Mwanamke Asiyempambia Mumewe Bali Anajipamba Akienda Harusini
Mwanamke Asiyempambia Mumewe Bali Anajipamba Akienda Harusini
SWALI:
Je nawaulizaje kwani ikiwa mtu anaolewa na pia hampambi mumee, akijipamba huwa yuwenda harusini, hata kujifukiza hafanyi angoja mpaka harusi je huyo mtu ana makosa? Ama dhambi?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hili ni suala muhimu la kijamii ambalo lau halitatekelezwa na wanandoa huwa linasababisha maafa na hata wanandoa hao kuachana.
Hapana budi si kwa mke pekee bali mume pia kujipamba. Wanandoa daima wanafaa wawe safi daima kila mmoja kwa ajili ya mwenzake. Kujipamba huku ni kwa kuvaa vizuri na kujitia manukato.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimependeshewa katika dunia yenu wanawake na vitu vizuri vilivyosalimika na uchafu (manukato)” [An-Nasaaiy]
Kujipamba kunarithisha mapenzi na hujenga na kukuza sababu zote zinazopelekea katika kuzoeana. Kisha kumbuka, “Allaah Hupenda yaliyo mazuri” [Muslim na at-Tirmidhiy].
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:
“Mimi napenda kujipamba kwa ajili ya mke wangu kama nilivyokuwa napenda yeye ajipambe kwa ajili yangu”.
Kujipamba ni haki ya wanandoa wote wawili – mwanamme na mwanamke. Ni vizuri sana tusilidharau jambo hili la kujipamba na kuona si la muhimu kwani mwenye kuhitajia maisha ya furaha ya ndoa na yenye matokeo mazuri hana budi kujishughulisha na kujipamba.
Kwa mukhtasari, ikiwa mke hajipambi ila anapokwenda harusini atakuwa anapata dhambi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama vile atakavyopata mume ikiwa naye atafanya hivyo. Haifai kwa mwanamke kujipamba anapotoka nje kwenda kuonyesha mapambo yake kwa wengine kwani anayestahiki kufurahishwa na mapambo hayo ni mume tu. Nasaha yetu kwa wanandoa ni kuwa wapambiane ili wapate thawabu na waepukane na madhambi kwa kutopambiana.
Na Allaah Anajua zaidi