Nifanyeje Nikisahau Rakaa Katika Swalah?

Nifanyeje Nikisahau Rakaa Katika Swalaah?

 

 

 

 

SWALI:

 

 

Naomba kuwapongeza kwa juhudi kubwa mufanyazo na mungu atawasahilishia kila la wepesi.

 Swali langu ni kuwa, nini hukumu ya mwenye kusahau rakaa, ama anatashuwishi na atafanya nini? Shukran.

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho 

 

 

 

Hakika ni kuwa mwanaadamu ameumbwa na sifa ya kusahau na shaytwaan naye ana bidii na hima ya kumshughulisha katika Swalaah kwa kumfanya afikirie mambo ya nje ya Swalaah yake. Kwa hiyo, huenda mwana Aadam akapunguza, au akaongeza, au akachanganyikiwa katika Swalaah yake. Ndipo Allaah (Subhaanahu wa  Ta‘aalaa) Akaweka kwa mwenye kuswali asujudu mwisho wa Swalaah yake anaposahau inayoitwa “Sajdatus Sahw (Sijdah ya kusahau) ambayo inafidia huko kusahau, inamtweza shaytwaan na inamridhisha Ar-Rahmaan.

 

Sahw ni kusahau. Hakika ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisahau katika Swalaah, ikawa kusahau kwake huko ni neema kwa Ummah wake na kukamilika kwa Dini. Kumenakiliwa kusahau kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) matukio mengi katika Swalaah:

Alipiga salaam baada ya rakaa mbili, akasujudu [al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Dhul Yadayn [Radhwiya Allaahu ‘anhu])

 

Alipiga salaam baada ya rakaa tatu, akasujudu [Muslim kutoka kwa ‘Imraan bin Haswiyn [Radhwiya Allaahu ‘anhu]

 

Alisimama baada ya rakaa ya pili na bila kukaa kitako cha tashahhud kwa kusahau, akasujudu [al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa ‘Abdullaah bin Buhaymah [Radhwiya Allaahu ‘anhu])

 

Aliswali kwake rakaa tano, akasujudu baadaye sijdah mbili [Muslim kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas‘uwd [Radhwiya Allaahu ‘anhu]

 

 Na Hadiyth nyinginezo zimethibiti.

Hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoa muongozo: “Anaposahau mmoja wenu, asujudi sijdah mbili” [Muslim kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas‘uwd [Radhwiya Allaahu ‘anhu]

 

Ama tukija katika maswali yako, tusasema kuwa mwenye kusahau rakaa katika Swalaah, basi Swalaah yake haijakamilika. Rakaa kamili ni nguzo na inabidi iletwe pindi unapokumbuka kwa mfumo ufuatao: 

 

 

1-Ikiwa umekumbuka baada ya Swalaah tu, utasimama kuiswali hiyo rakaa na kisha ulete sijdah mbili.

 

 

2-Ikiwa hakikupita kipindi kingi baina ya kumaliza Swalaah nawe upo katika hali ya twahara utaileta rakaa kamili kisha utasujudu sijdah mbili na itoe salaam.

 

 

3-Ikiwa kimepita kipindi kingi au wudhuu umetenguka, utaanza Swalaah yote upya.

 

 

Ama tashwishi katika Swalaah, swali lako halipo wazi lakini tutajaribu kulieleza kama tulivyofahamu. Ikiwa tashwishi iko katika idadi ya rakaa, na una shaka kama umeswali rakaa mbili au tatu kwa mfano, utachukua idadi ndogo (yaani mbili). Kisha kabla ya salaam, utaleta sijdah mbili. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth:

Anapokuwa na shaka mmoja wenu katika Swalaah yake, hajui ameswali moja au mbili, ajaalie moja. Na ikiwa hajui kama ameswali mbili au tatu, ajaalie mbili” [Muslim, Ahmad, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

 

Ikiwa yeye ni maamuma na ana shaka amempata Imaam rakaa ya kwanza au ya pili, atajaalia amepata ya pili kisha atasujudu sijdah mbili. Ikiwa ana shaka kama ameacha nguzo itakuwa ni kama ameacha, hivyo ataileta hiyo nguzo na matendo yanayokuja baada yake ikiwa ameweza kurudi katika hali ya hiyo nguzo kisha atasujudu sijdah mbili. Ikiwa ashakwenda sana na hawezi tena kurudi itabidi ulipe rakaa nzima.

 

 

Ama akiwa na shaka ya kuacha wajibu, hutotia maanani hilo na hakuna Sajdatus Sahw na hivyo hivyo ikiwa una tashwishi ya kuongeza, hutolitazama hilo, kwani asli ni kutokuwepo ziyada.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share