Matani Na Masikhara Yanayoruhusiwa Katika Dini
Matani Na Masikhara Yanayoruhusiwa Katika Dini
Imekusanywa na Ukht Ruqayyah A. Baahasan
Kanuni Za Mzaha
1. Jiepusheni na mzaha kwenye mambo ya Dini ya Kiislam.
Hiki ni kitu kimoja kinachotengua Uislam wa binaadam. Allaah Anasema:
وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ ۚ
Na ukiwauliza, bila shaka watasema: Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu. [Tawbah: 65- 66]
Ibn Taymiyah (Rahimahu Allaah) kasema kuwa: “Kumfanyia masikhara Allaah au Ishara Zake na Rasuli Wake ni kufru. Na mtu anayefanya hivyo amekufuru baada ya kuamini.” Hali kadhalika wale wanaokejeli baadhi ya Sunnah, kama kuwacheka watu wanaofupisha kanzu au kufuga ndevu, au wanawake wanaovaa Hijaab, au Niqaab n.k.
Shaykh Muhammad ibn ‘Uthaymiyn amesema katika al-Majmu’u ath-Thamiyn, 16/3: “Mambo yanayohusu shari'ah za Uungu, Utume, Wahy na Dini ni vitu vitakatifu vinavyopaswa kutukuzwa na kuheshimiwa. Si mambo ya kuchekeshana, na hairuhusiwi kutoviheshimu au kuvicheka au kuvifanyia mzaha. Mtu anayefanya hivyo ni Kaafir na inaonesha kama mtu huyo hamuheshimu Allaah, na Rusuli Wake na Vitabu Vyake na Sheria za Kiislamu. Mtu huyo lazima atubu kwa Allaah, na aombe msamaha na asuluhishe vitendo vyake na kujenga khofu kwa Allaah. Vile vile lazima amtukuze Allaah na azidishe mapenzi yake kwa Allaah kwenye moyo wake.”
2. Matani Lazima Yawe Yanayosadikika Na Ya Ukweli Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Salam) amesema:
"Ole wake yule anayesema uongo kwa ajili ya kuwafanya watu wacheke.” (Abu Daawuud)
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) katuonya kuhusu tabia hii waliyozoea watu na akasema:
"Binaadam anaweza akasema kitu kuchekesha wenzake na akaingia katika Moto wa Jahanam umbali mkubwa kwa tendo hilo." [Ahmad]
3. Msiwatishe Na Mkawashituwa Wenzenu Wale watu walio hodari na watendaji hususan, au wale wanaokamata silaha au chuma, au wanaotumia nafasi kwenye kiza kwa kutumia udhaifu wa wenzao na kuwatisha na kuwashtua. Amesema Abu Layla, “Swahaba wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) walikua wanasafiri na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) na mtu miongoni mwao alisinzia na akalala. Baadhi yao walimfunga na kamba na alipoamka Alishtuka sana na kuogopa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) akasema:
“Haifai kwa Muislam kumogopesha Muislam mwenzake. [Abu Daawuud]
4. Kumkejeli Mtu Kwa Kupwesa Jicho Nyuma Yake Au Kumtolea Maneno Ya Ujeuri Watu wanatofautiana kwa uwezo wao wa kufahamu na kwa tabia zao; watu wengine ni dhaifu, na waliozoea kudharau wenzao wanaweza kuwafanya watu kama hao wawe ni kitu cha matani. Allaah kakataza tabia hiyo kwenye aayah hii kutoka Suwrah Al-Hujuraat: 11]
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾
Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kudharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. Na wala msifedheheshane kwa kutukanana na wala msiitane majina (mabaya) ya utani. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya iymaan. Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu. [Al-Hujuraat :11]
Ibn Kathiyr kasema kwenye Tafsiyr yake:
“Imekusudiwa kuwatukana na kuwakejeli. Hii ni haraam na inahesabika kama tabia za wanaafik.”
Watu wengine wanacheka umbo la mtu, au mwendo wao au gari ya mwenzao. Hofu ya Allaah inaweza kumfanya mtu huyo awafikirie wale anaowacheka. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) amesema:
“Msije mkafurahia hali mbaya ya ndugu yenu wa Kiislam. Allaah Anaweza kufanya kikupate kile ulichokicheka au kukifanyia utani”. [at-Tirmidhiy]
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) alitutahadharisha juu ya kuwadharau na kuwashutumu watu kwa sababu tabia hiyo inaweza kuleta chuki kwenye jamii ya Kiislam. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) amesema:
“Muislam yeyote ni ndugu wa Muislam mwenzake. Asije akamdharau au kumshutumu. Taqwa ipo hapa (na akaonyesha kwenye kifua chake mara tatu) kila Muislam kaharamishiwa kwa mweziwe; damu yake, mali yake, na heshima yake.” (Muslim)
5. Mzaha Usivuke Mipaka Watu wengine wanafanya masikhara sana hadi inakuwa ni tabia yao. Hii ni kinyume na na tabia za Waislam ambao wanatakiwa wawe ni watu wa dhati na makini. Masikhara ni mapumziko kutokana na kazi na udhati na umakini wa muda mrefu, ni burudani ya moyo. 'Umar bin ‘Abdil ‘Aziyz alisema:
“Ogopeni masikhara kwa sababu inazalisha chuki.”
Imaam an-Nawawiy amesema kuwa:
“Aina za matani yaliyokatazwa ni matani yaliyovuka mipaka na yakawa ni kawaida na tabia. Aina hi ya matani husababisha kucheka sana na kuushupaza moyo wa Muislam. Pia husababisha mtu asahau kumkumbuka Allaah na inazidisha watu kuumizana na kuzalisha chuki baina yao”
6. Lazima Ujue Cheo Cha Mtu Baadhi ya watu wanaweza kufanya mzaha na kila mtu bila kutofautisha cheo cha mtu au hadhi yake. Wanachuoni wanasema kuwa wazee wana haki zao na lazima tujue tabia ya mtu tunayemkabili. Usifanye masikhara na wajinga na watu usiowajua.
Kuhusu maudhui hii, ‘Umar ibn ‘Abdil-‘Aziyz alisema:
“Ogopeni masikhara, kwa sababu yanapunguza uungwana na uanaume.” Sa’ad ibn Abi Waqqaas alisema kuwa:
“Wekeni mipaka kwa vichekesho vyenu, kwa sababu mkivuka mipaka mtapoteza heshima na mnaweza kuchochea ujinga dhidi yenu”
7. Kiasi Cha Mzaha Kinachokubalika Ni Lazima Kisizidi Kadiri Ya Chumvi Kwenye Chakula Chako Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Swallam) alisema:
“Msicheke sana kwa sababu kucheka sana kunaua moyo wa mtu.” [Sahiyh al-jaami’, 7312]
‘Umar ibn Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema:
“Yeyote anayecheka kupita kiasi anapoteza heshima. Na yeyote anayeshikilia kufanya kitu atajulikana kwa hicho kitu anachokifanya.”
Lazima tutahadhari na masikhara, kwa sababu yanaweza kumfanya mtu apoteze heshima baada ya kusifika kuwa ni mwenye heshima, na anaweza kufedheheka baada ya kuheshimiwa.
8. Kusengenyana Hairuhusiwi Kusengenya ni maradhi machafu. Baadhi ya watu wanafikiri kama wanaweza kuwasema wenzao na kukubalika kama ni masikhara, lakini imetajwa kwenye Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) kuwa, “Kumsengenya ndugu yako ni kutaja kitu anachokichukia.” [Muslim]
9. Chagueni Wakati Muwafaka Wa Kutaniana Kama kwenye safari ya kwenda mapumzikoni nje ya mji au kwenye hafla jioni au kama mmekutana na rafiki na mnataka kupumzika na kupeana mazungumzo mazuri na mzaha; mkataniana kwa ajili ya kuzidisha mapenzi, urafiki na furaha kwenye nyoyo zenu. Au kama matatizo ya kifamilia yamezidi au mmoja wenu amekasirika mnaweza kufanya masikhara kupunguza fadhaa na mazonge na kujifurahisha nafsi zenu.
Ee! Muislam, Mtu alimwambia Sufyaan ibn ‘Uyaynah (radhiya Allaahu ‘anhu), “Masikhara si kitu sahihi, lazima kikatazwe.”
Akamjibu, “Bali ni Sunnah, lakini kwa wale wanaojua vipi kuyafanya hayo masikhara na wanaofanya masikhara kwenye wakati wake unaotakikana.”
Siku hizi, Ummah wa Kiislamu wanatakiwa wazidishe mapenzi baina yao na kupunguza uchoshi, lakini wamepitisha kiasi kwenye kufanya matani, mzaha na vichekesho. Imekua ni kawaida kwenye mikusanyiko, na watu wanapoteza wakati mwingi. Wanapoteza maisha na wakati wao kwenye mzaha na hadi kwenye magezeti yao kumejaa vichekesho na michezo.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salam) alisema:
“Kama mlikua mnajua (mna elimu) kama navyojua mie basi mungecheka kidogo na kulia sana.” (Katika Fat-hul Baariy imeandikwa kuwa, “Elimu” hapa inamaanisha kuwa kwa nguvu za Allaah na kisasi Chake kwa wale wanaokufuru, na kwa khofu inayokuwa katika mauti, na kwenye makaburi na kwenye Siku ya Qiyaamah.)
Waislam wanaume na wanawake lazima wachague marafiki waadilifu na wa dhati (si wapenda utani na wapotezaji muda) katika maisha yao. Marafiki hao watawasaidia kutumia wakati wao vizuri na watawaelekeza katika njia sahihi na kujitahidi kwa ajili ya Allaah. Marafiki hao watawasaidia kuwa Waislam wema na thabiti.
Bilaal ibn Sa’ad alisema,
“Mimi niliwaona Maswahaba wanapigania vitu, kwa masikhara, wanacheka na wenzao lakini ukiingia usiku wanakuwa kama Maimaam.”
Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) aliulizwa,
“Je, Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wanacheka?”
Akajibu, “Naam, na Imani ilikuwa ndani ya nyoyo zao kama milima.”
Lazima tufuate mifano ya watu kama hao, waliokua mashujaa mchana na Imaam (wafuasi wacha wa Allaah wa Dini yetu) usiku.
Allaah Atuhifadhi sisi na nyinyi na wazee wetu siku ya Qiyaamah. Na tuwe katika wale watakaoambiwa siku hiyo:
أَهَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ أَقْسَمْتُمْ لَا يَنَالُهُمُ اللَّـهُ بِرَحْمَةٍ ۚ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمْ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ ﴿٤٩﴾
Je, hawa si wale ambao mliapa kwamba Allaah hatowafikishia kwa rahmah yoyote ile? (Leo wanaambiwa) Ingieni Jannah! Hakuna khofu juu yenu na wala nyinyi hamtohuzunika. [Al-A’raaf: 49]
Wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa Ahlihi wa Asw-haabihi.