008-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kukaa Na Kusimama Katika Swalah Ya Usiku (Tahajjud)
KUKAA NA KUSIMAMA KATIKA SWALAH YA USIKU (TAHAJJUD)
Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa (mara) akiswali usiku mrefu akiwa amesimama na (mara nyingine) akiswali usiku mrefu kwa kukaa. Na alikuwa anaposoma kwa kusimama, hurukuu kwa kusimama, na anaposoma kwa kukaa, hurukuu kwa kukaa.[1]
Na wakati mwengine, alikuwa anaswali kwa kukaa, na husoma hivyo hivyo huku amekaa. Na inapobakia katika kisomo chake kiasi cha Aayah thalathini au arubaini hivi, husimama na kuzisoma kwa kusimama, halafu hurukuu na kusujudu. Kisha hufanya hivyo hivyo katika Raka'ah ya pili.[2]
Bali aliswali Asw-Swubha (Swalah ya Asubuhi)[3] kwa kukaa chini katika siku za mwisho za maisha yake alipokuwa katika umri mkubwa, na na hilo lilikuwa kabla ya kufariki kwake kwa mwaka mmoja.[4]
Vile vile alikuwa akikaa kwa kukunja miguu (mkao wa chuoni).[5]
[1] Muslim na Abu Daawuud.
[2] Al-Bukhaariy na Muslim.
[3] Ni Swalah ya Sunnah (usiku au jioni) imeitwa hivyo kutokana na yaliyokuwemo humo ya tasbiyh (Kumtukuza Allaah).
[4] Muslim na Ahmad.
[5] An-Nasaaiy, Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake (1/107/2), 'Abdul-Ghaaniy Al-Maqdisi katika Sunan yake (80/1) na al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy amekubali.