka kujifananisha na makasisi wa Kikiristo au watawa wao na pia kama Masufi Waislamu ambao wanadai ya kwamba wanafanya hivyo kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na huu ukawa ni uzushi na kinyume na Uislamu.

 

 

4. Kila kitu katika Shari’ah kinaweza kuwa na bid’ah inayotengenezwa au kuhusiana nayo.

 

Shari’ah imejumlisha itikadi, ‘Ibaadah na biashara au mu’amalah na watu. Hivyo, bid’ah si mambo katika itikadi pekee au mambo ya ‘Ibaadah lakini inaweza kuwa hata katika biashara na mu’amalah. Kwa mfano, ikiwa mtu atadai ya kwamba kunahitajika mashahidi wanne katika mapatano ya kibiashara na wala sio wawili kama ilivyowekwa na Uislamu hivyo atakuwa amechupa mipaka ya kishari’ah na kuangukia katika bid’ah.

 

 

5. Bid’ah haina dalili katika Qur-aan, Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala haikukubaliwa na Ijmaa’ (kongamano) ya Swahaba.

 

Mfano maarufu ambao unatajwa na watu wa bid’ah (Ahlul-Bid’ah) katika yale matamanio yao ya kufanya aina fulani za bid’ah ziwe halali, ni ule mfano wa ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuifanya Swalah ya taraawiyh itekelezwe kwa Jama’aah. Wanadai ya kwamba ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alianzisha taraawiyh ya kila siku katika Ramadhwaan ambapo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitekeleza hilo kwa muda wa siku 3 pekee, na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema ya kwamba ameanzisha bid’ah nzuri, tunaweza kukubali fikra hii ya bid’ah. Hata hivyo, huku ni kufeli (kushindwa) kutofautisha baina ya maana ya bid’ah kilugha na maana yake ya ki-istilahi (yaani maana ya kishari’ah).

 

 

Kwa mfano Allaah katika Qur-aan anatuelezea kuhusu Sunnah Zake. Bila shaka ni kuwa yeyote anapotaja kuhusu Sunnah, inarudi kwa Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vipengele vyake vya kishari’ah. Hivyo hivyo, pale ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipotaja neon hilo bid’ah katika hizi Swalah za taraawiyh za kila siku, alikuwa anamaanisha ile maana yake ya kilugha. Dalili ya dai hili lipo wazi kabisa. Swalaah ya taraawiyh haikuwa ni jambo geni katika Dini. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alianzisha Swalaah hizi, na sababu ya pekee iliyomfanya yeye aache inaelezwa wazi katika Hadiyth zake ya kwamba hataki Ummah wake upate shida kwa Swalah hiyo kufanywa faradhi. Hata hivyo, alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), risala ya Uislamu ilikuwa imekamilishwa na Swalaah ya taraawiyh itakuwa daima ni yenye kuhimizwa kwa kiasi kikubwa na wala sio faradhi. Hivyo, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alianzisha tu kitendo ambacho tayari kilikuwa ni Sunnah na wala sio kuanzisha Sunnah. Na pia ile sababu ya kutoswaliwa kwa Jama’aah iliondoka baada ya kuaga dunia kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo hakukukuwa na aina yoyote ya uwezekano wa kuteremshwa wahyi. Na matendo ya makhalifa waongofu pia ni katika Sunnah. [Tazama Hadiyth nambari 28 katika kitabu al-Arba‘iyna an-Nawawiyyah].

 

 

Ummah huu haushirikiani katika jambo la upotevu. Hasa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa na ujasiri mkubwa sana wa kuweza kukemea jambo lolote ambalo halipo katika Dini. Na ndio katika shughuli kama hizo ukamkuta ‘Abdullaah bin Mas‘ud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipowakuta watu katika Msikiti na vijiwe na huku wanaleta dhikri kwa pamoja aliwakemea na kuwakataza hilo. Hili la taraawiyh lipo wazi kabisa na halina utata kwani lilifanywa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pindi pindi ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoihuisha Sunnah hiyo katika ukhalifa wake ilikubaliwa na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wote na hakuna aliyelipinga jambo hilo. Na kuafikiwa na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wote bila kupingwa ni miongoni mwa chimbuko la Shari’ah.

 

 

Ama kuhusu ukusanyaji wa Qur-aan ni kama Swalaah ya taraawiyh kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na waandishi wake waliokuwa wakiandika Qur-aan kama ilivyokuwa ikiteremka. Haikuandikwa katika kitabu kimoja kwa sababu kila siku Aayah zilikuwa zikiteremka na ingekuwa vigumu kuandikwa kila siku. Lakini ilivyokamilika kuteremshwa na baada ya muda wa siku chache Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaaga dunia ikaonekana haja ya kuandikwa katika kitabu kimoja katika ukhalifa wa Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kukubaliwa na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wote bila pingamizi yoyote.

 

 

Kuhitimisha sehemu hii ya majibu haya, ni lazima ieleweke ya kwamba bid’ah si jambo tu jipya ambalo limeanzishwa katika Dini kwa dai la kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini kwa yule mwenye kuanzisha na yule mwenye kufuata bid’ah kwa hakika anatuhumu ya kwamba Dini ina upungufu. Hakika ni kuwa wao wanatuonyesha ya kwamba zipo njia za kuja karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na kumridhisha ambako hakupatikani katika Qur-aan au Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kuwa wao wana njia ya kuamini au kufanya ‘amali na kumuabudu Allaah ambako kunampendeza Yeye na njia nzuri zaidi kuliko zile zilizofundishwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwamba hii Dini ya Uislamu iliyokamilika ina upungufu na hiyo ndio sababu iliyowafanya wao kuongeza baadhi ya vitu. Vilevile ni kumaanisha wao kuwa Dini hii ina vitu vingi sana na hiyo ndio sababu ya wao kupunguza baadhi ya mambo. Huku (Na’udhubiLlaah) ni kumtusi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kusema ya kwamba hakuweza kumkamilishia na kumfundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia bora na hivyo ilibidi watafute wao wenyewe njia nzuri. Hii ni kukana kauli ya Allaah mwenyewe katika Qur-aan:

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3].

 

Imaam Maalik (Imaam wa ardhi ya Hijrah) alisema: “Yeyote atakayezua katika Uislamu bid’ah ambayo anaiona ni nzuri amedai ya kwamba Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya khiyana katika kufikisha ujumbe, kwani Allaah aliyetukuka Anasema:

 

"Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu".

 

Hivyo chochote ambacho hakikuwa Dini wakati huo hakiwezi kuwa Dini sasa”. [Mwisho wa maneno ya Imaam Maalik].

 

 

Na huko ni kukana kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"Hakuna kitu ambacho kitakuleta karibu na Allaah kuliko yale niliyowaambieni kufanya na hakuna kitakacho wapeleka nyinyi mbali kuliko kufanya yale niliyowakatazeni kufanya".

 

 

Hivyo, tunatakiwa kuchukia bid’ah. Hiki ndicho kiini cha mambo. Uchukivu huu ni kuonyesha mapenzi yetu kwa Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia kuipenda Dini hii ambayo tunajua na kuwa na yakini kuwa ndio iliyo sahihi kabisa na itabaki hivyo mpaka siku ambayo Allaah Ataibadilisha ardhi hii kwa nyengine.

 

 

Ama kuhusu mazulia na vipaaza sauti Msikitini, kuendesha magari, kutumia kompyuta na teknolojia nyingine haya si mambo ya Bid‘ah katika Dini ambayo shari’ah imeyakataza, haya ni mambo ya Bid’ah ya kidunia ambayo shari’ah hayajayakataza kuwepo wala kutumika.

 

 

Kuhusu Mus-haf na I’iraab – Qur-aan ilikuwa imehifadhiwa katika vifua vya Swahaba ambao walikuwa ni wenye lugha ya Kiarabu fasaha, kwa hiyo hawakuhitaji I’iraab. Ilipotokea haja ya kukusanya Qur-aan katika mus-haf kwa vile Swahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuliwa katika vita vya Yamaamah, Maswahaba wakaingiwa na khofu ya kupotea Qur-aan kabisa hata isiweze kutufikia sisi na vizazi vyote hadi siku ya Qiyaamah. Ndipo ilipokusanywa baada ya ushauri mzito baina ya Makhalifa na Maswahaba na wakakubaliana kuikusanya katika Mus-haf.

 

 

Hata hivyo, kukawa vile vile hakuna haja ya kuweka I’iraab kutokana na ufasaha wa lugha ya Kiarabu. Ilipofikia zama za Yuusuf bin Hajjaaj, khofu iliingia ya kutowezekana kuisoma Qur-aan inavyopasa kwa vile lugha ya Kiarabu ilianza kupotea ufasaha wake. Kwa hiyo jambo kama hili lilikuwa ni jambo lililohitajika kufanyika ili kuendeleza ibada ya kuisoma Qur-aan na kupata mafunzo yake, na khaswa kwamba Qur-aan ni uongofu wa ulimwengu mzima, hivyo hata ambao si Waarabu waweze kuisoma baada ya kuweka I’iraab/harakaat/tashkili, la sivyo ingelikuwa vigumu kusomeka kwa wasiojua lugha ya Kiarabu sawa sawa.

 

 

Ama kuhusu nyenzo kama vipaza sauti, njia za usafirishaji, vifaa vya utamaduni vya kujifunzia na kadhalika vyote hivyo ni nyenzo tu za kutuwepesishia kutekeleza ibada zetu na yote yanayotupasa katika amri za Dini. Kuchanganya nyenzo na ibada ni jambo lilisilokuwa la mantiki. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Mjuzi wa mambo yasiyoonekana Amejua yote hayo kuwa yatatokea. Mfano kuhusu usafiri Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amejua kwamba watu watatoka kila pembe ya dunia kufika Makkah kutimiza Hajj, sasa vipi mtu ategemee kuwa usafiri wa nchi ya kutoka Kaskazini kufika Kusini asafiri na mnyama ilihali kuna magari, ndege n.k.? Bila shaka haingii akilini jambo hili.

 

 

Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametambua shida za usafiri zitakazotokea kutokana na umbali wa nchi na nchi ndio Akasema:  

 

وَالْأَنْعَامَ خَلَقَهَا ۗ لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ﴿٥﴾وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ﴿٦﴾وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَىٰ بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُوا بَالِغِيهِ إِلَّا بِشِقِّ الْأَنفُسِ ۚ إِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿٧وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً ۚ وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴿٨﴾

 

Na wanyama wa mifugo Amewaumba. Mnapata humo (sufi, ngozi za kutia) ujotojoto na manufaa (mengineyo) na miongoni mwao mnawala. Na mnapata humo jamala wakati wa mnaporudisha jioni na mnapopeleka machungani asubuhi. Na wanabeba mizigo yenu kupeleka nchi msizoweza kuzifikia isipokuwa kwa mashaka ya nafsi. Hakika Rabb wenu bila shaka ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. Na farasi na baghala na punda ili muwapande na wawe mapambo. Na Anaumba msivyovijua. [An-Nahl: 5-8].

 

 

Tusivyovijua ndio kama njia za usafiri za kisasa kama magari, ndege, matreni na kadhalika [Aysarut-Tafaasiyr Shaykh Abu Bakr Al-Jazairy: 3: 102].

 

 

Si kuendesha gari tu bali zipo ishara za kuendesha hata ndege angani. Tazama Anayosema Allaah Aliyetukuka kuhusu hilo:

 

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا ۚ لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ ﴿٣٣﴾

Enyi jamii ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye zoni za mbingu na ardhi, basi penyeni. Hamtoweza kupenya isipokuwa kwa mamlaka (ya Allaah). [Ar-Rahmaan: 33].

 

 

Hii ni ishara ya kwamba wanadamu wanatakiwa watafute mbinu za kuweza kusafiri katika ardhi kwa njia mbali mbali. Allaah Aliyetukuka pia Anatueleza kuwa:

 

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ

Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika nchi kavu na baharini,.. [Al-Israa: 70].

 

 

Hivyo, vyombo vya usafiri vyote vimo katika kukubaliwa na Dini yetu. Katika safari ya Israa na Mi’iraaj, Allaah Aliyetukuka Anatuonyesha miujiza Yake ya kumchukua Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sehemu ndogo ya usiku. Hii ni ishara ya kwamba upo uwezekano wa usafiri kuwa sahali na hili ni jambo ambalo tunalishuhudia sasa.

 

 

Ama kompyuta ambayo siku hizi inatumika kurahisisha mawasiliano baina ya watu ni jambo ambalo linapendekeza katika Uislamu. Kwani chombo hicho kinatumika kukupasha habari na shughuli nyingine nzuri.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia Ametupatia ishara ya uwezekano wa mawasiliano kuwa sahali kwa mmoja au mwingine pale Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-salaam) alipomtumia ndege, Hud Hud kufikisha ujumbe (barua) kwa Malkia wa Sabaa huko Yemen kwa haraka (tizama 27: 28 – 31).

 

 

Allaah Aliyetukuka Ametupatia ishara ya watu wa kale waliokuwa na teknolojia nzuri ya kuigwa na kupigiwa mfano. Anasema:

 

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الْأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا 

Je, hawatembei katika ardhi wakatazama jinsi ilivyokuwa hatima ya wale walio kabla yao? Walikuwa ni wenye nguvu zaidi kuliko wao, na walichimbua ardhi, na wakaistawisha zaidi kuliko walivyoistawisha (makafiri), [Ar-Ruwm: 9].

 

 

Hivyo, kuiimarisha na kuistawisha ardhi ni jambo linatakiwa na Uislamu kwa kutumia mbinu za kiteknolojia zozote ambazo zitaleta manufaa kwa wanaadamu.

 

 

Na mifano ni mingi ya kisayansi ambayo Qur-aan imeelezea kwa uwazi. Ndio Allaah Aliyetukuka Akawa Anataka tufikirie, tutumie akili, tuzingatie, tutafiti na mengineo ambayo yatakuwa ni yenye manufaa kwa wanaadamu wenyewe.

 

 

Kwa hiyo kila inapopatikana njia au kifaa bora cha kutusahilishia maisha yetu kinafaa kutumika na haiwi ni jambo la bid'ah katika Dini, bali unaweza kuita bid'ah kilugha kwani hivyo sio ibada iliyokusudiwa kuwa ni bid'ah kishari’ah.

 

 

Na tukitazama vitu hivyo vingine kama vipaaza sauti n.k. tutaona yanatokana na yale maslahi ambao watu wanapata na haipingani na kipengele chochote cha shari’ah. Tukisoma katika vitabu vya Siyrah tunamkuta Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Vita vya Hunayn akimwambia ‘ammi yake, ‘Abbaas bin ‘Abdil-Muttwalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anyanyue sauti kuwaita Muhaajirina na Answaar waje kwake na wajipange kwa ajili ya kukabiliana na Banu Hawaazin. Tunamkuta Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hijjatul Wada’ (Hijjah ya Kuaga) ambapo alitoa khutbah yake nzito Siku ya ‘Arafah akiwachagua baadhi ya Swahaba, akiwemo ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ili wawe ni wenye kuyarudia yale anayosema kwa watu wote wapate kusikia. Twafahamu kuwa katika mkusanyiko huo kuliwepo Swahaba takriban laki moja. Hii ni ishara ya wazi kuwa vipaaza sauti Msikitini au kwengineko kunaruhusiwa ili yatimu maslahi ya kuwa kila mmoja atasikia na kupata faida kwa khutbah ya Ijumaa, darsa au mawaidha.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share