Zingatio: Ibilisi Hakati Tamaa

 

Zingatio: Ibilisi Hakati Tamaa

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Imesimuliwa ya kwamba kulikuwa na mcha wa Allaah aliyependwa sana na watu wa wakati wake akiitwa Wadd. Alipofariki, swahiba zake walilizunguka kaburi lake huko Babylon kwa masikitiko makubwa. Ibilisi alipoona hilo, aliwashauri kumtengenezea sanamu ili wapate kumkumbuka.

 

Walikubaliana na hilo, hivyo likatengenezwa na kuwekwa mbele ya umma wa watu. Kizazi kilipokuja kuona namna sanamu la Wadd linavyotukuzwa, wakaamua kuweka sanamu hilo ndani ya kila nyumba. Baada ya kupita muda mrefu na pia kuondoka elimu ya Dini, watoto wa hao watu walikuja kuabudia masanamu hayo.

 

Kisa cha Wadd kinatudhihirishia ya kwamba hawakuanza kuabudia masanamu kwa ghafla moja tu. Walianza kidogo kidogo hadi kuingia kwenye shirki moja kwa moja. Na kisa hichi kinadhihirisha Qawl ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwamba Ibilisi ni adui aliye wazi kabisa: 

إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴿٥٣﴾

Hakika shaytwaan anachochea baina yao. Hakika shaytwaan kwa bin Aadam daima ni adui bayana. [Al-Israa: 53]

 

Ibilisi hana haraka ya kuwavuta viumbe na wala hakati tamaa, huanza kidogo kidogo na hatimaye kuwatumbukiza ndani ya dimbwi la maasi bila ya kujijua. Mfano mwengine ni wa Muislamu mwenye kusimamisha Swalaah tano. Ibilisi huanza kumuondoshea hamu ya kufika Masjid mapema, baadaye humshughulisha ili asipate kuswali, huendelea kwa kuswali nyumbani na hatimaye huacha kabisa.

 

Maandishi ya SW kusimama kwa Subhaanahu wa Ta’aalaa na SAW kuelezea Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam ni mambo mengine ambayo hapana budi kuyafikiria vizuri. Kwa hali hii, haitokuwa ajabu kuona kizazi kinachofuata kikitamka: Allaah Ess Dabal Yuu (SW) au Nabiy Ess Eee Dabal Yuu (SAW).

 

Halikadhalika, mambo ya kusherehekea birthday hayana mnasaba ndani ya Diyn hii tukufu. Wanaswara wanayo birthday ya Yesu (Krismasi), Waislamu nao wakaweka birthday ya Nabiy! Laa hawla! Jina la birthday likabadilishwa ili lipate lafdhi zile za Kiarabu na kuitwa Mawlid. Kwa mtindo huu, ndio tunaona sasa hata Waislamu hawaelewi kufunga Jumatatu wala Alkhamisi, Sunnah za Swalah ya dhuhaa na witri zote kaachiwa mwenyewe Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wanasubiri Mfunguo sita waende kusoma hayo Mawlidi wakielewa kuwa ndio kumtukuza kipenzi chetu.

 

Yeye Ibilisi hamuachi mtu hadi mauti yamfike. Hivyo, haifai kusema kwamba ‘nitatubu baadaye’ au ‘nitaanza kuvaa hijabu nikifika umri kadhaa’. Kwani tunashuhudia ndani ya jamii zetu kizee cha kupindukia miaka 85 kikiwa kinaimba kwa matusi ya juu na kunywa pombe mithili ya kijana wa miaka 20!

  

Vipi tutaepukana naye?

 

Kuna njia mbili kuu za kuepukana na Ibilisi ambazo ni:

Kwanza ni kufuata amri za Allaah. Hii ni pamoja na kukumbuka wasia wa Rabb Mlezi wa kutomfuata Ibilisi na badala yake kumuabudia Yeye pekee kwani hii ndiyo njia iliyonyoka:

 

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٦٠﴾ وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦١﴾

 

Je, Sijakukuahidini enyi wana wa Aadam kwamba: Msimwabudu shaytwaan, hakika yeye kwenu ni adui bayana! Na kwamba Niabuduni Mimi? Hii ndio njia iliyonyooka. [Yaasiyn: 60-61]

 

Pili ni kushikamana kwa hali zote katika mwendo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Makhalifa wake waadilifu:

 

"... Basi shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa wangu waongofu, kamataneni nazo kwa magego (shikamaneni nazo kwa nguvu zote)" [Abu Daawuud 4607, At-Tirmidhy 2676 Nayo ni Hadiyth Nzuri Sahihi]

 

Huyo ndie Ibilisi ambaye Radhi za Allaah zipo mbali na yeye. Athari ya kumfuata Ibilisi ni mbaya mno, kwani hutuwekea kizuizi baina yetu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na kila mwenye kumfuata yeye ataelekea kwenye njia potofu.

 

 

 

Share