Wanawake Na Wanaume Kusalimiana Na Kupeana Mikono
Wanawake Na Wanaume Kusalimiana Na Kupeana Mikono
Swali:
Mashekhe wetu wa Alhidaaya tunaomba mtupe maelezo kuhusu makatazo ya wanawake kusalimia wanaume kwa kutoa mikono maana nnavyojua haifai lakini nilipomkataza mwenzangu amenijibu: “Wapi imeandikwa katika Quran”. Asanteni.
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kutokana na mwenye kusema “Wapi imeandikwa katika Quran” atambue kwamba sheria zetu za Kiislamu hazitokani na Qur-aan pekee, bali pia zinatokana na Sunnah pia ikiwa hazimo katika Qur-aan. Na hata mara nyingine utakuta kwamba sheria nyingine zimo katika Sunnah pekee na hazipatikani katika Qur-aan. Mifano mingi sana imo kuhusu mas-ala haya na Insha Allaah tutakapojaaliwa tutatayarisha makala inayoonyesha umuhimu au cheo cha Sunnah kulingana na Qur-aan.
Kisha mtu mwenye kukanusha Sunnah akaamini kuwa sheria zetu zinatokana na Qur-aan pekee na asitake kujua amri za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) atakuwa amekufuru kwani kutokumuamini Mtume wetu ni kutokuamini maneno ya Allaah Anaposema:
وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۚ
Na mtiini Allaah na mtiini Rasuli, [At-Twaghaabun: 12]
مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ
Atakayemtii Rasuli basi kwa yakini amemtii Allaah. [An-Nisaa: 80]
Kisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) Ametuamrisha tufuate yote aliyotupa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Ametuamrisha tujiepushe na yote aliyotukataza.
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7]
Na maonyo makali kama yafuatayo kwa mwenye kukanusha Sunnah na amri zake:
فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾
Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63]
وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾
Na atakayempinga Rasuli baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini; Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Jahannam. Na uovu ulioje mahali pa kuishia. [An-Nisaa: 115]
Sasa vipi basi ndugu yetu asione kuwa ni muhimu kufuata amri za Mtume bali atake kujua tu kama sheria au amri ziko katika Qur-aan?
Je mbona basi anaswali Swalah 5 akirukuu, akisujudu, akiswali Alfajiri 2, Adhuhuri 4, Alasiri 4, Magharibi 3 na ‘Ishaa 4? Je hayo yamo katika Qur-aan? Au ameyapata wapi ikiwa sio kutokana na Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) ambaye amesema:
((صلوا كما رأيتموني أصلي))
((Swalini kama mlivyoniona naswali)) [Al-Bukhaariy]
Au mafunzo ya Hajj na taratibu zake zote, je tumezipata wapi? Je yamo katika Qur-aan? Bali ni kutokana na mafunzo ya Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) aliposema:
((يا أيها الناس خذوا عني مناسككم)) صحيح الجامع
((Enyi watu, chukueni kwangu Manaasik zenu [utaratibu wa ibada ya Hajj])) [Muslim]
Hivyo atambue kuwa makatazo ya mwanamke kutoa mkono kusalimia mwanamue ni amri kutoka kwa Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) kama tunavyonukuu chini Hadiyth kutoka kwake na kukanusha ni kukufuru. Hivyo awe na tahadhari kubwa na pia aombe maghfira kwa Mola wake kwani hakika ni jambo linalohitaji ili arekebishe ‘Aqiydah (Iymaan) yake.
عن معقل بن يسار يقول : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( لئن يطعن في رأس أحدكم بمخيط من حديد خير له من أن يمس امرأة لا تحل له )) رواه الطبراني في " الكبير الحديث : قال الألباني عنه في " صحيح الجامع : صحيح
Imesimuliwa kutoka kwa Ma’qil ibn Yaassar ambaye amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Mmoja wenu kudungwa kichwa kwa sindano ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiyeruhusiwa kwake)) [At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’]
Jambo hili limekuwa ni mazoea katika jamii yetu na linaonekana ni jambo la kawaida na kuliacha huwa ni kama muhali kwa mtu kukhofu kuwa atakuwa amemdharau mwanamume asipopokea mkono wake anaposalimia. Inampasa Muislamu aondoshe fikra hii ambayo ni wasiwasi wa Shaytwaan na abakie thabiti katika Iymaan yake ya utiifu wa amri wa Mola wake na asione aibu kwani Allaah Haoni aibu katika haki. Anaweza kuota udhuru kwa upole bila ya kumuumiza hisia zake na kufahamisha mwanamume kjuwa ni jambp lisiloruhusiwa kisheria kutendeka.
Inapasa tutambue kwamba kutokufuata amri za mafunzo ya dini yetu kama haya yataleta natija zifuazo:
-
Kupata madhambi kwa kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
-
Kuendeleza maasi katika jamii ikiwa wengi wanaendelea kufanya, ama ikiwa kila mmoja ataacha ndipo maasi kama haya yatakaposita kuendelea.
-
Kukataa kutoa mkono itakuwa ni mafunzo kwa wale ambao hawajui sheria hii na hivyo itakuwa mwenye kuanza kukataa katimiza amri ya Rabb wetu na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kukataza maovu na kuamrishana mema.
-
Kupeana mikono husababisha fitna ya matamanio baina ya mwanamke na mwanamume na hata kusababisha kuingia katika maasi ya zinaa.
-
Mwanamke atapata heshima zaidi kwa huyo mwanamume kuona kwamba amethamini mafunzo ya dini yake na kuonekana kuwa ni mwenye kujua sheria za dini badala ya kumdharau.
Mfano mzuri kabisa tunao kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyopata usimulizi kadhaa ufutao:
"Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema: “Waumini wanawake walipohamia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakifanyiwa mtihani kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu a Ta'aalaa) :
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا جَاءَكَ الْمُؤْمِنَاتُ يُبَايِعْنَكَ عَلَىٰ أَن لَّا يُشْرِكْنَ بِاللَّـهِ شَيْئًا وَلَا يَسْرِقْنَ وَلَا يَزْنِينَ وَلَا يَقْتُلْنَ أَوْلَادَهُنَّ وَلَا يَأْتِينَ بِبُهْتَانٍ يَفْتَرِينَهُ بَيْنَ أَيْدِيهِنَّ وَأَرْجُلِهِنَّ وَلَا يَعْصِينَكَ فِي مَعْرُوفٍ ۙ فَبَايِعْهُنَّ وَاسْتَغْفِرْ لَهُنَّ اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Ee Nabiy! Wakikujia Waumini wa kike wanafungamana nawe ahadi ya utiifu kwamba hawatomshirikisha Allaah na chochote, na wala hawatoiba, na wala hawatozini, na wala hawataua watoto wao, na wala hawatoleta usingiziaji wa kashfa walioizua baina ya mikono yao na miguu yao na wala hawatakuasi katika mema; basi pokea ahadi yao ya utiifu, na waombee maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Mumtahinah: 12]
Akasema ‘Aaishah: yeyote katika waumini wanawake aliyekubali hayo na akapasi walipokubali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia: ((Nendeni kwani mmetimiza kiapo cha utiifu)) Hapana! Naapa kwa Allaah, mkono wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haukugusa mkono wa mwanamke yeyote bali walitoa viapo vyao vya utiifu kwa maneno pekee”. Kisha ‘Aaishah akasema: “Naapa kwa Allaah, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokea viapo vya utiifu kwa njia Aliyoitolea sheria Allaah na mkono wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haujapata kugusa mkono wa mwanamke yeyote. Alipofungamana nao viapo vya utiifu alisema: ((Nimekubali kiapo chako cha utiifu [kwa matamshi])) [Muslim]
Vile vile:
عن أميمة ابنة رقيقة قالت : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((إني لا أصافح النساء)) رواه النسائي وابن ماجه وصححه الألباني " صحيح الجامع
Imetoka kwa Umaymah bint Raqiyqah ambaye amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mimi sisalimiani na wanawake kwa kupeana nao mkono) [An-Nasaaiy, Ibn Maajah na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh al-Jaami’]
Tunatumai kuwa dalili hizo zitakuwa ni mafunzo miongoni mwa ndugu zetu ambao wana tabia hii ya kuamkiana kwa mikono na wanaume wasio mahram wao ili wabakie katika radhi za Rabb wao na pia kuepukana na madhara yake.
Na Allaah Anajua zaidi