022-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Alivyokuwa Akisoma (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Swalah Mbalimbali. 1 - Swalah Ya Alfajiri
ALIYOKUWA AKISOMA (صلى الله عليه وآله وسلم) KATIKA SWALAH (MBALI MBALI)
Kuhusu Surah gani na Aayah gani aliyokuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiisoma katika Swalah, hilo linatofautiana kwa kutofautika kwa Swalah tano na Swalah nyenginezo. Basi chukua maelezo ya upambanuzi wake kwa kuanzia na Swalah ya kwanza katika Swalah tano:
1- SWALAH YA ALFAJIRI
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Surah([1]) ndefu za mufasswal([2]) hivyo alikuwa (wakati mwengine) akisoma Al-Waaqi'ah (56: 96) na mfano wake katika Rakaa mbili.([3])
Alisoma kutoka Surat-Twuur (52: 49) katika Hijjatul-Wadaa’ (Hijjah ya Kuaga).([4])
Mara nyingine, alikuwa akisoma Surat Qaaf [50: 45] na mfano wake [katika Rakaa ya mwanzo].([5])
Mara nyingine alikuwa akisoma Surah fupi za mufasswal kama:
((إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ))
((Jua litakapokunjwa)) [At-Takwiyr 81: 29)).([6])
Na mara moja alisoma:
((إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا))
((Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemeko wake!)). [Az-Zilzalah 99: 8)
katika Rakaa zote mbili, jambo lililomfanya msimulizi kusema: "Sielewi kama Mjumbe wa Allaah alisahau au aliisoma kwa makusudi.([7])
Alisoma mara moja akiwa safarini:
((قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ))
((Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko)). [Al-Falaq 113: 5]
na
((قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ))
((Sema: Najikinga kwa Mola wa wana Aadam)). [An-Naas 114: 6][8]
Akasema kumwambia 'Uqbah bin 'Aamir (رضي الله عنه): ((Soma Al-Mu'awwidhatayn([9])katika Swalah zako, kwani hakuna mwenye kutafuta kinga kama hiyo))([10]).
Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma zaidi ya hivo, kwani alikuwa akisoma Aayah sitini (60) au zaidi([11]). Baadhi ya wasimulizi wake wamesema: " Sielewi kama ilikuwa katika moja ya Rakaa mbili au katika zote mbili."
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Surat Ar-Ruum [30: 60]([12]) na mara nyingine akisoma Surat Yaasiyn [36: 83)([13]).
Mara moja aliswali Swalah ya Alfajiri Makkah, akaanza kusoma Suratul-Mu-minuun [23: 118] hadi alipofikia kutajwa Muusa na Haaruun au kutajwa 'Iysa([14]) -Msimulizi mmoja hakuwa na hakika- alianza kukohoa hivyo akarukuu([15]).
Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwaswalisha katika Swalah ya Alfajiri kwa kusoma Suratu Asw-Swaaffaat [77: 182]([16])
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiiswali Swalah ya Alfajiri siku ya Ijumaa kwa kusoma Surat As-Sajdah [32: 30] (katika Rakaah ya mwanzo na Rakaa ya pili) Surat Ad-Dahr [76: 31].([17])
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akirefusha Rakaa ya kwanza na kufupisha Rakaa ya pili.([18])
KISOMO KATIKA SUNNAH YA ALFAJIRI
Kisomo chake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri, kilikuwa chepesi mno([19]) hadi 'Aaishah رضي الله عنها) ) alikuwa akijiuliza kwa kusema: "Je, amesoma ndani yake Kifungulio cha Kitabu (Suratul Faatihah)?"([20]).
Mara nyingine alikuwa akisoma baada ya al-Faatihah katika Rakaa ya mwanzo ya hizo mbili Aayah hii:
((قُولُواْ آمَنَّا بِاللّهِ وَمَآ أُنزِلَ إِلَيْنَا ...))
((Semeni nyinyi: Tumemwamini Allaah na yale tuliyoteremshiwa sisi…)). [Al-Baqarah 2:136) mpaka mwisho wa Aayah.
(katika Rakaa ya kwanza,) na katika ya pili alikuwa akisoma Aayah:
((قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْاْ إِلَى كَلَمَةٍ سَوَاء بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ ...))
((Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi…)) [Al-'Imraan 3: 64] ([21]) mpaka mwisho wa Aayah.
Mara nyingine husoma badala ya Aayah ya pili:
((فَلَمَّا أَحَسَّ عِيسَى مِنْهُمُ الْكُفْرَ))
(('Iysaa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri)) [Al-'Imraan 3:52]([22]) mpaka mwisho wa Aayah.
Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Suratul-Kaafiruun [109 -6] katika Rakaa ya kwanza, na Suratul-Ikhlaasw [112-4] katika Rakaa ya pili.([23])
Pia alikuwa akisema: ((Hizi ni jozi bora kabisa za Surah (hizi)).([24])
Alimsikia mtu akisoma Surah ya mwanzo - Suratul-Kaafiruun - katika Rakaa ya kwanza, akasema: ((Huyu mja amemwamini Mola wake)). Kisha mtu huyo akasoma Surah ya pili - Suratul-Ikhlaasw - katika Rakaa nyengine, akasema: ((Huyu mja amemwelewa Mola wake)).([25])
[1] An-Nasaaiy na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[2] Sehemu ya saba ya mwisho ya Qur-aan, kuanzia Surah Qaaf (Namba 50) kama ilivyo rai yenye nguvu kabisa kama ilivyotangulia.
[3] Ahmad, Ibn Khuzaymah (1/69/1) na Al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahaby amekubaliana naye.
[4] Al-Bukhaariy na Muslim.
[5] Muslim na At-Tirmidhiy. Imetolewa pamoja na inayofuatia katika Al-Irwaa (345).
[6] Muslim na Abu Daawuud.
[7] Abu Daawuud na Al Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh. Kinachodhihiri ni kuwa yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) alifanya hivyo kwa makusudi ili kuthibitisha kujuzu kwake.
[8] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (1/76/1), Ibn Bushraan katika Al-Amaaliy na Ibn Abi Shaybah (12/176/1). Al-Haakim amesema kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahaby amekubaliana naye.
[9] Surah mbili za kujikinga; yaani Surah mbili za mwisho katika Qur-aan, zote zinaanzia na Qul-A'udhu…. (Sema najikinga….).
[10] Abu Daawuud na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[11] Al-Bukhaariy na Muslim.
[12] An-Nassaaiy, Ahmad na Al-Bazzaar kwa isnaad nzuri.
[13] Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[14] Muusa ametajwa katika Aayah ya 45: ((ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَى وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ)) na 'Iysa ametajwa katika Aayah ya 50: ((وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَى رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ))
[15] Muslim na Al-Bukhaariy katika Ta'aliyqan, nayo ni Hadiyth inayoondoshwa mwanzo wa isnaad yake msimulizi mmoja au zaidi kwa mfululizo kama ilivyoelezwa nyuma. Imetolewa katika Al-Irwaa (397).
[16] Ahmad na Abu Ya'laa katika Musnad zao, na Al-Maqdisiy katika Al-Mukhtaarah.
[17] Al-Bukhaariy na Muslim.
[18] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[19] Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[20] Al-Bukhaariy na Muslim.
[21] Muslim, Ibn Khuzaymah na Al-Haakim.
[22] Muslim na Abu Daawuud.
[23] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[24] Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah.
[25] Atw-Twahaawiy, Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake na Ibn Bushraan. Ibn Hajar amesema kuwa ni nzuri katika Al-Ahaadiyth Al-'Aaliyaat (Namba, 16).