025-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kisomo Chake (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Swalah Za Alasiri, Maghrib Na 'Ishaa
1- SWALAH YA ALASIRI
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma katika Rakaa mbili za mwanzo al-Faatihah na Surah mbili, hurefusha Rakaa ya kwanza kuliko ya pili([1]) na walikuwa wakidhani kuwa alikuwa akifanya hivyo ili watu waweze kuidiriki Rakaa ya mwanzo.([2])
Alikuwa akisoma kadiri ya Aayah kumi na tano katika kila Rakaa mbili za mwanzo, kiasi cha nusu ya kisomo alichokuwa akisoma katika Rakaa mbili za mwanzo za Swalah ya Adhuhuri, na alikuwa akizifupisha Rakaa mbili za mwisho kiasi cha nusu ya urefu wa Rakaa mbili za mwanzo.([3])
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma al-Faatihah katika Rakaa mbili za mwisho.([4]) Alikuwa akiwasikilizisha Aayaah (au zaidi) mara nyingine([5]), na alikuwa akisoma Surah tulizozitaja hapo nyuma katika Swalah ya Adhuhuri.
2- SWALAH YA MAGHRIB
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma katika Swalah hii – baadhi ya nyakati -Surah fupi za Mufasswal([6]), kiasi cha “wao wanapomaliza kuswali naye, huondoka mmoja wao, na hakika mtu (angeweza kuutupa na) kuona sehemu iliyoangukia mshale wake.”([7]).
Na (Mara moja), alipokuwa safarini alisoma:
((وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ))
((Naapa kwa tini na zaytuni!)) [At-Tiyn 95:8) katika Rakaa ya pili.([8])
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) mara nyingine akisoma Surah ndefu za Mufasswal na za wasitani, hivyo alikuwa akisoma:
الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّهِ
((Waliokufuru na wakazuilia njia ya Allaah)). [Muhammad 47: 1].([9])
Mara nyingine akisoma Suratu-Twuur [52: 49]([10])
Na mara nyingine akisoma Suratul-Mursalaat [77: 50] ambayo aliisoma katika Swalah (yake) ya mwisho aliyoiswali (صلى الله عليه وآله وسلم).([11])
Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma moja kati ya Surah mbili ndefu (atw-Twuwlayayn)([12]); [Al-A'araaf 7: 206] (katika Rakaa mbili).([13]) Na mara nyingine akisoma Al-anfaal [8: 75] katika Rakaa mbili.([14])
KISOMO KATIKA SUNNAH (BAADA YA SWALAH) YA MAGHARIBI
Ama katika Sunnah ya baada (al-ba’diyyah) ya Maghrib, alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma:
((قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ))
((Sema: Enyi makafiri!)). [Al-Kaafiruun 109: 6], na
((قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ))
((Sema: Yeye Allaah ni wa Pekee)). [Al-Ikhlaasw 112: 4].([15])
3- SWALAH YA 'ISHAA
Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Surah za kati na kati za Mufasswal katika Rakaa mbili za mwanzo([16]), hivyo alikuwa mara nyingine akisoma:
((وَالشَّمْسِ وَضُحَاهَا))
((Naapa kwa jua na mwangaza wake!)) [Ash-Shams 91: 15] na Surah nyingine zilizofanana na hiyo([17]).
Na mara nyingine alikuwa akisoma:
((إِذَا السَّمَاء انشَقَّتْ))
((Itapochanika mbingu)) [Al-Inshiqaaq 84: 25), na alikuwa akileta Sajdah humo([18]).
Pia mara moja alipokuwa safarini alisoma:
((وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ))
((Naapa kwa tini na zaytuni!)) [At-Tiyn 95:8) (katika Rakaa ya mwanzo).([19])
Alikataza (صلى الله عليه وآله وسلم) kurefusha kisomo katika 'Ishaa, katazo hili lilikuja wakati Mu'aadh bin Jabal alipowaswalisha watu wake Swalah ya 'Ishaa akaifanya ndefu, akajiondoa mtu mmoja katika Answaar na kuswali pekee. Mu'aadh akaelezwa habari ya mtu huyo akasema: "Hakika yeye ni mnafiki". Mtu yule ilipomfikilia taarifa, alikwenda kwa Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumweleza vile alivyosema Mu'aadh. Basi hapo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)akamwambia Mu'aadh: ((Je, unataka kuwa mfitini ewe Mu'aadh? Utaposwalisha watu basi soma:
((وَالشَّمْسِ وَضُحَاهَا))
((Naapa kwa jua na mwangaza wake!)) [Ash-Shams 91: 15], na
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى
((Litakase Jina la Mola wako Aliye juu kabisa)) [Al-A'laa 87: 19], na
((وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَى))
((Naapa kwa usiku unapofunika!)) [Al-Layl 92: 21] [Bila ya shaka huswali nyuma yako watu wazima, wagonjwa na wenye haja zao].[20])
[1] Al-Bukhaariy na Muslim.
[2] Abu Daawuud ikiwa na isnaad Swahiyh na Ibn Khuzaymah.
[3] Ahmad na Muslim.
[4] Al-Bukhaariy na Muslim.
[5] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[6] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[7] An-Nasaaiy na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[8] Atw-Twayaalisy na Ahmad katika isnaad Swahiyh.
[9] Ibn Khuzaymah (1/166/2), Atw-Twabaraaniy na Al-Maqdisiy ikiwa na isnaad Swahiyh.
[10] Al-Bukhaariy na Muslim.
[11] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[12] At-twuulayayn ni Al-A'raaf [7] kwa makubaliano, na Al-an'aam [6] kutokana na kauli iliyo sahihi zaidi kama ilivyotajwa katika Fat-h al-Baariy.
[13] Al-Bukhaariy, Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (1/68/1), Ahmad, Siraaj na Mukhlisw.
[14] Atw-Twabaraaniy katika Mu'jam Al-Kabiyr ikiwa na isnaad Swahiyh.
[15] Ahmad, Al-Maqdisiy, An-Nasaaiy, Ibn Naswr na Atw-Twabaraaniy.
[16] An-Nasaaiy na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.
[17] Ahmad na At-Tirmidhy ambaye amekiri ni nzuri.
[18] Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy.
[19] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.
[20] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni. Imetolewa pia katika Al-Irwaa (295).