Wamezini Kisha Wakaoana Bila Kufanya Tawbah Kwa Kuwa Walikuwa Hawajui, Nini Hukmu Ya Ndoa Yao?

 

SWALI:

 

masheikh wangu mimi nnasuala langu ambalo linanitia wasiwasi.  kwa ufupi niliposa mwanamke na nilimtolea mahari wakati tunasubiri kufunga ndoa, tulifanya maskosa ya zinaa (tulizini), lakini kabla ya kufunga ndoa kama mwezi au zaidi hatukufanya kitendo hicho, huyo mwanamke alikuwa mbali na mimi. baadae siku ile iliyopangwa tukafunga ndoa na sasa ni muda wa miaka mingi.

Suala langu jee hii ndoa ni halali?  Kwani nimeona kwenye website yenu (alhidaaya ) kuwa lazima mnatakiwa mjute kwanza kabla ya kuowana. mimi nilokuwa nnajuwa kuwa kama mmezini basi mnaweza kuowa (na ndivyo nilivyo fanya).

jee kujuta huko ni vipi? Maana mimi nilikuwa siyajuwi hayo, nnachojuwa kuwa tulikuwa na nia ya kuowana, basi tumetimiza ile ahadi yetu, japokuwa tulifanya makosa (inshaalah ALLAAH atatusamehe), tulifanya haramu na kuigeuza iwe katika uhalali.

Wasiwasi wangu nini nifanye? Kwani naogopa kuwa bado nimo katika zinaa hata ibada zangu zikawa hazikubaliki na pia tumebahatika kupata mtoto hivi karibuni tuu, jee mtoto huyu ni wa halali au laa. Ningependelea kupata jawabu kwenu ili nijuwe nini nnafanya.

Sina cha kukulipeni lakini ALLAAH ndie atakupeni funguleni kwa kutusaidia sisi kutatuwa matatizo yetu. Ameen

Wasaalamu alykum

 



 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako na kutaka kwako kupata ufumbuzi wa masuala hayo mazito. Ni ajabu kuwa mwanadamu katika maumbile yake ya papatiko anakuwa ni mwenye kujiingiza katika maangamivu. Ni ajabu kuona mtu anazini na mchumba wake na hali anajua atamuoa na hivyo inasikitisha kuona mwanaadam alivyo na uchu wa maasi na kukosa subira kwa jambo ambalo baada ya muda mfupi litakuwa halali kwake kishari'ah.

 

Na yaliyotokea ni natija ya Muislamu kukosa subira ambayo tumehimizwa sana tuwe nayo.

 

Tawbah ni lazima kwa kila dhambi analofanya Muislamu, naye Allaah Aliyetukuka Amechukua dhamana ya kusamehe madhambi yote kama tunavyokuta katika Aayah mbalimbali za Qur-aan.  

 

Ama masharti ya tawbah ni haya yafuatayo:

1.    Kujiondoa katika maasiya.

2.    Kujuta kwa kufanya maasiya.

3.    Kuazimia kutorudia tena katika hayo maasiya.

Yaonyesha kutoka katika maelezo yako kuwa mlitengana na mchumba wako au mlijiondoa katika maasi baada ya matendo hayo ya zinaa, ikiwa kutengana huko ni kwa Niyah ya kutubu kutokana na matendo hayo, basi ulishatimiza sharti moja. Sharti ambalo limebakia ni kujuta kwenu na kwa sababu hukuwa na elimu juu ya hilo Allaah Aliyetukuka Anasamehe kwa madhambi yaliyofanywa katika hali ya ujinga. Anasema Aliyetukuka:

Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Allaah Huwakubalia tawbah yao, na Allaah ni Mjuzi na ni Mwenye hikima” (4: 17).

 

Kwa kuwa sasa umejua uwajibu wa jambo hilo inafaa ujute sana ndani ya moyo kwa kufanya matendo hayo machafu huko nyuma, na kisha jitahidi sana utende yaliyo mema pamoja na kuleta istighfaar kwa wingi.

 

Ikiwa ndoa yenyewe baada ya zinaa ilitekeleza masharti ya ndoa kama ifuatavyo ndoa yenyewe itakuwa ni sawa:

1.    Kukubali kwa msichana anayeolewa.

2.    Bwana harusi kukubali kwa ndoa hiyo.

3.     Bibi harusi kupewa mahari yake.

4.    Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

5.    Kuwepo na kupatikana idhini ya walii.

 

Endelea kuomba msamaha na kufanya mema wala usitie wasiwasi kwa yaliyopita yafaa kwa sasa uganje yajayo. Uhalali wa mtoto inategemea je, mimba yenyewe iliingia kabla ya kumuoa baada ya kitendo cha zinaa au baada yake. Ikiwa iliingia kabla basi mtoto hatokuwa wako kishari'ah, na hatoweza kukurithi wala wewe kumrithi lakini ikiwa mimba ilipatikana baada ya Nikaah ya halali, basi mtoto huyo atakuwa wa halali.

 

Na ikiwa mlikuwa tu mumeacha maasi yale kwa muda kwa ajili ya kusubiri kuoana bila ya Niyah wala maazimio ya kutubia na kujutia yale makosa mliyoyafanya, basi Maulamaa wanaonelea ikiwa mko ndani ya ndoa yenu hivi sasa, ni bora na kwa usalama zaidi kufanya ndoa mpya ambayo atakuwepo walii na mashahidi wawili. Vilevile wanaonelea kuwa ikiwa mtu atashindwa kabisa kueleza sababu ya hiyo ndoa mpya kwa watu na hao wahusika wa kuisimamia ndoa hiyo kwa kuogopa madhara zaidi na mengineyo yanayoweza kuleta matatizo, basi wanaweza kuendelea na ndoa yao na huku wakizidisha sana istighfaar na kutenda mambo mema kwa wingi.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atusamehe sote katika madhambi tuliyoyafanya kwa kujua au kutojua.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share