Mke Wangu Hasemi Na Mimi Kwa Sababu Sitaki Kusherehekea Birthday Ya Mtoto Wetu
Mke Wangu Hasemi Na Mimi Kwa Sababu Sitaki Kusherehekea Birthday Ya Mtoto Wetu
Alhidaaya.com
SWALI:
Asalamu Alaykum ndungu waislamu.
Mke wangu ni muislamu na mimi mwenyewe ni muislamu nashkuru Alhamdullillahi na Allaah katujaalia tumepata mtoto mmoja na ni wa kwanza. Suala ni hili mke wangu anajua wazi kama kusherehekea siku ya kuzaliwa haifai ingawaje tumo baadhi ya waislamu mpaka leo tunasherehekea na hasa kwa watoto wetu tukijua wazi kama jambo hili halikubaliki ki maadili yetu ya kiislamu. habari ni hii mkewangu aliandaa sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mtoto wetu na akaalika watoto kama watatu jirani zake na yeye mwenyewe.Mimi Mumewe nilitoka tangu asubuhi nyumbani na shughuli zangu.ilipofika jioni kabla mimi kufika nyumbani nikapigiwa simu na mke wangu kua ananisubiri mimi ili nihudhurie katika sherehe hio ya mtoto wetu.mimi nikaona nisiende mpaka sherehe itakapokwisha na majirani kwenda zao ndio nirudi ili nisiwemo katika makosa hayo ya hio sherehe. niliporudi mke wangu alikua mkali mno na vilio kwa juu kahisi kua nimemdharau wito wake na kunitia mimi makosani ati sijali familia yangu.watu wote wanafurahika na familia zao na kufurahikia sherehe za kuzaliwa za wana wao lakini mimi sijali na nimemtia hasara kagharamika sana na picha za ukumbusho wa sherehe kwa vile mimi sikuepo haitoleta picha nzuri. sasa mimi binafsi kwa vile ni mwanamke na ana ghadhabu na hasira sijammjibu kitu wala sijamwambia kitu ila nimemuomba msamaha anisemehe na kasema itachukua muda mimi kunisamehe na mpaka sasa hasemi na mie. Sasa ninaloomba ni ushauri kutokwa kwenu Munisaidie jamani nimfahamishe vipi huyu mke wangu ili anifahamu na awache suala hili la kusherehekea siku ya kuzaliwa yeye binafsi na waislamu wengine wenye mwenendo kama huu. Ahsanteni nasubiri jibu kutoka kwenu Shukran.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Twataraji kuwa kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) shida hiyo itaondoka. Hakika ni kuwa matatizo yetu mengi ya kindoa yanatokea kwa sababu ya kutochukua maelekezo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Uchaguzi katika ndoa ni muhimu sana kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ametuhimiza tuchague mwanamke wa kuoa awe ni mwenye Dini, maadili na tabia. Na hilo haliwezi kupatikana mpaka uwe umefanya juhudi ya kuulizia kuhusu hayo kwa wanaomjua mpaka ukinaike kabisa kumhusu. Hili si jambo la kufanya haraka kwani huenda ukajuta baadaye.
Pia ni muhimu kabla ya kuingia katika ndoa afahamu kuhusu unavyotaka awe, ajue unayoyapenda na pia wewe ujue anayoyapenda. Katika kufanya hivyo utajua kama mnaweza kukaa vyema pamoja naye au la.
Uislamu umetuusia sana tuwatendee wema wake wetu na tuweze kuwachukulia kwa zile kasoro zao walizonazo kwani hayo ndiyo maumbile yao. Lakini hizo kasoro zao ikiwa ni zinazokwenda kinyume na dini yetu, basi inawapasa wanaume waziwahi kuzirekebisha tokea mwanzo wa ndoa na kabla haujafika wakati akawa mwanamke mwenye amri ya kufanya atakavyo na mume asiweze kurekebisha maovu yanayotendeka nyumbani kwake: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Watendeeni wema wanawake, hakika wao wameumbwa kutokana na ujongo (mbavu ambazo zimepinda). Na hakika sehemu iliyopinda zaidi ni ile ya juu, hivyo ukijaribu kuinyoosha itavunjika na ukiiacha itabaki na ukombo wake. Hivyo nawausieni muwafanyie wema wanawake" [Al-Bukhaariy na Muslim].
Mfano pia ni usemi wetu 'Udongo upate ungalimaji'
Katika maelezo yako umetuelezea kuwa ulimuomba msamaha mkeo na hili kwa hakika lilikuwa ni kosa upande wako. Hiyo itakuwa kwake ni hoja nzito kuwa wewe ulikosea katika suala la kutokwenda katika sherehe hiyo. Mbali na kuwa tumeamriwa kuwa wapole, laini na wenye huruma kwa wake zetu lakini inatakiwa tuwe madhubuti na imara inapokuja mas-ala ya kutofanya yanayokwenda kinyume na Dini yetu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia kwa kutuambia:
"Hakuna twaa kwa viumbe, katika kumuasi Muumba".
Japokuwa linalotakiwa kwako wewe kufanya ili kurudisha uhusiano mwema na mkeo ni kujaribu kutafuta njia ya kumuelemisha pole pole katika mas-ala ya Dini. Mbinu ambazo unaweza kutumia inategemea kiwango chako cha Dini na chake pamoja na elimu ya Kiislamu. Kwa sababu hasira huenda zikachukua muda mrefu kupungua au zikawa zinachepuza kila leo ni vyema utumie hekima na njia muafaka. Kwa muono wetu tunaona mbinu zifuatazo zinaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa:
a. Ikiwa kiwango chake cha elimu ya Dini ni kidogo ni bora uwe unamzoesha kwenda katika darsa za kina mama wenye msimamo wa Sunnah. Hii itamuwezesha yeye kuweza kuongeza kiwango chake cha elimu na pia matendo na tabia yake itabadilika.
b. Au ikiwa ipo madrasa ya kina mama ukamuandikisha, ili apate elimu ya sawa.
c. Jaribu kumuhimiza mwanzoni kuwa anakwenda Msikitini siku ya Ijumaa ikiwa Msikiti wa sehemu mnayoishi inayo sehemu ya wanawake. Na ikiwa una fursa ukaenda naye itakuwa bora zaidi. Hii itamuwezesha kusikiliza khutbah na kutangamana na kina mama wenziwe.
d. Nunua kaseti, au kanda au VCD, au DVD za mawaidha ya mashaykh barabara na uwe ni mwenye kusikiliza naye au kuangalia pamoja. Ni busara awali kutonunua kaseti au kanda zenye kuzungumzia kuhusu birthday hadi kwanza aanze kuzoea na kuelewa mambo ya Dini.
e. Mara nyingi sherehe hizi zinafanywa kwa sababu wanawake wengi huwa na faragha na hawana ya muhimu ya kufanya, pia kwa sababu ya kutojua ubaya wake au kwa kufuata ada za watu wengine na kuziiga. Mchapishie makala hii ambayo iko Alhidaaya atambue ubaya wa kusheherekea siku ya kuzaliwa:
Historia Ya Keki Na Mishumaa Katika Kuadhimisha Siku Ya Kuzaliwa (Birthday)
f. Fanya juhudi kumshughulisha katika mambo yatakayomnufaisha na kuufaidisha Ummah huu wa Kiislamu.
g. Pata vitabu vya Dini hasa mwanzo kuhusu Imani, Itikadi, Ibaadah, mafunzo ya Qur-aan na Sunnah, Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Visa vya Rusuli (‘Alayhimus-salaam) umpatie asome na wakati mwengine msome pamoja.
h. Wakati mwengine toka naye matembezi kwa kuwazuru jamaa zako au jamaa zake, au wake au kutembea katika ardhi hii aliyotuumbia Allaah Aliyetukuka.
i. Tenga muda wa kuweza kukaa na mkeo ili mzungumze mambo tofauti katika Dini, maisha, na jaribu kufanya dhihaka naye katika mipaka ya Dini. Mtake shauri katika mambo ambayo unataka kufanya kwa maslahi ya familia yenu na rai yake ikiwa nzuri ifuate. Hili litamjenga na kuona kuwa unamjali. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliye ruwaza njema kwetu anatupatia kielelezo hicho pale alipokubali rai ya mkewe, Ummu Salamah Hind bint Umayyah (Radhwiya Allaahu ‘anha) katika Suluhu ya Hudaybiyah. Na mpongeze unapopoona kuwa amekufurahisha na nyamazia ukiona amekosea au mkosoe kwa njia nzuri ya hekima. Mpe nasiha kwa njia nzuri na kwa upole nawe ukubali nasaha yake unapokosea kwani kila mmoja anakosea. Ikiwa Msikiti uko mbali nawe unaswali nyumbani swali naye Swaalah za faradhi na hata za Sunnah kama Tahajjud kwa jamaa wewe ukiwa Imaam. Ikiwa Msikiti uko karibu na una sehemu ya wanawake nenda naye bega kwa bega.
Baada ya kujaribu yote hayo, na ukamuona kwamba bado hataki kubadilika na kujirekebisha kutenda yasiyopasa, basi muitie watu wenu katika jamaa zako au jamaa zake wanaojua dini au Shekhe wampe nasaha kwani mara nyingi mkaidi husikiliza nasaha kwa watu wengine kuliko aliyekaribu naye zaidi.
Tunatumai maelekezo haya yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutatua tatizo hilo lako na nasaha yetu kwako ni kuwa jitahidi kushikilia msimamo wako wa kukataza maovu katika nyumba yako kwani wewe ndiye mwenye mas-uliya na familia yako:
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ
Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah.. [An-Nisaa: 34]
Kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((كلكم راع وكلكم مسئول عن رعيته الإمام راع ومسئول عن رعيته والرجل راع في أهله وهو مسئول عن رعيته والمرأة راعية في بيت زوجها ومسئولة عن رعيتها))
((Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Imaam ni mchungaji na ataulizwa kwa anaowachunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. [Al-Bukhaariy, Muslim]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Akupe tawfiki katika hilo.
Na Allaah Anajua zaidi