Zingatio: Tuishi Kiislam

 

Zingatio: Tuishi Kiislam

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Tofauti yetu na wasio kuwa Waislam si chengine kipya ila ni tabia. Uzuri wa mwenendo wa maisha yetu ndio utakaotupatia sifa mbele ya jamii isiyokuwa ya Waislam. Hima yetu ya kutosema uongo na kufuata maadili ya ajabu ndio utakuwa msingi imara wa imani yetu. Haya yote yameelezwa na kipenzi chetu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakuletwa yeye isipokuwa kurekebisha jamii kuwa na tabia njema.

 

Hakika Uislamu wetu umekamilika kwa kuwa na tabia bora za kuigwa na Waislam wenyewe kwa ushahidi wa Qur-aan na Sunnah.

 

Kama kweli sisi ni Waislam tunaoipenda diyn yetu ni lazima tuwe tayari kuanza kubadilika kila hatua ya maisha yetu kwa kuishi Kiislam. Zingatio letu litatupeleka hatua baada ya hatua ili kurekebisha nyumba iliyojikita kwenye masuala yasioendana kabisa na mila zetu sisi Waislam.

 

1. - Tuzungumze Kiislam 

Muislam wa kweli ni lazima awe ni mkweli, hatakiwi kuzua uongo, kufitinisha, kusengenya wala kuzungumza kwa sauti ya juu. Haya tunayapata ndani ya Qur-aan:

 

وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ ۚ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ ﴿١٩﴾

Na kuwa wastani katika mwendo wako, na teremsha sauti yako, hakika sauti inayokirihisha zaidi bila shaka ni sauti ya punda. [Luqmaan: 19]

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kushikamana katika kusema ukweli:

 

 “Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Jannah.” [Muslim]

 

2. - Tule Kiislam 

Muislam anatakiwa ale kilicho mbele yake kwa kutumia mkono wa kulia na asiwe na papara ya kusukuma tonge namna ya kima anavyokula. Aanze kula kwa kusema “BismiLlaah” na amalize kwa kusema “AlhamduliLlaah”. Chakula cha Muislam ni lazima kiwe ni cha halali, hatakiwi kula ovyo ovyo kama wanavyofanya wasiokuwa Waislam. Anapokula aligawe tumbo lake kwenye thuluthi tatu. Thuluthi moja ni ya chakula, nyengine ni ya maji na mwisho ni hewa. Hii ni kwa mujibu wa dalili ya Hadityh:

 

"Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” [At-Tirmidhiy].

 

3. - Tusikilize Kiislam 

Muziki ni haramu na haifai kwa Muislam kuutengeneza, kutengenezewa, kuimba, kuimbiwa, kuutangaza, kuupeleka muziki, kuuza, kula thamani yake, kununua na kuuza. Muziki umekuwa ni tatizo kubwa kwa Waislam kwani wengine hata usingizi hawapati bila ya kusikiliza muziki. Nyumba za Kiislam sasa zimekuwa sawa na magofu kwa kutopatikana maadili ya Kiislam. Kwani wengi wanaishi tofauti na mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu kwa Waislam wakawa wanasoma Qur-aan kila siku kwa sauti na kwa kusikilizana kwa mtindo wa dawaar (mmoja baada ya mwengine). Tuzibadilishe nyumba zetu kwa kusikiliza idhaa za Kiislam zisizokuwa na mambo ya uchafu na uzushi.

 أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤﴾

Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali. [Al-Muzammil: 4]

 

Muislam anayesoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika na Rusuli (‘Alayhim-salaam). Hata yule asiyejua kusoma Qur-aan ni vyema akawa na jitihada ya kujifundisha ilhali anakosea au hata kuchekwa. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Rusuli (‘Alayhims-salaam) na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira mara mbili”. [al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa)]

 

4. - Tuvae Na Tutembee Kiislam

Maringo ya kutembea bila ya shaka yanatokana na mtu kuvaa nguo za kifakhari ambazo hazitakiwi kuvaliwa kwa Muislam. Muislam wa kiume anatakiwa avae nguo zisizoburura. Mwanamke hatakiwi kuonekana zaidi ya viganja vya mikono na kipaji cha sura yake. Mapambo yote ni halali kwa mumewe na walio Maharimu wake. Haitakikani Muislam kutembea kwa kujivuna, kujifakharisha na maringo. Hivi sivyo Uislam unavyotufundisha kuishi. Qur-aan inasema:

وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا ﴿٣٧﴾

Na wala usitembee katika ardhi kwa majivuno. Hakika wewe huwezi kupasua ardhi, na wala huwezi kufikia urefu wa milima. [Al-Israa: 37]

 

Usiwaangalie watu kwa jeuri au kwa upande mmoja wa uso. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾

Na wala usiwageuzie watu uso wako kwa kiburi, na wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye kujivuna mwenye kujifakharisha. [Luqmaan: 18]

 

5. - Tujenge Urafiki Wa Kiislam

Miongoni mwa matatizo makubwa ya vijana wetu pamoja na Waislam kukosa maadili ya Kiislam ni kuwa na marafiki wasiokuwa na maadili mema. Ni vyema Muislam akawa hana rafiki hata mmoja kuliko kuwa na marafiki kumi wasioishi Kiislam. Kuishi Kiislam yatakikana juhudi na inaanza kwa kuwa na rafiki mwema atakayekukemea unapofanya kosa na kukupa maneno ya subra wakati wa huzuni.

 

Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwa sababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na diyn yetu.

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unayemfanya rafiki.”  [Abuu Daawuud na At-Tirmidhiy]

 

6. - Tulale Kiislam

Tumalizie kwa kuona namna anavyotakiwa Muislam kuimaliza siku yake kwa kujipumzisha Kiislam. Muislam anatakiwa atie wudhuu kabla ya kulala, wudhuu unaendana na Sunnah ya kupiga mswaki. Ni vizuri ukaswali rakaa tatu za witri (kwa wasioamka usiku).

 

Alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suwrah Al-Ikhlaasw, na Suwrah Al-Falaq, na Suwrah An-Naas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele (akifanya hivyo mara tatu).

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani Allaah Ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shaytwaan mpaka asubuhi”

 

Unapolala ulaze ubavu kwa upande wa kulia na usome du’aa ifuatayo: 

 

اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وا جْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت

“Ee Allaah nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulichokiteremsha na Nabiy wako uliyemtuma”.

 

Na hizi hapa Nyiradi za Kulala 

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

028-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Kulala

 

 

 

Bila ya shaka tutakapoishi Kiislam tutakuwa mbali na wasiokuwa Waislam. Hivyo maisha yetu yatakuwa hakika ni ya Kiislam. Kila kitu yatakikana juhudi na inaanza kwa nafsi kujifunga kukubali mafundisho ya Kiislam. Inawezekana kubadilika kwa kuishi Kiislam. Anza sasa, katu usichelewe kuishi Kiislam.

 

Share