Fanya Biashara Na Allaah Isiyoanguka - Ramadhwaan Na Qur-aan

 

Fanya Biashara Na Allaah Isiyoanguka – Ramadhwaan Na Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾  لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ ﴿٣٠﴾ 

Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea. Ili (Allaah) Awalipe ujira wao timilifu, na Awazidishie kutokana na fadhila Zake, hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwingi wa kupokea shukurani. [Faatwir: 29-30]

 

Aayah hiyo ya mwanzo inajulikana kwamba ni 'Aaayatul-Qurraa' (Aayah wa wasomaji). Ni Aayah pekee katika Qur-aan inayojulikana hivyo. Anasema Shaykh Abu Bakar Al-Jazaairy katika kuifasiri kwake, kwamba: "Aayah hii inawahusu wale ambao wanaikhitimisha Qur-aan kila mwezi au chini ya mwezi". Na hivyo ndivyo Sunnah ilivyo kuikhitimisha Qur-aan kila mwezi kama ilivyo dalili katika usimulizi kwenye Al-Bukhaariy.

 

Biashara ya mwanzo ni kusoma Qur-aan. Biashara hii bila ya shaka itakuletea faida kubwa utakapoifanya mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan kwa vile ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ 

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185]

 

Vile vile:

 

حم﴿١﴾وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ﴿٢﴾إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴿٤﴾

Haa Miym. Na Kitabu kinachobainisha. Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku

uliobarikiwa, hakika Sisi daima ni Wenye kuonya. Katika (usiku) huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah. [Ad-Dukhaan: 1-4]

 

Vile vile

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾

Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar). [Al-Qadr: 1] 

 

Kwa hiyo mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa Qur-aan na kuisoma kwa wingi ndivyo inavyopasa kwa kila Muislamu.Ikiwa kusoma herufi moja ni sawa na thawabu kumi kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

عن عبدالله بن مسعودٍ رضي الله عنه أن النبيَّ صلى الله عليه وسلّم قال: ( من قَرأ حرفاً من كتاب الله فَلَهُ به حَسَنَةٌ، والحسنَةُ بعشْر أمْثالها، لا أقُول الم حرفٌ  ولكن ألفٌ حرفٌ ولاَمٌ حرفٌ وميمٌ حرفٌ)  رواه الترمذي

 

Imetoka kwa 'Abdillaah bin Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, Atakayesoma herufi moja katika kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja, na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, wala sisemi 'Alif-Laam-Miym' ni herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miym ni herufi moja.  [At-Tirimidhiy] 

 

Utakaposoma tu:

 

﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾

 Bismillahir-Rahmaanir-Rahiym

 

ambayo ina herufi 19 hivyo 19 x 10 ni sawa na thawabu190.

 

Suwrah-An - Naas (Qul A'uwdhu Birabbin-Naas) ina herufi 80. Hivyo 80 x 10 = 800 thawabu ambazo utazichuma kwa chini ya dakika moja! Basi itakuwaje biashara hii utakapoifanya kwa kusoma ukurasa mzima? Au robo juzuu? Au nusu juzuu? Au juzuu nzima n.k.? Je, itakuwaje thawabu endapo utakhitimisha Qur-aan nzima?

 

Jibriyl alikuwa akiteremka kila Ramadhwaan kumsikiliza Nabiy(صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Qur-aan na kumdarisisha:

 

  "كَانَ رَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ- أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ"  رواه البخاري   

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mbora mwenye matendo mema wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhwaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhwaan akimfundisha Qur-aan[Al-Bukhaariy]

 

Hali Za Swahaba Na Salafus Swaalih (Wema Waliotangulia) Na Qur-aan Katika Ramadhwaan:

 

'Uthmaan bin 'Affaan alikuwa akikhitimisha Qur-aan kwa siku moja.

Baadhi ya Salaf walikuwa wakikhitimisha kila siku tatu, wengineo kila wiki, wengineo kila kumi moja. Walikuwa wakiisoma Qur-aan katika Swalah na nje ya Swalah.

Imaam Ash-Shaafi'y alikuwa akikhitimisha Qur-aan mara nyingi mno katika Ramadhwaan.

Al-Aswad alikuwa akhitimisha kila siku mbili.

Az-Zuhri alikuwa inapoingia Ramadhwaan alijitenga na vikao vyote hata vya elimu na alikuwa akishughulika na kusoma Qur-aan pekee.

Salafus Swaalih aliyekuwa na duka, alikuwa akifunga duka lake mwezi wa Ramadhwaan akishughulika kusoma Qur-aan pekee.

 

Adabu za kusoma Qur-aan:

 

1 -   Kupiga mswaki

2 -   Kuchukua wudhuu

3 -   Kuelekea Qibla

4 -   (Wanawake) kujifunika vizuri

5 -   Kuelekea Qiblah

6 -   Anza na Isti‘adha na BismiLLaah

7 -   Soma kwa sauti ya kupendeza.

8 -   Zingatia maneno ya Rabb wako kwani ni amri kutoka Kwake:

 

 

 كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ 

Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad: 29]

 

9 - Unapopita kwenye Aayah za adhabu jikinge nazo; muombe Allaah Akuepushe na adhabu na moto, na unapopita katika Aayah za Rahma na Jannah usiache kumomba Allaah Akupatie hiyo Jannah.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atubarikie wakati wetu na Atuwezeshe kuifanya biashara hii kwa wingi khaswa katika mwezi huu Mtukufu. Aamiyn.

 

 

 

Share