Kumgharimia Mtu Hijjah Kabla Ya Kufanya Mwenyewe Inafaa?
Kumgharimia Mtu Hijjah Kabla Ya Kufanya Mwenyewe Inafaa?
Swali:
Assalam alaykum warahmattullah wabarakatuh.
Mimi ni mwanamke nilioolewa, ninahamu ya kwenda kumhijia bibi yangu ambae amefariki, swali langu je hajj itakubaliwa wakati mimi mwenyewe sijwahi kwenda hajj, nategemea kutoa gharama ya nauli ya hajj kwa mjomba wangu ambae na yeye hajawahi kuhiji ili akamuhije huyo bibi yangu ambae yeye atakuwa mama yake, mama yangu ameshaenda hajj ikiwa huyo mjomba wangu hawezi kwenda je mama yangu anaweza kwenda. Matumaini yangu mtaelewa hayo mazingira ili mnijibu swali kwa ufasaha zaidi. Assalam alaykum
Jibu:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Inatakiwa tufahamu kuwa Hijjah imewekewa Waislamu wenye uwezo wa kwenda kwa kutoa gharama. Kama machimbuko ya Uislamu yanavyo tueleza. Kuhusu hilo Allaah Aliyetukuka Anasema:
فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ
Ndani yake kuna Aayaat (ishara, dalili) zilizo wazi; mahali pa kisimamo cha Ibraahiym. Na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. [Al-'Imraan: : 97].
Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuambia hayo hayo: "Na kuhiji katika Nyumba kwa mwenye uwezo" [Muslim].
Ikiwa bibi yako hakuhiji kwa kutokuwa na uwezo basi ilikuwa si faradhi kwake. Lau angekuwa na mali na hakuhiji basi mgetenga katika mali yake ya kutumwa mtu kumhijia kabla kugawa urathi.
Ama mas-alah ya Hijjah mtu hawezi kumhijia mwenziwe hata akiwa ni mzazi wake kabla ya yeye mwenyewe kutekeleza faradhi hiyo. Hivyo, kwako imekuwa ni faradhi kuhiji si bibi yako wala mjomba wako. Na wewe au mjombako hamuwezi kumhijia bibi kwa kuwa nyinyi wewe hamjatekeleza hilo. Na ikiwa wewe una uwezo wa kuhiji basi inatakiwa mwanzo utumie pesa hizo kwenda wewe, na baada ya kwenda wewe kuhiji ukapata pesa nyingine unaweza kumpatia mamako akamhijie bibi yako, au wewe mwenyewe kufanya hivyo wakati huo.
Na suala hilo ni sahali wala lisikukere, bibi yako kwa kutokwenda hana madhambi mbali na kwamba niyyah yako ni nzuri Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atakulipa kwa niyyah yako. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie uende ukahiji na pia Akufanyie wepesi wa kumhijia bibi yako.
Na Allaah Anajua zaidi