Zingatio: Ukificha Au Ukidhihirisha Anakuona

 

Zingatio: Ukificha Au Ukidhihirisha Anakuona

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kumekuwa na mtindo wa kuiga mambo hata kwa nchi za Ulimwengu wa tatu ambao umegubikwa na ukame kushughulishwa na vitu vya kipuuzi na kupoteza wakati. Watawekwa watu wa jinsia tofauti na hulka tofauti kwenye jumba wakichunguzwa tabia na mwenendo wao hadi wakiwa sehemu za faragha kama chooni. Yote kuonesha kwamba upo uwezekano mkubwa wa mwanaadamu kumuona mwenziwe kwa kila hatua. Ni hivi karibuni pia Marekani wametaka kuongeza kamera za usalama mitaani kwa lengo la kuchunguza harakati za watu.

 

Hayo mambo yote yanayofanywa, bila ya shaka yapo na yamewezekana. Sasa kama binaadamu anaweza kumchungulia mwenziwe pasi na yeye kutambua. Iweje kazi hii Ashindwe Mfalme wa Wafalme?

 

Tambua ewe Muislamu kwamba Mola Mtukufu Anakuona katika hali yoyote ile uliyokuwa nayo, ikiwa siri au dhahiri, huna pa kujificha. Vilevile fahamu kwamba kila jambo utakalolifanya basi utalipwa jinsi litakavyokuwa ukubwa wake. Huo ndio unyenyekevu wa kweli kweli Autakao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِّمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ

Na nani aliye bora zaidi kwa Dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Allaah naye ni mtendaji ihsaan.. [An-Nisaa: 125]

 

Na vile vile Akasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

وَإِن تُبْدُوا مَا فِي أَنفُسِكُمْ أَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُم بِهِ اللَّـهُ

Na mkidhihirisha yale yaliyomo ndani ya nafsi zenu au mkiyaficha; basi Allaah Atakuhesabuni kwayo. [Al-Baqarah: 284]

 

Vyovyote tutakavyoweza kumchungua mwanaadamu, katu hatuwezi kufikia kutambua yale yaliyomo ndani ya nafsi ya mtu. Wahenga walisema: “Waweza kunizuia kusema, lakini huwezi kunizuia kufikiri”. Hivyo, yaliyomo ndani ya nafsi Ayajua Yeye Muumbaji wa hiyo nafsi kwani Yeye ndie Mchunguaji Mkuu kuliko yeyote. Naye Amesema: 

 

كَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ رَّقِيبًا ﴿٥٢﴾

Na Allaah daima ni Mwenye kuchunga kila kitu. [Al-Ahzaab: 52]

 

Kuna mafundisho mengi tu ndani ya Qur-aan ya kuifundisha nafsi kwamba unachunguliwa na Mola Mtukufu kwa kila jambo. Na katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaja nguzo za Ihsani katika Hadiyth maarufu ya Jibriyl alipokuja kumuuliza maswali ya kufundisha watu Dini kama ilivyopokewa na Amiyrul Muuminiyn ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu: “…Umuabudu Mwenyezi Mungu kama vile unamuona, kwani kama wewe humuoni, Yeye Anakuona...” [Muslim]

 

Mwendo huu ndio ulikuwa wa Salafus Swaalihiyn katika kuzilea nafsi zao, mpaka wakaziweza na wakazizoesha kutenda kila lenye kheri na Dini yao.

 

 

Share