Kuoga Na Kufanya Wudhuu Nusu Saa Kabla ya Kufuturu

 SWALI:

Asalam Aleykum ndugu zangu waislam mlio huko nyumbani ,napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa jitihada zenu za kutujulisha na kutupa mawaidha na pia Dua njema katika mtandao huu wa Alhidaaya kweli nimefurahishwa sana na napenda kuwapa pongezi nyingi na nawatakia pia Ramadhan maqbul.

Swali langu ni hili:Je mtu kuoga na kuchukua udhu nusu saa kabla ya kufunguli muadhana je ni sawa?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 Tunaanza na shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaana wa Ta'aala)   Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Kutia wudhuu ni jambo linalopendekezeka kwa Muislamu awe katika hali ya wudhuu saa zote ikiwezekana. Kwani kubakia na wudhuu kuna faida kubwa kwa Muislamu kama kumuepusha na shaytwaan n.k. Hivyo kutia wudhuu saa yoyote ile hakuna ubaya hata kama mtu akiwa karibu na kufuturu, kwani hakuna dalili iliyokataza jambo hilo.

Hali kadhalika kuoga, hakuna ubaya kuoga wakati wowote wa Swawm hata kama kabla ya nusu saa au chini yake karibu na kufuturu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share