Hali Ya Nyuso Za Swaalihina Na Waovu Siku ya Qiyaamah

Hali Ya Nyuso Za Swaalihina Na Waovu Siku ya Qiyaamah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Baada ya Kauli za Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾ وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ﴿٥٤﴾ وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٥٥﴾ أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ﴿٥٦﴾ أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ﴿٥٧﴾ أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٥٨﴾

 

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. Na rudini kila mara kutubu kwa Rabb wenu na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa. Na fuateni yaliyo mazuri zaidi ambayo mmeteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu kabla haijakufikieni adhabu ghafla na hali nyinyi hamhisi. Isije nafsi ikasema: Ee majuto yangu kwa yale niliyokusuru katika upande wa Allaah! Na hakika nilikuwa miongoni mwa wenye kufanya masikhara. Au iseme :  Lau Allaah Angeliniongoa, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye taqwa. Au iseme pale itakapoiona adhabu: Lau ningelikuwa na fursa ya kurudi (duniani) basi ningekuwa miongoni mwa wafanyao ihsaan. [Az-Zumar: 53- 58]

 

 

Hapo nafsi iliyojidhulumu akafikia katika khasara na majuto kubwa, atakumbushwa ujeuri wake aliokuwa nao alipokuwa duniani kwa kutokukubali haki;

 

بَلَىٰ قَدْ جَاءَتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ﴿٥٩﴾

(Ataambiwa) Ndio! Kwa yakini zilikujia Aayaat Zangu ukazikadhibisha, na ukatakabari na ukawa miongoni mwa makafiri. [Az-Zumar: 59].

 

Maana; Ee unayejuta uliyoyafanya, ukazifanya Aayah za Rabb wako pale zilipokufikia kuwa ni dalili na hoja bayana, pindi ulipokuwa duniani lakini ulizikanusha ukawa mjeuri sana kuzifuata ukawa miongoni mwa wale waliozikufuru. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Anaendelea Allaah (‘Azza wa Jalla) kusema:

 

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ﴿٦٠﴾

Na Siku ya Qiyaamah utawaona wale waliomsingizia uongo Allaah, nyuso zao zimesawajika. Je, kwani si katika Jahannam ndio makazi kwa ajili ya wanaotakabari? [Az- Zumar: 60]

 

Maana: Hao ni waliomkufuru Allaah (‘Azza wa Jalla) na  kumhusisha  kwa mambo ambayo Ameepukana Nayo wala Hayampasi   kama kumshirisha na viumbe Vyake, au kusema Ana msaidizi, au mtoto. Na hapa inahusu pia yeyote atakayemhusisha na sifa nyenginezo zisizokuwa ni Sifa Zake Allaah (‘Azza wa Jalla). 

 

Vile vile inamhusu atakayetunga Shariy’ah isiyokuwa ya haki inayomhusu Allaah (‘Azza wa Jalla) ikatangaa na kufuatwa na watu bila ya dalili. Lakini hii haiwahusu ‘Ulamaa wenye kuhukmu kwa Ijtihaad zao pindi   wanapokosea katika jitihada zao kwa kutumia Qiyaas inayokubalika katika Shariy’ah.

 

Wala haimpasi mtu kusema Allaah Kasema, au Kaamrisha jambo bila ya kutoa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

 

Siku ya Qiyaamah watagawanywa katika makundi mawili; Swaalihina (watu wema) na watu waovu. Na Allaah (‘Azza wa Jalla) Ametofautisha aina za nyuso za makundi hayo mawili; nyuso za Swalihina siku hiyo zitakuwa nyeupe zenye nuru, zinazong'ara na zenye furaha kama Anavyosema:

  

  وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُّسْفِرَةٌ ﴿٣٨﴾  ضَاحِكَةٌ مُّسْتَبْشِرَةٌ ﴿٣٩﴾   

Ziko nyuso siku hiyo zitanawiri. Zitacheka na kufurahika. ['Abasa: 38 - 39].

 

Na kama Anavyosema pia katika Suwratul-Ghaashiyah:

 

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاعِمَةٌ ﴿٨﴾  لِّسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ ﴿٩﴾

Na nyuso Siku hiyo zitakuwa ziko katika taanisi. Wakiridhika na juhudi zao. [Al-Ghaashiyah: 8-9].

 

 

Ama nyuso za watu waovu zitakuwa ni nyeusi zenye kuchoka, na zilizojaa huzuni kwa majuto:

 

وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ ﴿٤٠﴾ تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ ﴿٤١﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ ﴿٤٢﴾

Na ziko nyuso siku hiyo zitakuwa na vumbi juu yake. Zitafunikwa na giza totoro. Hao ndio makafiri waovu ['Abasa: 40 - 42].

 

 

Na pia

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ ﴿٢﴾ عَامِلَةٌ نَّاصِبَةٌ ﴿٣﴾

Nyuso siku hiyo zitadhalilika. Zenye kufanya kazi ngumu na kuchoka mno. [Al-Ghaashiyah: 2 – 3].

 

*******

 

Share