Wanawake Wanafaa Kuvaa Dhahabu?
Wanawake Wanafaa Kuvaa Dhahabu?
Swali La Kwanza:
Asalam Aleikum,
Ndugu zangu ningependelea kuliza kuhusu mwanamke kuvaa dhahabu inafaa ama haifai?In shaa Allaah na subiri jawab...JazakkAllaah kheir
Swali La Pili
Nilikuwa na swali kuhusu hayo mawaidha naona watu wengi wenyewe nimeuliza kuhusu hao mawaidha ya wanawake kuwa wameharamishiwa kuvaa dhahabu, hawaelewi nawaniuliza kwenyewe imeandikwa aayah gani hadiyth gani na mashekh wahuku kwetu wanakata kabisa wanasema kuwa hayo maneno siyo yauhakika ,Basi nimeona niwaulize Mashekhe wetu wa Alhidaaya kuhusiana na hayo mambo mnieleweshe
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Mas-ala haya wametofautiana rai 'Ulamaa. Wanachuoni wengi ambao kwa dalili zingine walizozitaja, wameonyesha kuwa mapambo ya dhahabu ni halaal kwa mwanamke. Na rai hiyo ya Wanachuoni wengi ndio iliyoenea na kutumika sehemu nyingi.
Kuna wanachuoni wachache waliokwenda katika rai kuwa dhahabu haijuzu hata kwa mwanamke mfano wa Shakykh Al-Albaaniy ambaye kwa Ijitihaad yake amefikia ufumbuzi kuwa mapambo ya dhahabu hayajuzu hata kwa mwanamke na akatoa dalili katika kitabu chake cha Adaabuz-Zafaaf. Na dalili alizozitegemea ni Hadiyth zifuatazo ambazo wanachuoni wanaokubali dhahabu kwa mwanamke wamezieleza kuwa Hadiyth hizo, ima zingine zilikuwa zimefutwa na zingine zenye kuruhusu, au baadhi hazina nguvu na kutegemewa kuwa ni ushahidi wa kukataza. Nazo ni hizi:
عن ثوبانَ رضي الله عنه قالَ: جاءَتِ ابْنَةُ هُبَـيْرَةَ إلـى النبـيِّ وفـي يَدِهَا فَتَـخٌ من ذَهَبِ أَيْ خواتـيـمُ ضخامٌ، فَجَعَلَ النبـيُّ يَضْرِبُ يَدَهَا،(بعصية معه يقول لها ((أيسرك أن يجعل الله في يدك خواتيم من نار؟!)) فَأَتَتْ فاطمةَ تَشْكُو إلَـيْهَا، قال ثوبانُ: فَدَخَـلَ النبـيُّ إلـى فاطمةَ وأَنَا معهُ وقد أَخَذَتْ من عُنُقِهَا سِلْسِلَةً من ذَهَبٍ، فقالتْ: هَذِهِ أَهْدَاهَا لِـي أَبُو حَسَنٍ وفـي يَدِهَا السِّلْسِلَةُ، فقالَ النبـيُّ: ((يا فاطمة! أَيَسُرُّكِ أَنْ يقولَ الناسُ فاطمةُ بنتُ مـحمدٍ فـي يَدِهَا سِلْسِلَةٌ من نارٍ))، (ثم عذمها عذماً شديداً)، فَخَرَجَ ولـم يَقْعَدْ، فَعَمَدَتْ فاطمةُ إلـى السِّلْسِلَةِ فَبَاعَتْهَا واشْتَرَتْ بِهِ نَسَمَةً وَأَعْتَقَتْهَا، فَبَلَغَ ذلِكَ النبـيَّ فقالَ: ((الـحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي نَـجَّى فاطمةَ من النارِ))
Kutoka kwa Thawbaan Radhwiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Bint wa Hubayrah alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)akiwa amevaa pete kubwa za dhahabu mkononi mwake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akaanza kumpiga piga mkono wake kwa kijiti kidogo alichokuwa nacho huku akisema, ((Utafurahi Allaah Akikuvalisha pete za moto katika mkono wako?)) Akaenda kwa Faatwimah kumlalamikia". Thawbaan akasema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikwenda kwa Faatwimah nikiwa naye. Alimnyang'anya mkufu wa dhahabu kutoka shingoni mwake na kusema: "Huu nilipewa na Abu Hasan" ('Aliy mume wake) na mkufu ulikuwa mkononi mwake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema, ((Ee Faatwimah, utafurahi kama watu watasema kwamba Faatwimah mtoto wa Muhammad ana mkufu wa motoni mkononi mwake?)) Kisha akawa mkali kwake, na akaondoka bila ya kuketi. (Faatwimah) Akachukua mkufu, akauuza na badili yake akaacha huru watumwa wengi. Ilipomfikia habari hii Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alisema, ((Sifa zote Anastahiki Allaah Aliyemnusuru Faatwimah na moto)) Ahmad, An-Nasaaiy na wengineo: Swahiyh
((مَنْ أحَبَّ أنْ يُحَلِّقَ حَبِيبَهُ حَلْقَةً مِنْ نَارٍ فَلْيُحَلِّقْهُ حَلْقَةَ مِنْ ذَهَبٍ، وَمَنْ أحَبَّ أنْ يُطَوِّقَ حَبِيبَهُ طَوْقاً مِنْ نَارِ فَلْيُطَوِّقْهُ طَوْقاً مِنْ ذَهَبٍ، وَمَنْ أحَبَّ أنْ يُسَوِّرَ حَبِيبَهُ سِوَاراً مِنْ نَارٍ فَلْيُسَوِّرْهُ سِوَاراً مِنْ ذَهَبٍ، وَلَكِنْ عَلَيْكُم بالْفِضَةِ فَالْعَبُوا بِهَا (الْعَبُوا بِهَا،الْعَبُوا بِهَا)
((Yeyote anayetaka kumvisha pete ya moto mpenzi wake, basi amvishe pete ya dhahabu. Na Yeyote anayetaka kumvisha kidani cha moto mpenzi wake, basi amvishe kidani cha dhahabu. Na Yeyote anayetaka kumvisha bangili ya moto mpenzi wake, basi amvishe bangili ya dhahabu. Bali pendeleeni fedha na muichezee, ichezeeni, ichezeeni)) Abu Daawuud na Ahmad: Hasan
عَنْ عائشة أنَّ النَّبِي صلى الله عليه وسلم رَأى فِي يَد عائشة قُلبين ملويين مِنْ ذَهَب، فقال: ((أَلْقيهِمَا عَنكِ، وَاجْعَلي قلبين مِنْ فِضَّة، وَصفريها بِزَعْفَران))
Kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah Radhwiya Allaahu 'anhaa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam aliona bangili mbili za dhahabu zilizopindika katika mkono wake. Akasema, ((Zitupilie mbali na vaa badala yake bangili za fedha na zitie rangi ya manjano kwa zaafarani)) An-Nasaaiy na wengineo: Swahiyh.
عن أم سلمة زوج النبيّ صلى الله عليه وسلم قالت: جعلت شعائر من ذهب في رقبتها، فدخل النبيّ صلى الله عليه وسلم فأعرض عنها، فقلت: ألا تنظر إلى زينتها؟ فقال: ((عَنْ زِينَتِكِ أَعْرَضَ)) (قالت: فقطعتها، فأقبل علي بوجهه).قال: زعموا إنه قال: ((ما ضَرَّ إحْداكُنَّ لو جَعَلَتْ خُرْصاً مِنْ وَرَقٍ ثُمَّ جَعَلَتْهُ بِزَعْفَرَانٍ))
Kutoka kwa mama wa waumini Ummu Salamah, mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema: "Nilivaa shanga za dhahabu shingoni mwangu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) wa akaingia na akageuza (uso wake asizione). Nikasema: Hutaki kutazama uzuri wake?" Akasema, ((Ni mapambo yako niliyoyageuzia uso)). Nikakivunja kidani, kisha akageuza uso wake kwangu". Msimuliaji akasema: "Waliamini kwamba Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam alisema, ((Itamdhuru nini mmoja wenu akitengeneza hereni za fedha kisha akazitia rangi (ya manjano) kwa zaafarani?)) Ahmad na wengineo: Swahiyh
Ama wenye kuunga mkono kuwa wanawake wanauhusiwa kuvaa dhahabu wao dalili zao ni kama zifuatazo:
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
أَوَمَن يُنَشَّأُ فِي الْحِلْيَةِ وَهُوَ فِي الْخِصَامِ غَيْرُ مُبِينٍ﴿١٨﴾
Ah! (Wanampendelea Allaah kiumbe) aliyelelewa katika mapambo naye katika mabishano si mbainifu? [Az-Zukhruf: 18]
Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anapotaja mapambo yanayowahusu wanawake yanajumuisha pia mapambo ya dhahabu. Na dalili ni kwamba wanawake wameruhusiwa kujipamba kwa dhahabu kutokana na bayana ya makatazo hayo kwa wanaume pekee kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ifuatayo:
عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال : (( أحل الذهب والحرير للإناث من أمتي وحرم على ذكورها)) رواه أحمد والنسائي والترمذي وصححه وأخرجه أبو داود والحاكم وصححه وأخرجه الطبراني وصححه ابن حزم
Kutoka kwa Abu Muwsaa Al-Ash'ariyyi (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Imehalalishwa dhahabu na hariri kwa wanawake katika Ummah wangu na imeharamishwa kwa wanaume)) [Ahmad, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy na kaisahihisha na kuitoa Abu Daawuud na Al-Haakim na kaisahihisha na kuitoa At-Twabaraaniy na kaisahihisha Ibn Hazm]
Hiyo ni rai ya 'Ulamaa wengi waliotangulia na wamesimulia kwamba muwafaka wa Ijmaa wameruhusu mwanamke avae dhahabu.
Vile vile wanasema kuwa ilikuwa ni desturi ya wanawake zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba hadi sasa wanawake kuvaa dhahabu na hakukuwa na makatazo.
Na wanaeleza kuwa mwanamke anahitaji kujipamba mbele ya mumewe kwani ni jambo lililopendekezwa, kwa hiyo ameruhusiwa kujipamba kwa kila aina ya mapambo yakiwemo dhahabu.
Dalili nyingine ni usimulizi wa Hadiyth zifuatazo:
عن عمرو بن شعيب عن أبيه عن جده أن امرأة أتت النبي صلى الله عليه وسلم ومعها ابنة لها وفي يد ابنتها مسكتان غليظتان من ذهب فقال لها : (((أتعطين زكاة هذا؟)) قالت : لا قال : ((أيسرك أن يسورك الله بهما يوم القيامة سوارين من نار ؟)) فخلعتهما فألقتهما إلى النبي صلى الله عليه وسلم وقالت هما لله ولرسوله فأوضح لها النبي صلى الله عليه وسلم وجوب الزكاة في المسكتين المذكورتين ، ولم ينكر عليها لبس ابنتها لهما ، فدل على حل ذلك وهما محلقتان - رواه أبو داود والنسائي والحديث صحيح وإسناده جيد ، كما نبه عليه الحافظ في البلوغ
Kutoka kwa 'Amr ibn Shu'ayb kutoka kwa baba yake, kisha kutoka kwa babu yake kwamba: "Mwanamke alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na mtoto wake wa kike ambaye alikuwa amevaa bangili mbili nzito mikononi mwake. Akamwambia ((Je, unazitolea Zakaah hizi?")) Akajibu: 'Hapana'. Akasema: ((Utafurahi Allaah Akikupa bangili mbili za moto siku ya Qiyaamah kwa sababu ya hizi?)) Akazivua na kuzitupa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: 'Hizo ni za Allaah na Mjumbe Wake'. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamfahamisha wajibu wa kuzitolea Zakaah bangili hizo mbili lakini hakumkataza kumvisha mwanawe" [Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Hadiyth ni Swahiyh na Isnaad yake ni nzuri kama alivyotanabahisha Al-Haafidhw katika Al-Buluugh]
Vile vile:
عن عائشة رضي الله عنها قالت : " قدمت على النبي صلى الله عليه وسلم حلية من عند النجاشي أهداها له فيها خاتم من ذهب به فص حبشي قالت : فأخذه رسول الله صلى الله عليه وسلم بعود معرضا عنه أو ببعض أصابعه ثم دعا أمامة ابنة أبي العاص ابنة ابنته زينب فقال : ((تحلي بهذه يا بنية)) ، فقد أعطى صلى الله عليه وسلم أمامة خاتما ، وهو حلقة من الذهب ، وقال :(( تحلي بها)) ، فدل على حل الذهب المحلق نصا . سنن أبي داود بإسناد صحيح
Kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ambaye amesema: "Mapambo (Ya vito na dhahabu) yaliletwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni zawadi zake kutoka kwa an-Najjaashiy (Mfalme wa Abyssinia [Ethiopia]). Na pete ya dhahabu ilikuwa miongoni mwayo ambayo ilitiwa jiwe la Abyssinia. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaichukua kwa kusita sita akiivuta kwa kijiti au kidole chake kisha akamwita Umaamah mtoto wa Abu Al-'Aasw na mtoto wake wa kike Zaynab. Akasema: ((Jipambe nayo ewe mwanangu)) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akampa pete Umaamah ambayo iliundwa kwa dhahabu ya mfumo wa duara akasema: ((Jipambe kwa hii)) [Sunan Abu Daawuud ikiwa na isnaad Swahiyh]
Hii inabainisha kwamba dhahabu iliyo katika mfumo wa duara inaruhusiwa kutokana na masimulizi hayo.
وعن أم سلمة رضي الله عنها أنها كانت تلبس أوضاحا من ذهب فقالت : يا رسول الله أكنز هو ؟ قال : (( إذا أديت زكاته فليس بكنز)) رواه أبو داود والدارقطني وصححه الحاكم كما في بلوغ المرام
Na kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba alikuwa akivaa mikufu ya dhahabu miguuni akasema: "Ee Rasuli wa Allaah, hii ni kanz" (hazina iliyohifadhiwa). Akasema: ((Ikiwa utailipia Zakaah haitokuwa ni hazina)) [Abu Daawuud na Ad-Daaraqutwniy na kaisahihisha Al-Haakim katika Buluugh Al-Maraam]
Pamoja na kwamba ukizitazama rai za makundi hayo mawili ya wanachuoni, utaona kuwa zinachuana kwa dalili mbalimbali walizoegemea kwazo, ila wengi wanaonelea kuwa rai za kuruhusu kwa dalili zilizotolewa, kuwa ni zenye nguvu zaidi na hitimisho ni kwamba dalili hizo zimeruhusu mwanamke kuvaa dhahabu na hiyo ndiyo rai ya Wanachuoni wengi zaidi na ndiyo inayojulikana na kukubalika hadi sasa.
Ama kuhusu wanaume hakuna mashaka yoyote ya kukatazwa kwao kuvaa dhahabu kwa dalili nyingi. Na hakuna hata mwanachuoni mmoja mwenye kuaminika au kutegemewa aliyesema kuwa mwanaume anaruhusiwa kuvaa dhahabu. Dalili zinapatikana katika kiungo hichi ndani kwenye paragrafu za mwisho:
40 Kukataa Kufanya Mambo Yanayopingana Na Sheria
Na Allaah Anajua zaidi