01-Fatwa: Hairuhusiwi Kumpa Zakaatul-Fitwr Mtu Ambaye Umewajibika Kumuhudumia
Hairuhusiwi Kumpa Zakaatul-Fitwr Mtu Ambaye Umewajibika Kumuhudumia
SWALI
Mimi mwanamke nnayeishi nchi za nje. Nimeolewa nikiwa na watoto saba. Kila mwaka nampelekea mama yangu Zakaatul-Fitwr ambaye anaishi mbali namimi, nami ndiye nnayemhudumia kwa mahitajio yake (mwenye mas-uliya naye). Je, naruhusiwa kumpa Zakaah au haifai?
JIBU:
AlhamduliLlaah,
‘Ulamaa wamekubaliana bila ya kukhitilafiana kwamba hairuhusiwi kutuma Zakaah ya fardhi ambayo inajumuuisha Zakaatul-Fitwr kwa mtu ambaye inampasa kumhudumia (kuwa na mas-uliya nao) kama wazazi na watoto.
Inasema katika al-Mudawaanah (1/344):
Je, Vipi kuhusu Zakaah ya mali, kutokana na rai ya Maalik nimpe nani?
Akajibu:
"Usimpe yeyote katika jamaa zako ambaye unapaswa kumhudumia" [mwisho wa kunukuu]
Ash-Shaafi'iy kasema katika Al-Umm (2/87)
"Asimpe (Zakaah ya mali) baba yake, mama, babu au bibi" [mwisho wa kunukuu]
Ibn Qudaamah kasema katika Al-Mughniy (2/509):
“Zakaah yoyote ya fardhi isitolewe kwa wazazi hata mstari (wa ukoo) ukifikia vipi (yaani mababu na mabibi) au watoto hata mstari (wa ukoo) ukifikia vipi (yaani wajukuu).”
Ibn Mundhir kasema:
"’Ulamaa wamekubaliana bila ya kukhitilafiana kwamba hairuhusiwi kuwapa Zakaah wazazi ikiwa hali ya mtoaji ni mwenye kuwahudumia kwa sababu kuwapa Zakaah kutamaanisha kuwa hawahitaji tena awahudumie na manufaa yake yatamrudia yeye. Hivyo ni kama kujipa mwenyewe (hiyo Zakaah) nayo hairuhusiwi. Hali hiyo kadhalika ingelikuwa kama kujilipia deni lake mwenye" [mwisho wa kunukuu]
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu hukmu ya kumpa Zakaatul-Fitwr jamaa ambaye ni masikini:
Akajibu:
"Inaruhusiwa kumpa Zakaatul-Fitwr na Zakaah ya mali ya mtu kwa jamaa ambao ni maskini. Bali kuwapa jamaa ni bora kuliko kuwapa watu wageni kwa sababu kuwapa jamaa ni sadaka na pia kuunga ukoo. Lakini sharti kwamba kuwapa sio kwa kuhifadhi mali yake mtu, yaani ikiwa huyo jamaa masikini ni ambaye anapasa kumhudumia. Katika hali hii, hairuhisiwi kumtimizia haja zake kwa kumpa Zakaah kwa sababu akifanya hivyo atakuwa amehifadhi pesa zake mwenyewe kwa kumpa yeye Zakaah na hivyo hairuhusiwi. Lakini ikiwa hana mas-uliya naye ya kumhudumia basi anaweza kumpa Zakaah yake, na kumpa Zakaah yake ni bora kuliko kumpa mtu mgeni kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sadaka yenu kwa jamaa ni sadaka na pia kuunga ukoo)) [mwisho wa kunukuu]
Kwa hiyo, hairuhusiwi kwako kuitoa Zakaatul-Fitwr yako kumpa mama yako, bali umhudumie kutokana na mali yako nyingine isiyokuwa ya Zakaah. Na tunamuomba Allaah Akuruzuku rizki kwa wingi"
Na Allaah Anajua zaidi