Mdhukuru Allaah Kwa Wingi Na Omba Maghfirah Baada Ya Kutenda Mema Katika Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah
Mdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) Kwa Wingi Na Omba Maghfirah
Baada Ya Kutenda Mema Katika Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚ
Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika. [Al-Baqarah:203]
Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: "Siku zinazohisabiwa ni siku za Tashriyq" (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) [Al-Qurtwubiy: 3.3] Kwa maana ni siku ya pili, ya tatu na ya nne baada ya siku ya 'Iyd.
Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) baada ya kusherehekea siku kuu yetu ya 'Iydul-Adhwhaa ('Iyd ya kuchinja) ni amri Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na hivi ndivyo ilivyo desturi ya ‘ibaadah zetu kuwa zinamalizika kwa kuambatana na mema na si kwa maasi.
Mahujaji wanapotekeleza Hajj ipasavyo na wanapomaliza kisimamo cha 'Arafah, huwa wameghufuriwa madhambi yao kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن عائشة رضي الله عنها عن النبي صلى الله عليه وسلم قال :((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبدأ من النار من يوم عرفة، وإنه ليدنو ثم يباهي بهم الملائكة فيقول: ما أراد هؤلاء؟)) مسلم
Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Hakuna siku ambayo Allaah Huwaacha waja huru zaidi kutokana na moto kama siku ya 'Arafah, na siku hiyo Allaah Hukaribia [Huteremka katika mbingu ya dunia kwa namna inayomstahiki Yeye] kisha kwa fakhari Husema kwa Malaika Wake: “Wanataka nini hawa” [waja wangu])) [Muslim]
Na katika usimulizi ufuatao pia imetajwa kufughuriwa kwao madhambi:
عن أبي هريرة رضي الله عنه ((إن الله تعالى يباهي بأهل عرفات ملائكة السماء ، يقول : انظروا إلى عبادي ، أتوني شعثا غبرا من كل فج عميق ، أشهدكم أني قد غفرت لهم)) المصدر: حلية الأولياء خلاصة الدرجة: صححه شيخ الباني
Kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ((Allaah Huwafakharisha watu (waliosimama) 'Arafah kwa Malaika wa mbinguni na Husema: Watazameni waja Wangu waliokuja wamejaa nywele, wana mavumbi, wamekuja kutoka kila pande (za dunia) Nakushuhudieni kuwa Nimewaghufuria)) [Hilyat al-Awliyaa – Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Swahiyh]
Lakini juu ya kuwa wameghufuriwa, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaamrisha Mahujaji wamdhukuru kwa wingi na waombe maghfirah Kwake baada ya kumaliza Hajj kama Anavyosema:
فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ ۖ وَاذْكُرُوهُ كَمَا هَدَاكُمْ وَإِن كُنتُم مِّن قَبْلِهِ لَمِنَ الضَّالِّينَ ﴿١٩٨﴾
Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafaat mdhukuruni Allaah kwenye Mash’aril-Haraam (Muzdalifah) na mdhukuruni Yeye kama Alivyokuongozeni kwani hakika mlikuwa kabla ya hapo ni miongoni mwa waliopotea.
ثُمَّ أَفِيضُوا مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٩٩﴾
Kisha miminikeni kutoka pale wamiminikapo watu; na ombeni maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.
فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا
Mtakapomaliza kutekeleza manaasik (‘ibaadah za Hajj) zenu, basi mdhukuruni Allaah kama mnavyowadhukuru baba zenu au kumdhukuru zaidi. [Al-Baqarah: 198-200]
Amri hii ya kuomba maghfirah na kumdhukuru kwa wingi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kila baada ya amali njema tunapata katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.
Haya ni mafunzo kwetu kujidhalilisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuishi daima katika hali ya khofu na matarajio (al-khawf war-rajaa). Na hivi ndivyo hali ya Waumini inavyopasa kuwa. Na Hadiyth zifuatazo zimethibiti:
حَدَّثَنَا أَبُو بَكْرٍ، حَدَّثَنَا وَكِيعٌ، عَنْ مَالِكِ بْنِ مِغْوَلٍ، عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ سَعِيدٍ الْهَمْدَانِيِّ، عَنْ عَائِشَةَ، قَالَتْ قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَهُوَ الرَّجُلُ الَّذِي يَزْنِي وَيَسْرِقُ وَيَشْرَبُ الْخَمْرَ قَالَ " لاَ يَا بِنْتَ أَبِي بَكْرٍ - أَوْ يَا بِنْتَ الصِّدِّيقِ - وَلَكِنَّهُ الرَّجُلُ يَصُومُ وَيَتَصَدَّقُ وَيُصَلِّي وَهُوَ يَخَافُ أَنْ لاَ يُتَقَبَّلَ مِنْهُ " .
'Aaishah (رضي الله عنها) alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ee Rasuli wa Allaah:
وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾
Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao. [Al-Muuminuwn: 60]
Je, huyo ni mtu ambaye anazini, anaiba na anakunywa pombe? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akajibu: “Sio ee bint wa Abubakar, (au) binti wa As-Swiddiyq! Lakini huyo ni mtu ambaye anafunga (Swiyaam), na anatoa swadaqa, na anaswali na huku anakhofu asitaqabaliwe. [Sunan Ibn Maajah].
Na Riwaaya nyengine:
حَدَّثَنَا ابْنُ أَبِي عُمَرَ، حَدَّثَنَا سُفْيَانُ، حَدَّثَنَا مَالِكُ بْنُ مِغْوَلٍ، عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ سَعِيدِ بْنِ وَهْبٍ الْهَمْدَانِيِّ، أَنَّ عَائِشَةَ، زَوْجَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَتْ سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَنْ هَذِهِ الآيَةِ : والَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ ) قَالَتْ عَائِشَةُ أَهُمُ الَّذِينَ يَشْرَبُونَ الْخَمْرَ وَيَسْرِقُونَ قَالَ " لاَ يَا بِنْتَ الصِّدِّيقِ وَلَكِنَّهُمُ الَّذِينَ يَصُومُونَ وَيُصَلُّونَ وَيَتَصَدَّقُونَ وَهُمْ يَخَافُونَ أَنْ لاَ يُقْبَلَ مِنْهُمْ أُولَئِكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ " . قَالَ وَقَدْ رُوِيَ هَذَا الْحَدِيثُ عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ سَعِيدٍ عَنْ أَبِي حَازِمٍ عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم نَحْوَ هَذَا .
Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Sa’iyd bin Wahab Al-Hamdaaniyy kwamba ‘Aaishah (رضي الله عنها) mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Aayah hii:
وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾
Na ambao wanatoa vile wavitoavyo na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao. [Al-Muuminuwn: 60]
‘Aaishah akasema: Je, hao ni wale wanaokunywa pombe na wanaoiba? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hapana ee bint wa Asw-Swiddiyq! Lakini hao ni wale wanaofunga (Swiyaam), na wanaswali, na wanatoa swadaqa, na huku (pamoja na hayo yote) wanakhofu wasitaqabaliwe.” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaendelea kusema kwa kutaja Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ ﴿٦١﴾
“Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri, na wao ndio wenye kuyatanguliza.”
Tukiangaza katika Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tokea kuanza da'wah yake kama Rasuli wa Allaah, zile tabu alizopata, maudhi mbali mbali ya Makafiri wa Ki-Quraysh, watu wake kumtenga, kufukuzwa na kupigwa mawe na watu wa Twaaif, maafa mbali mbali yaliyomjaza huzuni kubwa, juhudi nzito za kupigana vita na Makafiri, na mengi mengineyo, hadi mwisho wa Fat-hu Makkah (Ufunguzi wa (kuitwaa) Makkah), makundi kwa makundi ya watu waliingia katika dini ya Kiislam. Mafanikio hayo yamechukua muda wa miaka 23 tokea alipopewa Urasuli Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kukaribia kufariki kwake. Tujiulize, je, baada ya kufaulu huko, ni jambo gani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimfunza afanye? Jibu ni uteremsho wa Suwrah tukufu ifuatayo:
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ ﴿١﴾
Itakapokuja nusura ya Allaah na ushindi.
وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّـهِ أَفْوَاجًا ﴿٢﴾
Na utawaona watu wanaingia katika Dini ya Allaah makundi makundi.
فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ﴿٣﴾
Basi sabbih kwa Himidi za Rabb wako na muombe maghfirah; hakika Yeye daima ni Mwingi mno wa kupokea tawbah. [An-Naswr: 1-3]
Ni Suwrah ya mwisho iliyoteremshwa kikamilifu [kauli ya ibn 'Abbaas katika Swahiyh Muslim]
Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe na hata Maswahaba walitambua kuwa hii ni alama ya kukaribia mauti yake.
Mfano mwengine mzuri tunao wa kipenzi cha Allaah (Khaliylul-Allaah) Nabiy 'Ibraahiym (alayhis-salaam) alipomaliza kujenga Ka'bah yeye na mwanawe Ismaa'iyl. Ka'bah hiyo inayozungukwa (twawaaf) na mamilioni ya Waislamu kama ni ‘ibaadah tukufu tokea zama hizo hadi siku ya Qiyaamah. Lakini hawakutegemea kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawapokelea amali hiyo moja kwa moja, bali walimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awatakabalie kisha Awaghufurie. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٢٧﴾
Na (taja) aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’iyl msingi wa Nyumba (Al-Ka’bah): “Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.
رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٨﴾
“Rabb wetu, Tujaalie tuwe wenye kujisalimisha Kwako pamoja na kizazi chetu wawe ummah wenye kujisalimisha Kwako na Tuonyeshe taratibu za ‘ibaadah zetu na Pokea tawbah zetu, hakika Wewe ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah: 127-128]
Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa kila tunapomaliza Swalaah za fardhi tuombe maghfirah mara tatu kwa kusema:
أَسْـتَغْفِرُ الله
AtastaghfiruLLah
“Naomba maghfirah kwa Allaah”
Ikiwa hali ni kama hizo tulizozitaja, basi na sisi tutakapomaliza kutenda mema katika siku kumi bora kabisa za Allaah, za Dhul-Hijjah, au misimu yoyote ile ya 'Ibaadah kama baada ya Ramadhwaan, au kutenda 'amali njema zozote, inatupasa tuombe maghfirah na tumdhukuru kwa wingi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani hatujui kama ‘amali zetu zitakuwa zimetakabaliwa au laa. Desturi hii tuwe tunaidumisha daima tunapotoka kumaliza kutenda ‘amali na ‘ibaada zozote zile tuzifanyazo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuwezeshe kuzidisha juhudi kufanya mema mengi tukiwa na khofu na matarajio ya kukubaliwa amali zetu. Aamiyn,
wa biLLaahi At-Tawfiyq.