Kujikinga Na Ushirikina Wa Uchawi Na Mauaji

 

Kujikinga Na Ushirikina Wa Uchawi Na Mauaji 

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam alaykum warahmtuLLAHI wabarakatu.

SWALI:Ikiwa familia au ukoo una mambo ya ushiriknia na wanafika kutoana vikoa au kuuwa kwa kutumia uchawi,pamoja na vitusho mbali mbali ambavyo huvionesha wazi.Je inafaa kwa mtu kufanya kifungo cha mwili.Na kama haifai Kwa mislamu anatakiwa afanyeji na yeye yumo katika familia kama hiyo?

Ahsanteni.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hapa inafaa tufahamishane kuwa ushirikina ni jambo ovu linamtia mtu motoni. Kwenda kwa wachawi, wapiga ramli ni katika ukafiri na ushirikina.

 

Uislamu haukupiga vita makahini, bali vile vile wanaokwenda kwao kuwauliza na kusadiki mazingaombwe yao, utabiri wao na upotofu wao. Kwa hiyo, Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Mwenye kumwendea mpiga bao (mpiga ramli) akamuuliza kuhusu jambo lolote, kisha akamsadiki aliyoyasema, hazikubaliwi Swaalah zake kwa siku arobaini" [Muslim].

 

Pia alisema:

 

"Mwenye kumwendea kahini na akamsadiki aliyoyasema, huwa amekanusha yale aliyoteremshiwa Muhammad" [al-Bazzaar kwa Isnadi iliyo sahihi].

 

Vile vile, Uislamu umepiga vita uchawi na wachawi, kwani Qur-aan inasema:

وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ 

Na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; [Al-Baqarah: 102].

 

Haya yamehesabiwa miongoni mwa madhambi makubwa yanayoangamiza. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Jiepusheni na maovu saba yanayoangamiza!” Wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni yapi hayo?" Akasema: “Shirki, uchawi …" [Al-Bukhaariy na Muslim]. Hakika ni kuwa uchawi ni ukafiri na shirki. Uchawi unampeleka mtu kutoingia Peponi kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Haingii Peponi mlevi chakari, wala mwenye kuamini uchawi wala mwenye kukata undugu" [Ibn Hibbaan].

 

Uislamu kuupinga ushirikina umefunga njia zinazotupelekea huko, mojawapo ni kufunga hirizi. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mwenye kuivaa hii (hirizi) huwa ameshirikisha" [Ahmad na al-Haakim]. Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mwenye kuvaa hirizi, Allaah Asimtimizie yake, na mwenye kutundika kaure, Allaah Asimhifadhi" [Ahmad na Abi Ya’la].

 

Ifahamike kuwa shirki ni dhuluma kubwa, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

...لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno! [Luqmaan: 13].

 

Shirki inafanya amali za mja zote zipomoke kama ambavyo hakufanya chochote katika amali nzuri. Hivyo, hii ni dhambi ambayo haisamehewi na Allaah kwa uzito wake mkubwa (tazama Qur-aan, 4: 48; 116).

 

Ni vyema pia tufahamu kuwa hakuna anayejua mas-ala ya ghaibu isipokuwa Muumba wetu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Wapo watu wanaofahamika kama waaguzi au wapiga ramli, bao, makahini au wachawi au maprofesa maji marefu au mnajimu maarufu Afrika Mashariki wenye kutumia joho la Dini na huku wakipoteza watu na kuwatapeli, na wengine wengi ambao wanadai kujua mambo ya ghaibu kwa kuongea kwao na maruhani au majini. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza wazi kabisa kuhusu hilo pale Aliposema:

 

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ 

Sema: Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye ghayb isipokuwa Allaah. [An-Naml: 65].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitangaza kuwa yeye hajui elimu ya ghaibu kama Qur-aan inavyotueleza:

 

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٨﴾

Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya khayr, na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini. [Al-A'raaf: 188].

 

Malaika na majini hawajui elimu ya ghaibu pia. Jibriyl (‘Alayhis-salaam) alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "…Hebu nipe habari ya Qiyaamah". Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mwenye kuulizwa si mjuzi kuliko mwenye kuuliza” [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anatoa habari kuhusu majini wa Nabii Sulaymaan (‘Alayhis- salaam) ambao walisema:

فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿١٤﴾

Kwamba lau wangelikuwa wanajua ya ghayb, basi wasingebakia katika adhabu ya kudhalilisha. [Sabaa: 14]

 

Ifahamike kuwa hakuna anayeweza kukudhuru au kukunufaisha na chochote. Jambo hili ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:

 

"Mjali Allaah naye Atakuhifadhi. Mjali Allaah utampata Yuko nawe. Ukimuomba muombe Allaah; ukitaka msaada taka msaada kwa Allaah. Na ujue kwamba hakika lau watu wote wakusanyike ili wakunufaishe wewe kwa jambo lolote, hawawezi kukunufaisha ila kwa jambo alilokuandikia Allaah; na walikusanyika ili wakunufaishe wewe kwa jambo lolote, hawawezi kukunufaisha ila kwa jambo alilokuandikia Allaah” [at-Tirmidhiy].

 

Kwa muhtasari, Muislamu haruhusiwi kufanya kifungo cha mwili, kuvaa hirizi, kutundika, kuweka matalasimu kwenye maduka au majumbani, au kwenda kwa wachawi ili wakuhifadhi na mambo mblimbali. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia mambo lau tutayafanya basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atupatie hifadhi dhidi ya uchawi na mazingaombwe. Hivyo ni vyema zaidi kutumia Aayah za Qur-aan na du‘aa alizotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kujikinga na uchawi aina yoyote.

 

Baadhi ya Aayah zilizotajwa ambazo tunaweza kuzisoma kwa ajili ya kujikinga ni kama zifuatazo:

 

1.     Suwrah Al-Faatihah (1).

2.     Suwrah Al-Baqarah (2): Ayah 1 – 5; 255 – 257 na 284 – 286.

3.     Suwrah Aal ‘Imraan (3): Ayah 1 – 2.

4.     Kusema: Hasbiya-Alllah laa ilaaha illa Huwa 'alayhi tawakkaltu wa Huwa Rabul-'Arshil-'Adhiwym.  (Mara saba).

5.     Suwrah Al-Kaafiruun (109).

6.     Suwrah Al-Ikhlaasw (112) – Mara tatu.

7.     Suwrah Al-Falaq (113) – Mara tatu.

8.     Suwrah An Naas (114) – Mara tatu.

9.     Kuwa na mpangilio wa kusoma Qur-aan kila siku kwani ni dawa kubwa.

 

Hizi ni Aayah unazofaa kuzisoma asubuhi na jioni. Ama kuhusu du‘aa ambazo ametufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni kinga ni kama zifuatazo:

 

1.     Du‘aa ya kutoka Nyumbani: Imepokewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Yeyote mwenye kusema – yaani pindi anapotoka nyumbani kwake; ‘Bismillahi Tawakkaltu ‘ala Llahi wala Hawla wala Quwwata illaa Billahi’ (Kwa jina la Allaah, nimemtegemea Allaah na hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allaah)’. Anaambiwa: ‘Umeongozwa na umelindwa na umeokolewa’. Shetani wakati huo humkimbia (humwondokea)" [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy na wengineo, na kusahihishwa na Ibn Hibbaan].

 

Ameongeza Abu Daawuud: "Anasema: - yaani shetani kumwambia shetani mwenziwe, Utamwezaje mtu ambaye ameongozwa na kulindwa na ambaye ameokolewa?"

 

2.     Du‘aa ya Kuingia Chooni: Hii ni du‘aa ambayo inamlinda mwenye kuisoma wakati yuko faragha yeye na mashetani chooni wasiwe ni wenye kumdhuru. Anapoingia mmoja wetu chooni anatakiwa aseme kama alivyotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Allaahumma Innii A‘udhu bika minal Khubuth wal Khabaa’ith (Ee Allaah! mimi najilinda kwako kutokana na mashetani wanaume na wanawake)"  [al-Bukhaariy na Muslim).

 

3.     Zipo du‘aa nyingine nyingi ambazo unaweza kuzitumia katika maisha yako. Zipo nyiradi za asubuhi na jioni. Kitu ambacho kinaweza kukusaidia katika hili ni kununua kijitabu kinachoitwa Hiswnul Muslim. Hicho ni kitabu chenye dua za kila kitendo na wakati. Pia unaweza kukisoma kitabu hicho chote hapa:

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

Humo zimo nyiradi za asubuhi na jioni ambazo ni muhimu sana na kinga kubwa ya Muislamu kumuepusha na kila shari. Tunakuwekea hapa kiungo hicho kwa wepesi wako:

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akulinde na Akuhifadhi na Atuhifadhi sote na wasiwasi wa shetani na Atuingize katika rehema Yake siku ya Qiyaamah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 
 
 

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٦٥﴾

Share