Ijumaa: Kuanzisha Swalaah Ya Ijumaa Chuoni Kwa Vile Khutbah Inatolewa Msikitini Kwa Lugha Geni

 

SWALI:

 

Assalam alaykum, tunashukuru sana kwa msaada wenu wa kuweza kujibu maswali yetu, ALLAH SUBHANNA WA TAALA awape tawfiq muendelee.

MIMI NI MWANAFUNZI NILIYEPO NJE YA TANZANIA, KATIKA CHUO CHETU TUPO WAISLAMU (foreign students) KATI YA 10 HADI 20 AMBAO HUSWALI PAMOJA SWALA YA IJUMAA CHUONI, HUFANYA HIVYO KWANI 1: MSIKITI UPO MBALI KIDOGO. 2: WAKATI WA MCHANA HUWA TUNA VIPINDI HUCHELEA KUCHELEWA DARASANI, 3: KHUTBA INAYOTOLEWA HUKO MSIKITINI NI KWA LUGHA TUSIYOIFAHAMU SWALI: JE NI SAHIHI KUFANYA HIVYO?

 

NAWAOMBENI MUNIJIBU KWA HARAKA ILI TUWEZE KUONDOKANA NA WASIWASI JUU YA SWALI HILI

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Swalah ya Ijumaa. Tunawatakia kila la kheri ndugu zetu ili muweze kuhifadhi Dini yenu katika nchi ya ugenini.

 

Hakika ni kuwa khutbah na mkusanyiko wa Ijumaa hauna lengo la kupata mafundisho siku hiyo (ingawa ni bora) bali ni mkutano baina ya Waislamu wa sehemu wanayoishi. Hii sababu ya pili ni nzito zaidi hata kupata yaliyomo ndani katika khutbah yenyewe. Kwa kuwa nyinyi mpo katika nchi ya kigeni mnatakiwa mjuane na ndugu zenu katika nchi hiyo ili muweze kufahamiana na huenda mkasaidiana kwa mengi.

 

Ikiwa umbali wenyewe si mkubwa basi nasaha zetu kwenu ni kuwa muende katika Msikiti huo kwa Swalah hiyo kwani ni siku moja kwa wiki na ni masaa machache tu.

 

Na kusema kuwa mtakosa baadhi ya masomo ya siku hiyo sio neno ukilinganisha na yale ambayo mtayapata katika kuswali kwa Jama’ah Swalah ya Ijumaa. Haijapatikana katika maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na watangu wema watu kuswali katika hali hiyo mnayotaka kuswali kwayo.

 

Hata hivyo, ikiwa sehemu hiyo ni mbali sana, basi Uislamu haukuja ila ni kuwaondolea wanadamu uzito na mashaka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao” (7: 157).

 

Kwa kuondolewa uzito huo ikiwa chuo kimewapatia chumba ambacho kitabaki ni mswala kwa ajili ya Swalah zote na hata mkiondoka kitabaki hivyo. Katika hilo, sheria inawaruhusu nyinyi kuswali Swalah ya Ijumaa hapo. Hata hivyo inatakiwa kuwa kuwe na mtu ambaye anaweza kuongoza khutbah hiyo na Swalah. Swalah ya Ijumaa na khutbah ina masharti yake ambayo mnatakiwa muwe ni wenye kutekeleza kabla ya Swalah yenu hiyo kukubaliwa.

 

Ikiwa masharti hayo hayakutekelezwa basi itawabidi muswali Swalah ya Adhuhuri badala ya Ijumaa.

 

Soma zaidi kuhusu Swalah ya Ijumaa hapa chini:

 

Mambo Ya Kufanya Siku Ya Ijumaa

Khutba Ya Ijumaa Ikimpita Mtu Aswali Jamaa na Wengine?

Utukufu Wa Ijumaa

Imaam Kutoa Khutbah Ya Ijumaa Bila Ya Kusimama Katika Mimbar

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share