Anataka Kuzini Kabla Ya Ramadhaan. Je Swawm Yake Itakubaliwa?

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum,

swali: siko katika ndoa, na ninafahamu kuwa sitakiwi kuzini.Je, ni kweli kwamba nikiingiliana na mwanamume mfano siku tatu kabla ya ramadhan,funga yangu hata pokelewa mpaka siku thelathini zipite?

 

 


JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukurani kwa swali lako hili la mtu kuzini kabla ya Ramadhaan.

 

 

Ni makosa, makubwa, bali ni dhambi Muislamu kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan kwa maasi badala ya vitendo vyema. Tunaona kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuwekea mwezi mtukufu wa Rajab, kisha mwezi wa Sha'abaan ambayo yote ni faida kwetu kujitayarisha na vitendo vyema kuupokea mwezi wa Ramadhaan. Lakini ni jambo la kusitikisha sana kuona kwamba ndugu zetu wengine hufanya kinyume chake; wengine kuukaribisha kwa kama inavyojulikana 'vunja jungu', na humo wengine ima huingia katika mambo ya munkaraat kama michanganyiko wa wanawake na wanaume kwenda mandarini (picnics), wengine kufanya maparty ya muziki na wengine hufika hadi kutenda maasi ya kulewa au kuzini kama ilivyo hali ya muulizaji.

 

 

Ikiwa jambo hili limekwishatokea, hivyo linaulizwa tu kuhusu funga ya mtu huyo, naye akarudi kutubu kwa Mola wake, basi funga hiyo itakuwa sahihi na Allaah ni Mwingi wa Msamaha. Lakini ikiwa jambo hilo umelitilia nia, tunakupa nasaha za dhati ujiepushe nalo haraka kwa kubadilisha nia yako na badala yake uukaribishe mwezi wa Ramadhaan kwa vitendo vyema, kwa sababu, binaadamu hatuna uhakika kama tutaishi hadi kufika Ramadhaan, au mwezi kabla yake, au wiki, au siku au hata saa moja. Je, umewaza ndugu kuwa huenda mauti yakakuta wakati uko katika maasi hayo? Je, hutambui kwamba mja hufufuliwa akiwa katika hali aliyoondokea? Je, hufikiri kwamba huenda mauti yakakufika na huku umetia nia hiyo? 

  

 

Tunakupa nasaha ujiepushe kabisa na jambo hilo na mche Mola wako. Bbadilisha nia yako hiyo na  weka nia ya kutenda vitendo vyema vya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Soma makala na sikiliza mawaidha yafuatayo yakusaidie kujiepusha na maasi hayo haraka.

 

 

 Binti Mwenye Kufanya Maasi Ya Zinaa

 

 

Nakaribia Kuzini Na Shemeji, Je, Nifanyeje Kujiepusha Na Vipi Nitahukumiwa Na Allaah?

 

 

Nakaribia Kuzini na Mke wa Ndugu Yangu Vipi Nijiokoe?

 

 

Kufanya Mapenzi Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Kwa Ambaye Hajaolewa?

 

 

Ubaya Wa Zinaa

 

 

Adhabu za kilimwengu za wazinifu

 

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

 

 

 

 

Share