Kujifunza Tajwiyd Kwa Kufuatilia Wasomaji
Kujifunza Tajwiyd Kwa Kufuatilia Wasomaji
SWALI:
Nawashukuru sana kwa kuweza kutusaidia kujibu majibu yetu na inshaAllaah jaza yenu iko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Mimi ni miongoni wa wanafunzi niliosoma Quraan zamani sana. Na wakati ule tulikuwa tunasomeshwa tu, hatujui wapi katika harufu, kunavutwa, wapi kuna kikomo, n.k. Sikama sasa ambapo wanafunzi wanafundishwa sawa sawa.
Si mlaumu mtu kwa hili na namshukuru mwalimu wangu wa mwanzo kunifundisha mimi Quraan na jaza yake iko kwa Allaah na Mungu amrehemu na amuweke penye wema (Amin) Sasa mimi hujaribu kusikiza na kufuata quran inaposomwa na masheikh kwenye CDS, ili nipate kujua wapi kunavutwa, shadda n.k na alhamdullillah nime improve sana. Je ninafanya sawa kufanya hivi ama mutanipa ushauri gani?
Jakaza Allaah
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Bila shaka unafaa upongezwe kwa juhudi nasi tunakuombea ufanikiwe na uwe ni mwenye kuisoma Qur-aan kwa njia iliyo bora zaidi.
Hakika zipo njia na mbinu nyingi za kujifunza Qur-aan. Mojawapo ni hiyo ambayo unaitumia kwa kufuatanisha msomi.
Hata hivyo, tungekunasihi upate mtu ambaye ni mjuzi wa Tajwiyd na kusoma Qur-aan awe anakusikiliza kadiri itakavyowezekana. Hiyo ni kuwa katika kufuatanisha inakuwa ni rahisi na yenye ufanisi zaidi kuliko mtu kusoma Qur-aan peke yake kwani si rahisi kuyajua makosa yake anapokosea.
Kujifunza Qur-aan ni muhimu sana na hata ikikubidi kuigharamia basi fanya hivyo. Na elimu hiyo yahitaji mazoezi sana na marudio ya kila mara, hivyo usiache kufanya hivyo unapojifunza.
Na Allaah Anajua zaidi