Kumsomea Mwenye Majini Aayah Za Qur-aan Kwa Kiswahili Ikiwa Hawezi Kusoma Kiarabu

 

Kumsomea Mwenye Majini Aayah Za Qur-aan

Kwa Kiswahili Ikiwa Hawezi Kusoma Kiarabu

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Kutoka kwenye mawaidha ya video kwenye Alhidaaya.com yenye kichwa cha habari  Ulimwengu Wa Majini ('Abdul-Latwiyf 'Abdul-Kariym )

Je katika kumsomea mgojwa mwenye jini inawezekana kusoma zile aya za Quran zilizotajwa kwa kutumia tafsiri ya kiswahii au ni lazima ujue kusoma Quran.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Mwanzo tufahamu kuwa kutoa jini aliyemvaa mtu ni fani kama fani nyingine na hivyo kutaka uzoefu kwa hilo. Haiwezekani kwa mtu kuingia mara moja katika suala hilo kabla ya mwanzo kufuata na mjuzi wa suala hilo ili kuona kinachofanywa. Maana inasemwa na hao watoaji kuwa ukikosea kidogo tu basi jini huyo huenda akatoka kwa mgonjwa na kukuingia wewe unayetaka kumtibu. Hivyo, ni vyema tuwe na tahadhari kuhusu hilo.

 

Ama kumsomea mgonjwa huyo aliyekumbwa na jini kwa lugha nyingine yoyote kama vile Kiswahili haifai kwani hiyo si Qur-aan bali tunaiita tafsiri au tarjuma. Na katika tafsiri huwa yapo mambo mengi na mara nyingine pia hupati maana sawa ya neno fulani. Hata hilo lingekuwa linatekelezeka pia haingekuwa ni Qur-aani.

 

Kwa muhtasari tunasema kuwa ni lazima umsomee kwa ile ile Qur-aan ya asili ambayo ipo katika lugha ya Kiarabu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share