Mtu Mwenye Majivuno Atasamehewa?

 

Mtu Mwenye Majivuno Atasamehewa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Swali:

 

Assalam alaykum

 

Kwanza napenda kumshukuru Allaah kwa kuniweza kupata nafasi hii ya kuweza kuuliza maswali na kutujaalia kuwa na maustadh ambao wanajitolea kuelimisha jamii ya kiislamu. Swali langu lilikuwa je mtu akiwa ana swali, anatoa zaka, na anafanya ibada nyingine lakini mtu huyo huyo anatokea mtu wenye majivuno je Allaah anaweza kumsamehe. Au hato msamehe kama hajaomba msamaha. Kama kumbukumbu zangu ziko sawa basi nakumbuka kusoma aya ambayo inasema kuwa Allah atawasamehe na atawafutia waumini walio tenda wema makosa yao  kwa kuwa wamefuata haki. Lakini pia kuna aya ambayo inasema.

 

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahanam wadhalilike.  [Ghaafir: 60]

 

Katika aya inaonyesha ubaya wa kujivuna. Swali langu la pili ni je majivuno yanaweza kuharibu amali zote za mtu na hatimaye ikamwingiza motoni? Na je kama umejevuna bila kujua au kukusudia je utakuwa na dhambi? Hayo ndio maswali yaliokuwa yanatatiza. Asante kwa muda wako wala mimi sina uwezo wa kulipa kwa juhudi zako juu ya kuwasaidia watu kuelekea kwa Allah ila mwenyewe Allaah.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ni kitu kilicho wazi kuwa kosa lolote ambalo mwanadamu na hasa Muislamu analofanya ni lazima aombe msamaha. Na anapoomba msamaha ni lazima atimize masharti ya toba. Wamesema wanavyuoni:

 

"Toba ni wajibu kwa kila dhambi. Ikiwa dhambi aliyoifanya mja ni baina mja na Allaah aliyetukuka haiingiliani na haki ya binadamu,  itakuwa na sharti tatu:

 

Ya kwanza: Kuacha maasiya.

Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.

Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele.

Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi".

 

 

Na ikiwa dhambi iliyofanywa  ina mafungamano na mwanaadamu sharti za kupata toba zinakuwa ni nne: Sharti hizo tatu zilizotajwa hapo juu na ya nne ni kuirudisha haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie. Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Hii aya ambayo umeitoa inafanana na aya mbili katika Suratun Nisaa’ ambazo zina maana zifuatazo:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48].

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116].

 

 

Lakini katika mas-ala haya, Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuweka wazi kuwa Yeye Anasamehe madhambi yote na wala tusikate tamaa katika hilo kwani Yeye Ametuahidi pale Aliposema:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ﴿٥٤﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. Na rudini kila mara kutubu kwa Rabb wenu na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa. [Az-Zumar: 53 – 54].

 

 

Hivyo, maadamu mtu atatubia kikweli kweli basi atasamehewa. Ikiwa dhambi kubwa zaidi ambayo ni shirki husamehewa mtu seuze majivuno.

 

 

Hakika kwa mwenye kutaka msamaha wa kweli basi hata madhambi yake hubadilishwa na (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa mema pindi anapojibadilisha na kutenda yaliyo mema. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:  

 

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli. [Al-Furqaan: 70 – 71].

 

 

Hakika kujivuna ni jambo ambalo limekatazwa kabisa katika Uislamu. Hili ni kosa ambalo linaharibu mema ya Muislamu na wanaadamu, hivyo tufanye juhudi katika kujitoa katika kosa hilo. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, "Allah Aliyetukuka amesema: ((Kibri ni vazi Langu na utukufu ni vazi Langu la chini na Nitamtia motoni yeyote anayeshindana Nami katika moja ya hivyo viwili)) [Abu Daawuud kutoka kwa Abu Hurayrah  (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Na amesema tena: ((Mtu mmoja alipokuwa anatembea, huku anaburuza nguo yake kwa kibri, alifanywa amezwe na ardhi na ataendelea kudidimia ndani yake mpaka Siku ya Kiyama)) [Al-Bukhaariy kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)].

 

Na amesema tena (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Allah Hatomwangalia mja Siku ya Kiyama kwa sababu ya kuburuza nguo yake kwa kibri))  [Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)]  

 

Na amesema tena: ((Yeyote atakaye kufa bila ya kuwa na kibri, utovu wa uaminifu katika ngawira na deni ataingia peponi)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy kutoka kwa Thawbaan (Radhwiya Allaahu 'anhu)].

 

Na amesema tena: ((Yeyote mwenye chembe ndogo ya kibri katika moyo wake hataingia peponi)) [Muslim kutoka kwa Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu 'anhu)].   

 

 

Na zipo aayah nyingi zinazoelezea kuhusu kibri na sifa hiyo inaharibu 'amali kabisa na hivyo kumuingiza mtu motoni.

 

 

Ikiwa umekuwa na sifa hiyo bila ya kujua Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakusamehe lakini pindi unapofahamu na kujua hilo inabidi ufanye juhudi kubwa kuiacha tabia hiyo. Allah Anasema:

 

إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾

Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Maaidah: 17].

 

Twatumai tutakuwa tumejibu maswali yako yote.

 

 

Na  Allaah Anajua zaidi.

 

Share