Kutumia Ukumbi (Hall) Unaotumiwa Na Makafiri Kwa Ajili Ya Kuswalia
SWALI:
Assalam aleikum.
Ndugu zangu katika Uislam. Swali langu ni: - JEE TWAFAA KUSWALI KWENYE HALL AMBALO WAKATI MWENGINE HUKODIWA
HALL LENYEWE SI KANISA WALA HALIKUJENGWA KAMA KANISA BALI NI HALL AMBALO HUKODIWA KWA MAMBO TAFAUTI TAFAUTI KAMA VILE SWALA YA SIKU IJUMAA KWA WAISLAMU, MADRASA KWA WAISLAMU SIKU YA IJUMAMOSI, MAOMBI YA WAKIRISTO SIKU YA IJUMAPILI
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hakujaalia katika Dini yetu Tukufu uzito wa aina yoyote. Kinyume chake ni kuwa Dini hii yetu imejengwa na usahali na tahfifu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuarifu kuwa yapo mambo matano ambayo hakupatiwa mwengine yeyote katika Ummah zilizopita. Moja wapo katika hizo ni: “Ardhi yote imejaaliwa mimi na Ummah wangu kuwa ni Msikiti na twahara” (al-Bukhaariy na Muslim).
Kwa minajili hii hakuna tatizo kabisa lenu nyinyi kulitumia hall
Muhakikishe kuwa hakuna masanamu wala mapicha sehemu hiyo.
Kufagia au kuliosha kunakuja tu ikiwa mumeona najisi ambayo inabidi ioshwe lakini ikiwa hakuna mnaweza kufanya Ibadah zenu bila ya tatizo au wasiwasi aina yoyote. Ila mnatakiwa muwe mmefanya jitihada za kutosha za kutafuta sehemu nyingine isiyo na mashaka, na endapo mmekosa kabisa ndipo mnaweza kutumia sehemu hiyo.
Na Allaah Anajua zaidi