Adhabu Za Kaburi Katika Qur-aan Na Hadiyth
Adhabu Za Kaburi Katika Qur-aan Na Hadiyth
SWALI:
Ningependa kuelemishwa kuhusu adhabu ya kaburi kwa Quran na hadithi.
jazakumullah
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hawa ni watu ambao wanatilia shaka Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu moja au nyingine. Na huenda wakaona adhabu hiyo haieleweki wala haingii katika akili ya mwanadamu kwa mawazo yao.
Hata hivyo, Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zipo wazi kabisa katika suala hili. Hebu tutizame dalili zifuatazo:
a). Allaah Aliyetukuka Anasema:
فَوَقَاهُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِ مَا مَكَرُوا ۖ وَحَاقَ بِآلِ فِرْعَوْنَ سُوءُ الْعَذَابِ﴿٤٥﴾ النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ﴿٤٦﴾
Basi Allaah Akamlinda na maovu ya yale waliyoyapangia njama, na watu wa Fir’awn ikawazunguka adhabu mbaya kabisa. Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa (itasemwa): Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa. [Ghaafir: 45 – 46]. Hii Aayah iko wazi kabisa kuwepo kwa adhabu ya kaburi kabla ya Siku ya Qiyaama.
b). Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ قَالَ أُوحِيَ إِلَيَّ وَلَمْ يُوحَ إِلَيْهِ شَيْءٌ وَمَن قَالَ سَأُنزِلُ مِثْلَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ ۗ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ ﴿٩٣﴾
Na nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemtungia uongo Allaah au akasema: Nimefunuliwa Wahy na hali hakufunuliwa Wahy wowote. Na yule asemaye: Nitateremsha mfano wa yale Aliyoyateremsha Allaah. Na lau ungeliona madhalimu pale wakiwa katika mateso makali ya mauti, na Malaika wamenyosha mikono yao (wakiwaambia): Toeni nafsi zenu! Leo mnalipwa adhabu ya kudhalilisha kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki, na mlikuwa mkitakabari kuhusu Aayaat Zake. [Al-Anaam: 93]. Hotuba hii ni kwa madhalimu wanapokuwa katika mauti, wakijulishwa kuwa wataadhibiwa siku hiyo hiyo ya kuaga dunia kwao. Lau kama adhabu ingeakhirishwa mpaka Siku ya Qiyaama, hawangeambiwa: “Leo mnalipwa”. Hii ni dalili kuonyesha ipo adhabu ya kaburi.
c). Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٧﴾
Na hakika wale waliodhulumu watapata adhabu nyingine isiyokuwa hiyo, lakini wengi wao hawajui. [Atw-Twuwr: 47].
Aayah hii inaonyesha kuwa adhabu ya kwanza ni ile ya kaburini, kwani haitakuwa sawa kuifasiri kuwa ni adhabu katika maisha haya kwani madhalimu wengi hawaadhibiwi hapa duniani.
d). Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ ۖ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ ۖ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ ۖ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ ۚ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَىٰ عَذَابٍ عَظِيمٍ﴿١٠١﴾
Na katika Mabedui wanaokuzungukeni wako wanafiki. Na katika watu wa Madiynah (pia) walibobea katika unafiki. Huwajui (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Sisi Tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili; kisha watarudishwa katika adhabu kuu. [Al-Tawbah: 101].
Adhabu ya kwanza katika Aayah inahusu adhabu ya hapa duniani na ya pili ni adhabu ya kaburi. Kisha Allaah Aliyetukuka Anasema: “Kisha watarudishwa kwenye adhabu kuu”, ina maana ya adhabu ya Siku ya Qiyaamah.
Dalili katika Sunnah kuhusiana na adhabu ya Kaburi ni kama zifuatazo:
1-Amesimulia Ibn 'Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyapitia makaburi mawili na akasema: “Hakika hawa wawili wanaadhibiwa, na wala hawaadhibiwi kwa sababu ya jambo kubwa (la kuwashinda kulitekeleza au kujiepusha nalo).” Kisha hapo hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Hapana! Bali ni kubwa (dhambi kubwa na adhabu zake)! Ama mmoja wao, huyu alikuwa akipita kufitinisha watu, na ama mwingine, huyu alikuwa hajikingi na mkojo wake [anapokojoa].” [Al-Bukhaariy na Muslim]
2-Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Nimeteremshiwa wahyi kuwa watu wako watatiwa katika mtihani sawa na mtihani wa ad-Dajjaal, makaburini mwenu. Lau haingekuwa kwa sababu ya kwamba mtaacha kuzika wafu wenu makaburini kwa kusikia adhabu humo ambayo naisikia, hakika ningefanya nanyi muisikie" [Muslim].
3-Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema tena: “Mmoja wenu anapomaliza tashahhud ya mwisho aombe ulinzi wa Allaah kwa mambo manne: Adhabu ya moto (wa jahannam); adhabu ya kaburi; mtihani wa maisha na kifo; na shari ya mtihani wa Masihi ad-Dajjaal” [Muslim].
Ni muhimu kuhimiza hapa kuwa Hadiyth zote hizi ni sahihi zilizopokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa isnadi zilizo sahihi na wapokezi wenye kutegemewa. Ifahamike kuwa yeyote asiyeamini basi yuko katika hatari kubwa. Shaykh wa Uislamu, Ibn Taymiyyah, amesema: "Zipo Hadiyth sahihi nyingi zinazothibitisha kuwepo kwa adhabu na raha kaburini kwa anayestahiki. Pia kusualiwa (kuulizwa) kaburini na Malaika wawili ni hakika na kweli".
Jambo hili la ghaybu ni muhimu kila Muislamu awe ni mwenye kuliamini bila tashwishi yoyote ile. Hilo tuelewe kuwa lipo mbali na kuweza kuelewa na mwanaadamu mwenye mapungufu mengi.
Na Allaah Anajua zaidi